MAWAKILI WAVUTANA JUU YA NANI AMEMCHUKUA MZEE OLENG'IYO

MABISHANO makali ya kisheria yameibuka mahakamani juu ya ni wapi alipo na nani anamshikilia Mzee Oriais Pasilange Oleng'iyo,(85) mkazi wa  Ololosokwani tarafa ya Loliondo.


Aidha wakati mawakili wa waleta maombi wakieleza kuwa mzee huyo alikamatwa na polisi  Juni 20,2022 upande wa jamhuri unadai hakuna mtu mwenye jina hilo aliyekamatwa na polisi kati ya juni 9 na 20 2022 huku wakitaka namba ya polisi aliyemkamata au namba ya gari.



Mabishano hayo yameibuka leo Machi 30,2023 mbele ya Jaji Mohamed  Gwae wa mahakama kuu kanda ya Arusha anayesikiliza maombi hayo namna 68/2022 yaliyowasilishwa mahakamani na mtoto wa mzee huyo,  Ndoloi Oriais.


Ndoloi anaiomba mahakama itoe amri kwa wajibu maombi kwa ujumla wao kumleta, kumuachilia au kusema popote alipo Oleng'iyo. 




Kwenye shauri hilo linalovuta hisia za wengi wajibu maombi ni pamoja na Kamanda wa Polisi (RPC) mkoani Arusha, Mkuu mkoa wa Arusha, Mkuu wa wilaya na OCD wa Ngorongoro, Mkuu wa jeshi la polisi(IGP) na Mwanasheria Mkuu wa serikali, (AG).



Wakili wa mleta maombi, Saimon Mbwabo alieleza mahakamani hapo  kuwa  mnamo Juni 9,2022 huko katika kitongoji cha Nailowa kata ya Ololosokwani na kijiji cha Ololosokwani katika tarafa ya Loliondo wilayani Ngorongoro, askari polisi waliokuwa wakitoa ulinzi kwa maafisa wanaoweka alama za mipaka huku zoezi la kuwaamisha  baadhi ya wakazi likiendelea ambapo wananchi  wengine walikuwa wakipinga zoezi hilo kifanyika ndipo yalipotokea machafuko kati ya wananchi na polisi 


Aliieleza kuwa vurugu hizo zilifanyika karibu na makazi ya mzee Oriais baada ya mabishano ya polisi na wananchi wengine yakiendelea walisogea nyumbani kwa Mzee huyo ambaye alikuwa hausiki na vurugu hizo lakini alipigwa na risasi na mmoja wa askari ambaye hakujulikana.


Amesema kuwa mleta maombi, Ndoloi aliyekimbilia eneo la mlimani  kutokana na vurugu hizo akiwa kwenye maficho ya mlimani  ndipo alipomuona Mzee Oriais akichukuliwa na Askari polisi na kuondoka nae akiwa amepata jeraha.


"Hata hivyo pamoja na Mzee Oriais kukamatwa na watu wengine 19  ambao baadhi yao walifikishwa mahakamani kutokana na kukabiliwa na mauaji ya askari polisi Mzee Oriais hakuletwa mahakamani,"ameeleza wakili Mbwambo.


Ameendelea kueleza kuwa   kabla ya hao waliokamatwa kufikishwa mahakamani walikuwa hawajulikani walipo ambapo baada ya siku kadhaa mawakili wao walileta maombi ya kutaka waletwe mahakamani ambapo mmoja wa waliokuwa kwenye maombi hayo ni  Mzee Oriais.



"Waliletwa mahakamani watu 19 lakini Mzee huyo hakuletwa kwenye mahakamani ya hakimu mkazi Arusha ingawa watu waliendelea kuongezwa kidogokidogo hadi kufikia 27 tukiamini katika muendelezo huo pengine mzee huyo angeweza kuletwa,"ameeleza Wakili Mbwambo.


Wakili huyo aliongeza kuwa baada ya upande jamhuri kuondoa mahakamani shauri hilo la mauaji namba 11/2022, mnamo  Novemba 22,2022 ndipo walipogundua kuwa mzee huyo hataletwa tena na ndipo ilipowalazimu kukimbilia mahakamani ili aweze kuletwa kama yupo hai au amefariki.


Ameeleza kuwa wakati  Mzee Oriais anashikiliwa alikuwa eneo la Ololoswokwan hivyo kwa namna yeyote endapo atakuwa ameshikiliwa itakuwa kinyume na kifungu namba 391kifungu kidogo cha kwanza(a)(b) cha sheria ya mwenendo wa makosa ya jinai sura ya 20 kutokana na polisi hawana mamlaka ya kukaa na mtuhumiwa kwa muda wa miezi tisa.


Akijibu hoja hizo kwa niaba ya wajibu maombi,  Wakili wa serikali, Peter Mseti,amepinga maombi hayo kwa kile alichoeleza kuwa hakuna mahali walalamikaji waliposema namba ya polisi, au namba ya gari ya polisi zaidi ya kusema "defender" kwani gari hizo zipo nyingi nchini.


Ameeleza kuwa wateja wake hawajawahi kumshikilia mtu huyo, wala jina lake halijawahi kuonekana kwenye majina ya walioshikiliwa kuanzia tarehe 8 hadi 20 ya mwezi tajwa kati ya wale waliokuwa na kesi ya mauaji.


"Mleta maombi ameshindwa kuthibitisha kuwa anayeshikiliwa isivyohalali yupo jela pamoja na kutokupeleka malalamiko kwenye vyombo kama polisi ya kupotea kwa mtu,"ameeleza wakili Mseti.


Akijibu hoja hizo,  Wakili Mbwabwo amesema kwa mazingira ya watu wengi na vurugu zilizokuwepo isingekuwa rahisi kutambua namba ya polisi wala gari.


"Na hoja ya kutokutoa taarifa ya kupotea kwenye vyombo vya dola wasingeripoti kupotea wakati alikamatwa na wanaamini yupo kwenye mikono ya polisi na polisi ndio watuhumiwa ndio maana wameamua kwenda mahakamani wakiamini haki itapatikana,"amesisitiza wakili Mbwambo.


Baada ya kusikiliza hoja za pande zote mbili Jaji  Gwae ameahirisha shauri hilo mpaka Mei 10,2023 kwa ajiki ya kutoa  atatoa uamuzi mdogo.



0 Comments:

Post a Comment