RAIS SAMIA MGENI RASMI JUKWAA LA KODI KITAIFA FEBUARI 27 HADI 28 JIJINI DAR ES SALAAM

 RAIS SAMIA MGENI RASMI JUKWAA LA KODI KITAIFA FEBUARI 27 HADI 28 JIJINI DAR ES SALAAM


Happy Lazaro,Arusha.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika Jukwaa la Kodi kitaifa lililoandaliwa na Wizara ya Fedha kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji pamoja na Sekta Binafsi linalotarajiwa kukutanisha wadau mbalimbali wa kodi.




Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Elijah Mwandumbya, ameyasema hayo wakati  akizungumza na waandishi wa Habari jijini Arusha, katika ukumbi wa Hazina Ndogo, kuhusu Jukwaa la Kodi na Uwekezaji Kitaifa 2024  katika ukumbi wa Kimataifa wa Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam.




‘’Serikali imeshirikisha Sekta Binafsi katika hatua zote za maandalizi ikijumuisha ziara za Kikanda ambazo zilifanyika kuanzia tarehe 20 Novemba, 2023 hadi tarehe 07 Desemba, 2023 katika Kanda za Kaskazini (Arusha), Kanda ya ziwa (Mwanza na Shinyanga), Kanda ya Magharibi (Kigoma), Kanda ya Nyanda za Juu Kusini (Mbeya), na Kanda ya Kusini (Mtwara)’’, alisema  Mwandumbya.



Alisema kuwa Wizara ya Fedha ina jukumu la kuratibu upatikanaji wa maoni ya wadau, kuchakata maoni hayo na hatimaye kuwasilisha kwenye Kamati ya Ushauri wa Kodi mapendekezo mbalimbali ya sera za kodi yanayotarajiwa kufanyika katika mwaka wa fedha unaofuata.



‘’Kila mwaka Kamati hii imekuwa ikipokea maoni ya wadau, kufanya uchambuzi, na kufanikisha majadiliano ya masuala mbalimbali yanayohusiana na sera za kodi na usimamizi wake ambayo yamekuwa na mchango mkubwa kwetu waandaa sera na yamesaidia katika kuunda mfumo wa kodi ambao umewezesha utatuzi wa masuala mbalimbali ya kodi kwa ufanisi na uwazi’’, alifafanua Mwandumbya.



Mwandumbya aliongeza kuwa katika kupanua wigo wa kupata maoni ya wadau, Wizara ya Fedha ilianzisha Jukwaa la Kodi Kitaifa (National Tax Forum) mwaka 2023, ambalo kwa mara ya kwanza lilifanyika tarehe 11 Januari 2023, Jijini Dar es salaam, ambalo maoni yaliyopokelewa yalitumika katika maandalizi ya Bajeti Kuu ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2023/24 inayotekelezwa hivi sasa.


Alifafanua kuwa Jukwaa hilo limeongeza ushirikishwaji wa sekta binafsi katika maandalizi ya Bajeti Kuu ya Serikali ambapo maoni yaliyotolewa yalilenga kuboresha mazingira ya ufanyaji biashara na uwekezaji, kulinda viwanda vya ndani, kuvutia uwekezaji nchini na kuongeza ushindani wa viwanda vya ndani.



Aidha, Mwandumbya alitoa rai kwa wananchi kutumia fursa iliyotolewa na Serikali kwa kila mmoja kutoa maoni na kuwasilisha mapendekezo yake ya kuboresha sera za kodi na uwekezaji kupitia dirisha la kidigitali kwa ku-scan QR code iliyoambatishwa kwenye tangazo ambalo tayari linasambazwa kupitia mitandao ya kijamii.



Kauli Mbiu ya Jukwaa la Kodi na Uwekezaji Kitaifa mwaka huu ni " Mageuzi ya Sera za Uwekezaji, Ukusanyaji wa Mapato ya Ndani na Ukuaji wa Uchumi Jumuishi’’.




0 Comments:

Post a Comment