BOT Yatoa Onyo Kuhusu Matumizi ya Mawakala na Washauri Elekezi



Leo, Benki Kuu ya Tanzania imewaonya umma na wadau wa sekta ya fedha kuhusu matumizi yasiyo sahihi ya mawakala na washauri elekezi wakati wa kuomba leseni au usajili. Taarifa iliyotolewa na Benki Kuu inaeleza kuwa kumekuwa na ongezeko la taasisi na watu binafsi wanaojitangaza kutoa huduma ya kusaidia waombaji kupata leseni katika maeneo mbalimbali ya sekta ya fedha.


Benki Kuu imesisitiza kwamba haina utaratibu wa kuwataka waombaji kutumia mawakala au washauri elekezi katika mchakato wa uandaaji na uwasilishaji wa maombi ya leseni. Aidha, taarifa hiyo imewataka washauri kutoa taarifa sahihi kuhusu gharama za huduma zao na kuzitofautisha na gharama za leseni za Benki Kuu.


Viwango vya mitaji na gharama za maombi ya leseni kwa taasisi mbalimbali, ikiwa ni pamoja na benki, maduka ya kubadilisha fedha za kigeni, na watoa huduma ndogo za fedha, vimeainishwa kwa mujibu wa sheria na kanuni za sekta ya fedha. Benki Kuu imesisitiza kuwa malipo ya leseni yanafanywa moja kwa moja katika akaunti ya Benki Kuu na hayapaswi kuhusisha gharama za washauri.


Wadau wote wa sekta ya fedha wametakiwa kufuata taratibu na miongozo iliyotolewa na Benki Kuu wakati wa mchakato wa kupata leseni au usajili. Taarifa zaidi inapatikana kwenye tovuti ya Benki Kuu au kwa mawasiliano moja kwa moja kupitia simu au barua pepe.



0 Comments:

Post a Comment