MAKAMU wa Rais, Dkt Philip Mpango ameipongeza Mamlaka Mamlaka
ya Hifadhi ya Ngorongoro,(NCAA) kwa kuamua kujenga makao makuu yake nje ya
hifadhi hivyo kuonyesha kwa vitendo umuhimu wa kupunguza shughuli za kibinadamu ndani ya
hifadhi kwa uhifadhi endelevu.
Ameyasema hayo leo, Mei 16,2023 wakati akiweka jiwe la msingi
kwenye jengo la makao makuu ya NCAA, linalojengwa kwenye mji wa Karatu.
“Niseme kwa kifupi nimeridhishwa na kazi inayoendelea kampuni ya
ukandarasi inayojenga jengo hili, (kampuni ya China Jiangxi International
Economic and Technical Cooperation Limited) wasimamizi, Wizara
ya Maliasili na Utalii na uongozi mzima wa NCAA,” amesema Profesa, Mpango na
kuongeza
…Nimeangalia nimeona
ujenzi ni bora kabisa na imejengwa mpaka kufika hapa... Kazi nzuri ingawa najua
kazi bado ni kubwa, kukamilisha jengo la utawala, nyumba za kamishina wa
uhifadhi na za wafanyakazi wengine,”.
“ Simamieni kazi hizo
zikamilike kwa wakati na ubora unaotakiwa tunataka kupata thamani ya fedha
katika ujenzi huu.Tunataka kama inawezekana zitumike mali ghafi kutoka hapahapa
nchini mpaka ‘furniture’ (samani) itapendeza sana tukitumia
‘furniture’ zetu za hapahapa nchini,”.
AWAPA NENO WATUMISHI
Dkt Mpango aliwaeleza
watumishi wa NCCA kuwa jengo hilo la makao makuu likapokamilika na kuanza
kulitumia wahakikishe wanalitunza kwa weledi wa hali ya
juu kwa faida ya kizazi cha sasa cha Tanzania, Ulimwengu na vizazi
vijavyo.
“Mtakapopata jengo la
utawala la kisasa na makazi bora natumani itakuwa ni hamasa kwenu watumishi
kufanya kazi kwa ari na ufanisi zaidi hivyo mna dhamana kubwa sana kwa Taifa
rasilimali hizi ambazo Mungu alitupa ni muhimu sana kwa Taifa,” amesisitiza Dkt
Mpango na kuongeza.
….Nachotaka mimi ni
mapinduzi ya kiutendaji, muongeze ufanisi zaidi na muweze kujiendesha
kibiashara nimesikia suala la mapato lakini jitahidini muweze kufanya zaidi
mzidi malengo mliyojiwekea,”.
‘Tunachangamoto ya
jirani zetu wengine ni majangili wengine wanaleta ng’ombe tena wanaleta kutoka
nje ya mipaka yetu ninachowaomba watumishi wa mamlaka lakini pia wananchi
msishirikiane na majangili na niwambe sana muwe macho na jitihada zozote za
kuharibu uhifadhi.”.
MAHUSIANO NA JAMII
Makamu wa Rais,
ameikumbusha NCAA kuisaidia jamii inayowazunguka kwenye eneo hilo jipya la
makao yao makuu kwa kuwakwekea miundo mbinu itakayowasaidia kuendesha shughuli
zao za ufugaji kwa ufanisi zaidi.
“Waliotuzunguka hapa kwa
kiasi kikubwa ni wafugaji bila shaka pia wako na wakulima. Serikali inafanya
juhudi kubwa kuboresha miundombinu ya shule zetu, afya na maji,” amesema Dkt
Mpango na kuongeza .
….Lakini ningependa
nitume ombi mahsusi kwa mamlaka ya Ngorongoro kama sehemu ya kuboresha
mahusiano na jamii muongeze nguvu katika ujenzi wa malambo ya maji kwa ajili ya
mifugo,”.
MCHENGERWA AELEZEA
MATARAJIO
Kwa upande wake Waziri
wa Maliasili na Utalii, Mohamed Mchengerwa amesema kuwa kukamilika na kuanza
kutumika kwa majengo hayo inategemewa
kupunguza gharama za uendeshaji wa NCAA, kuongeza ufanisi na utoaji wa huduma
kwa wateja wao na kupunguza shughuli za kibinadamu ndani ya hifadhi.
Amesema
kuwa zoezi hilo lilienda sambamba na kuhamisha kwa hiari wananchi
waliokuwa ndani ya hifadhi ya Ngorongoro kwenda Msomera mkoani Tanga.
“Hii ni awamu ya kwanza
ya Mradi huu, tunawapongeza sana wajenzi wa mradi huu kampuni ya China
Jiangxi International Economic and Technical Cooperation Limited kwa
kwenda kwa spidi nzuri lakini unaokidhi viwango ambavyo wizara tunautegemea,”
amesema Waziri Mchengerwa na kuongeza.
…Kwa sasa hivi ujenzi
uko zaidi ya asilimia 35, (wajenzi) wameahidi ifikapo mwezi Oktoba utakuwa
umekamilika na ofisi zitakuwa zimefunguliwa. Tunategemea mkandarasi
atakamilisha ujenzi wake kama ambavyo ametuahidi,”.
UJENZI KUGHARIMU ZAIDI
YA BILIONI 10.4
Kwa upande wake, Kamishina Msaidizi Mwandamizi wa Uhifadhi,
NCAA, Elibariki Bajuta amesema kuwa ujenzi huo unatekelezwa na
kampuni ya China Jiangxi International Economic and Technical Cooperation
Limited kwa gharama ya shilingi bilioni 10.4.
Amesema kuwa mkataba wa ujenzi huo ulisainiwa mwezi Agosti mwaka
jana na ujenzi kuanza rasmi oktoba mwaka huohuo ambapo unatarajiwa kukamilika
Oktoba mwaka huu ukijumuisha jengo la utawala na nyumba tatu za makazi ya
Kamishina wa uhifadhi na wasaidizi wake wawili.
Bajuta amesema kuwa kutakuwa na awamu ya pili ya mradi huo
utakaogharimu kiasi cha shilingi bilioni 2.5 ambao utajumuisha ujenzi wa
zahanati, karakana mbalimbali za ujenzi, ufundi seremala na umeme na cafeteria
kuwawezesha wafanyakazi kupata huduma ya chakula.
Pia Ujenzi wa viwanja vya michezo na sehemu ya ukaguzi na
magwaride na shughuli za ukakamavu na sehemu itakayotumika kwa ajili ya malazi
na mapumziko kwa viongozi.
“Chimbuko la
ujenzi huu umetokana na tishio la kutoweka kwa bayoanuwai urithi wa utamaduni
na rasilimali za miamba kunakochangiwa na kuongezeka kwa shughuli za kibinadamu
ongezeko la watu na mifugo pamoja na mimea vamizi ndani ya hifadhi,” amesema
Bajuta na kuongeza.
…Sisi
(NCAA) tuliona ni vema kuondoka ndani ya hifadhi tuje huku na
tuliona ni njia moja ya kupunguza gharama kwa sababu tulikuwa tunaishi Karatu
halafu tunaingia ndani ya hifadhi na kurudi,”.
“Tuliona hiyo itasaidia
shughuli za kibinadamu zifanyike nje ya hifadhi na shughuli za uhifadhi na
utalii zifanyike ndani ya hifadhi,”.
Akizungumzia utendaji wa
NCAA, Bajuta amesema kuwa taasisi hiyo imefanikiwa kukusanya kiasi kikubwa cha
fedha kuliko wakati wowote tokea kuanzishwa kwake.
“Katika kipindi cha
kuanzia Julai,2022 mpaka Aprili, 2023 tumeshapokea jumla ya wageni 612, 252
ambapo wageni 231,181 ni watalii wa ndani na watalii wa nje ni 381,071. Idadi
hii ya watalii imeongezeka kwa asilimia 89 ukilinganisha na mwaka uliopita,”
amesema Bajuta na kuongeza.
…Ongezeko hilo
limechangia kuongezeka kwa mapato ambapo mpaka Mei 9, 2023 tumeshakusanya
shilingi bilioni 163.74 hii ni kiwango kikubwa sana cha fedha ambacho
hakijawahi kukusanywa tangu NCAA kuanzishwa,”.
Kwa upande wake
Mwenyekiti wa Chama cha Mawakala wa Utalii nchini,(TATO), Wilbard Chambulo,
amesema kuwa hatua ya NCAA kujenga makao makuu yake nje ya hifadhi ni uamuzi
sahihi kwani inapunguza msongamano wa magari yaliyokuwa yakiingia hifadhini kwa
shughuli zisizo za utalii.
“ (NCAA) Wanapotoka kule
ndani wameacha nafasi ya uasili (nature) iendelee na pia itasaidia kukuza
uchumi kwa wananchi wa Karatu kwani watapata huduma mbalimbali kutoka kwenye
eneo hili na hata thamani ya vitu vitaongezeka,” amesisitiza Chamburo na
kuongeza
…Ofisi hizi kuwa nje ya
hifadhi imetusaidia hata sisi (Makampuni ya Uwakala wa Utalii) kwa
sababu haitulazimishi kulipia au kupata kibali kama ilivyokuwa ili uweze
kuingia ndani ya hifadhi kwa jili ya kupata huduma za kiofisi. Hii itapunguza
ule msongamano wa magari ya wafanyakazi na sisi ambao hatukuwa tukienda kwa
ajili ya kuingiza watalii bali kufuata ofisi hizi ndani ya hifadhi,”
…Tuwaache magari ya
watalii ndiyo yapite ndani ya hifadhi kwa ajili ya kutalii,”.
0 Comments:
Post a Comment