MADEREVA WA MALORI WATAKIWA KUCHUKUA TAHADHARI MAAMBUKIZI YA VVU

Na Mwandishi wetu- Singida


MADEREVA wa magari yaendayo masafa marefu ndani na nje ya Nchi wamehimizwa kuchukua tahadhari dhidi ya maambukizi ya virusi vya UKIMWI wakati wote wanaofanya shughuli zao za usafirishaji pamoja na kujenga utamaduni wa kupima afya zao ili kuanza matumizi ya dawa mapema pindi watakapogundulik kuwa na maambukizi hayo.




Hayo yamesemwa na Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu, Ummy Nderiananga wakati akizungumza na madereva wa malori wanaoegesha malori hayo katika Kijiji cha Majengo, pamoja na kukagua Kituo cha Maarifa ya UKIMWI Halmashauri ya Wilaya ya Manyoni mkoani Singida akiwa ameambatana  na  Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Masuala ya Afya na UKIMWI tarehe 10 Oktoba, 2023. .


Ummy amesema lengo la kufika katika kituo hicho ni kuzungumza na madereva hao akisema wako katika hatari kubwa ya kupata maambukizi ya Virusi vya UKIMWI Kutokana na shughuli zao za masafa marefu pamoja na kukagua huduma za kiafya zinazotolewa kituoni hapo.


“Nipende kuwakumbusha na kuwasisitiza mjitokeze mpime afya zenu ili mjue mko katika hali gani, tunatambua kulingana na kazi zenu mnatembea umbali mrefu na mnaenda maeneo mengi kama mikoani na nje ya Nchi kwahiyo mko hatarini  kupata maambukizi mapya ya virusi vya UKIMWI na niwaombe mtumie kituo hiki cha Maarifa kupata elimu ya UKIMWI na magonjwa mengine ili muwe salama,” Amesema Ummy.


Aidha Naibu Waziri huyo amewakumbusha kuendelea na matumizi ya dawa kwa watu wanaoishi na virusi vya UKIWMI ili kuimarisha kinga ya mwili, kujiepusha na magonjwa nyemelezi ili waweze kufanya shughuli zao za kiuchumi wakiwa imara kiafya huku akiisisitiza  jamii kutowanyanyapaa watu wanaoishi na Virusi vya UKIMWI na badala yake kuwaonesha upendo, kuwajali  na kuwashirikisha katika shughuli za maendeleo.



Aidha akisoma taarifa ya Kituo hicho mbele ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Masuala ya Afya na UKIMWI Mratibu wa UKIMWI Halmashauri ya Wilaya ya Manyoni Dkt. Ainea Mlewa amebainisha kuwa hali ya upimaji kuanzia  mwezi Julai 2022 hadi Septemba 2023 jumla ya  madereva wa malori waliojitokeza kupima  maambukizi ya VVU ni 684 waliogundulika na maambukizi  wakiwa ni 19 kati yao 15 ni wanawake  wakati wanaume wakiwa ni wanne ambapo waliunganishwa katika Kliniki ya tiba na mafunzo.


 “Malengo ya mradi ni kuhamasisha wananchi kupima bila uoga, kutoa ushauri, kuhamasisha upimaji wa VVU kwa hiari, kuhamasisha upimaji kwa kutumia ushawishi wa mtoa wa huduma, kutoa elimu ya UKIMWI pamoja na matibabu ya magonjwa ya zinaa, kupunguza maambukizi ya VVU kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto, kugawa kinga na elimu ya matumizi yake, elimu kwa vikundi vya WAVIU na elimu sahihi ya matumizi ya dawa za kupunguza makali ya VVU,” Amefafanua Dkt. Mlewa.


(PICHA ZOTE NA OFISI YA WAZIRI MKUU)

0 Comments:

Post a Comment