Hukumu ya Kesi ya Mke wa bilione Msuya kutolewa leo

Hukumu ya Kesi ya Mke wa bilione Msuya kutolewa leo



Hukumu ya kesi ya mauaji inayomkabili Miriam Steven Mrita, mjane wa aliyekuwa mfanyabiashara maarufu wa madini mkoani Arusha, bilionea Erasto Msuya, inatarajiwa kutolewa leo na Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam. Kesi hii, ambayo imekuwa ikiendelea kwa miaka minane sasa, inamhusisha Miriam pamoja na mshitakiwa mwenzake, Revocatus Everist Muyella, maarufu kama Ray, ambao wanadaiwa kumuua kwa kumchinja, Aneth Elisaria Msuya, wifi ya Miriam.


Tukio hili la kusikitisha lilitokea Mei 26, 2016, huko nyumbani kwa Aneth, Kibada Kigamboni jijini Dar es Salaam. Aneth, ambaye alikuwa mdogo wa marehemu bilionea Erasto Msuya, alipoteza maisha yake kikatili katika tukio hilo la mauaji ya kukusudia. Kufuatia tukio hili, Miriam na Ray wamekuwa wakisubiri hukumu huku wakiwa mahabusu.


Kukumbuka historia ya kesi hii, bilionea Erasto Msuya pia alifariki kwa njia ya kutatanisha baada ya kuuawa kwa kupigwa risasi kwa kutumia bunduki ya kivita aina ya SMG, eneo la Mijohoroni, Barabara Kuu ya Moshi-Arusha wilayani Hai, Mkoa wa Kilimanjaro, Agosti 7, 2013. Kifo chake kilizua maswali mengi na kutia doa kwenye taswira ya amani katika jamii.


Hukumu hii inayotarajiwa kusomwa na Jaji Edwin Kakolaki itakuwa muhimu sana kwa familia za marehemu na washitakiwa wenyewe. Kwa mujibu wa sheria za nchi, iwapo watapatikana na hatia, adhabu inayotolewa kwa mauaji ya kukusudia ni kunyongwa hadi kufa. Hata hivyo, iwapo watapatikana hawana hatia, wanaweza kuachiwa huru.

0 Comments:

Post a Comment