ANAYEDAIWA KUMNG'OA MKE JINO KWA PLAIZI AFIKISHWA MAHAKAMANI


Isaack Mnyangi (45)Mkazi wa Sombetini Jijini Arusha anayedaiwa kumshambulia na kumng'oa jino moja mke wake Jackline Mkonyi,(38) amefikishwa mahakamani na  kusomewa shtaka moja la shambulio la kudhuru Mwili.



Mshitakuwa huyo ambaye habari zake zilisambaa na kuwa gumzo kwenye mitandao mbalimbali ya kijamii amesomewa mashitaka yake leo Mei 31,2023 mbele ya Hakimu, Jenifa Edward wa mahakama ya wilaya Arusha.

Wakili wa serikali, Charles Kagilwa amemsomea Mnyangi shitaka  hilo kwenye shauri hilo la jinai namba 80/2023,  akisaidiana na  mawakili wa mawakili wa serikali, Godfrey Nungu na Callorine Kasubi,

Imedaiwa mahakamani hapo kuwa mnamo Mei 23 mwaka huu majira ya saa tano usiku katika eneo la Osunyai kwa Diwani jijini Arusha mshtakiwa Mnyangi alimshambulia mke wake  Jackline na kumng'oa jino moja ,kumpiga kwa mkanda usoni na mgongoni na maeneo mengine ya mwili wake na kumsababishia madhara.



Mnyangi amekana kutenda kosa hilo ambapo upande wa jamhuri ulieleza upelelezi wa shauri hilo umekamilika hivyo kuiomba mahakama kumsomea mshatakiwa maelezo ya awali .


Akisoma maelezo ya kosa  kwa mshtakiwa huyo , wakili wa jamhuri Godfrey Nungu amedai mahakamani hapo kuwa mnamo Mei 23, 2023, majira ya saa tano usiku mhanga (Jackline) alisikia mlio wa honi ya gari nje ya geti na alipojaribu kwenda kufungua  alibaini kuwa mtoto wake wa kiume tayari alikuwa ameshafika getini kufungua


Wakili Kagilwa alieleza mahakama kuwa Jackline  aliendelea kumsubiria mshitakiwa, Mnyangi  sebuleni ambapo  mshitakiwa alipoingia ndani hakumsalimia badala yake alipitiliza kuelekea chumbani .


Aliendelea kudai mahakamani hapo kuwa Jackline alimfuata chumbani lakini mshitakiwa alimshika mkono na kumvuta  na kisha kumtupa sebuleni kwenye Kochi .


Kagilwa aliieleza mahakama hiyo kuwa mshitakiwa alianza mke wake, Jackline ngumi usoni na kuendelea kumpiga mateke na kumkanyaga na baadaye alichomoa mkanda wake wa suruale na kuendelea kumpiga  meneo mbalimbali ya mwili wake ikiwemo mgongoni.


Alidai kwamba mshitakiwa alichukua plaizi na kumng'oa jino moja la mbele, ambapo Jackline alitokwa na damu nyingi akiwa hajitambui.


Wakili huyo wa serikali aliendelea kudai kuwa, mshitakiwa, Mnyangi  alimwacha Jackline  akiwa na majeraha makubwa mwilini akiwa anavuja damu nyingi hapo sebuleni na kwenda kuwaamsha watoto na baadaye alimpigia simu mama yake na Mhanga(mama mkwe)na kumweleza kuwa anamleta mtoto wake nyumbani. 


Aliendelea kudai kuwa  mhanga huyo alipakiwa kwenye gari pamoja na watoto na kwenda hadi Sinoni Daraja mbili nyumbani kwa mama mkwe na kumtelekeza na kutoweka kusikojulikana .


Alidai kwamba siku iliyofuata Jackline  alipelekwa hospitali na kushonwa majeraha na daktari alithibitisha kuwa mhanga alikuwa amng'oka jino moja na kutobolewa sehemu ya jicho lake. 


Wakili huyo wa serikali aliieleza mahakama kuwa uchunguzi wa polisi ulifanyika na mtuhumiwa alikamatwa mei 27,2023 akiwa amejificha kwa mchungaji eneo la Himo Mkoani Kilimanjaro na baadaye kufikishwa mahakamani.


Upande wa jamhuri umesema kuwa unatarajia  kuleta mashahidi watano na kielelezo kimoja mahakamani hapo .

JAMHURI YAPINGA DHAMANA KWA MSHITAKIWA

Upande wa jamhuri uliwasilisha maombi madogo ya kupinga dhamana kwa mshtakiwa huyo kwa kile walichoeleza kuwa anaweza kutoroka baada ya tukio na hali ya taharuki kwa wananchi pamoja na kujenga chuki kwa mkewe na watoto.


Hakimu aliahirisha shauri hilo kwa saa moja na aliporejea alitoa uamuzi mdogo huku akikubaliana na ombi la upande wa jamhuri la kumnyima mshtakiwa dhamana kwa siku 14 hadi juni 13 mwala huu.
 


Mshtakiwa, Mnyangi amepelekwa  mahabusu kwenye  gereza la mkoa la Kisongo,Arusha hadi juni 13, 2023 ambapo mahakamaitatoa masharti ya dhamana.

0 Comments:

Post a Comment