MAJALIWA AKUTANA NA WAFANYAKAZI WA UBALOZI WA TANZANIA NCHINI ITALIA

 


Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amekutana na kufanya mazungumzo na watumishi wa ofisi ya Ubalozi wa Tanzania nchini Italia. Mazungumzo hayo yamejikita katika kuimarisha mahusiano ya kihistoria yaliyopo kati ya Tanzania na Italia.


Majaliwa ameeleza kuwa Tanzania inaendelea kutekeleza miradi ya maendeleo katika sekta mbalimbali ikiwemo kilimo, elimu, mifugo, na afya. Hivyo, aliwahimiza wafanyakazi wa ubalozi kuendelea kufanya kazi kwa bidii, weledi, na kutangaza fursa zilizopo nchini ili Taifa linufaike na uwepo wao nchini Italia.


Akizungumza jana (Jumanne, Oktoba 17, 2023) wakati wa ziara yake kwenye Ubalozi wa Tanzania nchini Italia jijini Rome, Waziri Mkuu alimwakilisha Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika Mkutano wa Jukwaa la Kimataifa la Chakula Duniani unaofanyika kuanzia Oktoba 16 hadi Oktoba 20, 2023.


Majaliwa aliwahimiza wafanyakazi wa ubalozi kuendelea kuwaunganisha Watanzania wote wanaoishi nchini Italia na sehemu nyingine zinazohudumiwa na ubalozi huo. Aidha, aliwataka kuendelea kufundisha lugha ya Kiswahili kupitia darasa lililoanzishwa kwani ni fursa muhimu ya kulitangaza Taifa na utamaduni wetu.


Balozi wa Tanzania nchini Italia,  Mahmoud Thabit Kombo, alimshukuru Waziri Mkuu kwa ziara yake na maelekezo aliyo toa. Aliahidi kuwa watafuatilia maelekezo hayo kwa lengo la kuchangia maendeleo ya Taifa.


Tanzania na Italia zina ushirikiano wa kimaendeleo tangu kuanzishwa kwa uhusiano rasmi wa kidiplomasia. Tanzania ilifungua Ubalozi wake mjini Roma mwaka 1972, na Ubalozi wa Italia nchini Tanzania ulifunguliwa rasmi mwaka 1961. Huu ni ushirikiano unaolenga kuleta maendeleo na kuimarisha uhusiano baina ya nchi hizi mbili.

0 Comments:

Post a Comment