LODHIA YAWAPANDISHIA MSHAHARA MARUPURUPU WAFANYAKAZI WAKE



Mwenyekiti wa Makampuni ya Lodhia Group, Arun Lodhia amewapandishia mshahara wafanyakazi wa kiwanda hicho ambapo kima cha chini cha mshahara kimeongezeka kutoka 150,000 mpaka 180,000 kwa mwezi.


Aidha amewahakikishia wafanyakazi wa kampuni hizo maslahi bora na mazingira bora ya kufanya kazi ikiwemo kuwalipa malipo ya kufanya kazi muda wa ziada na fedha kwa ajili ya maziwa na chakula zikiongezwa.


Ameyasema hayo leo Machi 29, 2023 mara baada ya kumalizika kwa kikao kilichoitishwa na mkuu wa wilaya ya Arusha, Felician Mtahengerwa nje ya lango kuu ya kiwanda hicho baada ya wafanyakazi zaidi ya 700 wa kampuni hiyo Arusha kugoma kwa siku mbili.

Lodhia amesema kuwa fedha za chakula itakuwa shilingi 2,000 na fedha za maziwa itakuwa shilingi 1,000 huku akiwataka wafanyakazi hao kuongeza juhudi katikanoufanya kazi ili na wao wapande vyeo.

“Na changamoto zingine zote ndogondogo zinafanyiwa  kazi nawaombeni sana mjitahidi kufanya kazi kwa bidii nitawapandisha cheo maana kampuni ni yetu  sote tupambane kuhakikisha kila kitu  kinakuwa sawa kwa maendeleo  ya kiwanda na sisi kwa ujumla,”amesema Lodhia.
Pia ameahidi kuwa na utaratibu wa kukutana na wafanyakazi mara mbili kwa mwaka kwa ajili ya kusikiliza  kero na changamoto  mbalimbali za wafanyakazi na kuweza kuzifanyia kazi ili kuboresha shughuli za uzalishaji na maslahi ya wafanyakazi hali itakayosaodia kuepusha mgomo kama huo. 
Kwa mujibu wa sheria kima cha chini cha mshahara kwenye sekta ya viwanda nchini ni shilingi 150,000 lwa mwezi.


 Kwa upande wake Mkuu wa wilaya ha Arusha, Mtahengerwa ameushukuru  uongozi huo kumaliza mgogoro huo na kuweza kuwaongezea  mshahara kama walivyokuwa wakiomba ambalo linaleta ufanisi mkubwa mahala pa kazi. 
Aidha amewataka wafanyakazi hao kufanya kazi kwa uaminifu na kuacha wizi hivyo waheshimu sehemu yoyote ambayo inawapatia  riziki.
“Mimi mwenyewe nitakuja kufuatilia yale yote tuliyokubaliana kuhakikisha haki inatendeka leo nendeni mkapumzike kesho muingie kazini rasmi na ongezeni  bidii katika utendaji kazi wenu ili muwe  mfano bora  wa kuigwa,”amesema
Aidha wafanyakazi hao walikuwa wakilalamikia kulipwa kiwango kidogo cha mshahara huku ikilinganishwa na kazi ngumu  wanayofanya katika kampuni hiyo.


Wakizungumza mbele ya Mkuu wa wilaya ya Arusha, Mtahengerwa wamesema kuwa wamekuwa wakiahidiwa kuongezewa mishahara kila mwezi lakini makubaliano  hayo yamekuwa hayafanyiwi kazi. 
Awali wafanyakazi hao, Martin Antony amesema kuwa wamekuwa wakiomba kwa muda mrefu kuongezewa mshahara lakini hau9ngezi huku akidai kuwa mshahara wa shilingi 150,000 kwa mwezi hautoshelezi  kwa mahitaji yao ya  kila siku.
Pia wafanyakazi hao wamelalamikia  kutokulipwa muda wa ziada wa kazi 'overtime' kwa muda mrefu kitendo ambacho kinawakatisha tamaa katika utendaji wao wa kazi.

Kampuni ya Lodhia inamiliki viwanda kwenye maeneo mbalimbali nchini ambapo Novemba 28, 2022 Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa aliweka jiwe la msingi la ujenzi wa kiwanda kikubwa cha mabati cha Makampuni ya Lodhia Group kilichopo Mkuranga akiwa ziarani mkoani wa Pwani.

0 Comments:

Post a Comment