MWANAJESHI NA WENZAKE WATATU WAHUKUMIWA KWA KULAWITI NA KUSAMBAZA VIDEO

 Watuhumiwa wa Kulawiti na Kusambaza Video za Unyanyasaji Kijinsia Wahukumiwa Miaka 30 Jela


Mtwara, April 9, 2024 - Jeshi l⁹a Polisi Mkoa wa Mtwara limefanikiwa kuwapeleka gerezani watuhumiwa wanne, akiwemo aliyekuwa Askari wa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWT), Shaibu Yusuph Saidi (MT.95850), baada ya kufanya uhalifu mbaya wa kulawiti na kumpiga picha mhanga wakati wa tukio hilo la kinyama.


Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mtwara, SACP Issa J. Suleiman, amethibitisha kwamba watuhumiwa hao walihukumiwa miaka 30 jela baada ya kukatwa rufaa katika Mahakama Kuu Kanda ya Mtwara. Awali, watuhumiwa hao walipewa adhabu ya kulipa faini ya Tsh milioni moja katika Mahakama ya Wilaya ya Mtwara, lakini upande wa Jamhuri ulikata rufaa kwa madai ya adhabu hiyo kutokuwa kali ya kutosha.


Kesi hiyo iliyogonga vichwa vya habari ilianza kuchukua sura mpya baada ya video ya unyanyasaji huo kusambazwa kwenye mitandao ya kijamii, ikionyesha mateso makubwa aliyopitia mhanga. Kufuatia hatua za haraka za Jeshi la Polisi, haki imeweza kutendeka kwa kuhakikisha watuhumiwa hao wanatumikia adhabu stahiki kwa uhalifu wao.


Kamanda Suleiman amewataka wananchi kutoa ushirikiano kwa vyombo vya sheria katika kupambana na matukio ya unyanyasaji kijinsia na kuhakikisha kwamba wahusika wanawajibishwa kikamilifu kwa mujibu wa sheria. Aidha, amesisitiza umuhimu wa kutunza usalama wa mitandaoni na kutoa wito kwa jamii kujenga uelewa wa kutosha kuhusu madhara ya matumizi mabaya ya teknolojia katika kufanya uhalifu.


Kufuatia hukumu hii, jamii ina matumaini kuwa hatua kama hizi zitatoa fundisho kwa wanaotenda au kufikiria kufanya vitendo vya unyanyasaji kijinsia na kwamba haki itawafikia wahanga wote wa uhalifu huo. Jeshi la Polisi Mkoa wa Mtwara linaahidi kuendelea kufanya kazi kwa bidii ili kuhakikisha kuwa jamii inakuwa salama na inaishi kwa amani na utulivu.


0 Comments:

Post a Comment