SAMIA KUFUNGUA MKUTANO WA 65 WA UNWTO-CAF JIJINI ARUSHA

 


RAIS ,Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kufungua mkutano wa 65 wa kimataifa wa shirika la utalii duniani, (UNWTO), Kamisheni ya Afrika,(CAF) unaotarajiwa kufanyika kesho Oktoba 5,2022 kwenye hoteli ya kitalii ya Grand  Melia, jijini Arusha. 





Waziri wa Maliasili na Utalii,Balozi, Pindi Chana ameyasema hayo leo Oktoba 4, 2022 jijini Arusha wakato akiongea na waandishi wa habari juu ya mkutano huo ambao pia utahudhuriwa na Katibu mkuu wa UNWTO, Zurab Pololikashvili.



Amesema  mkutano huo unatarajia kukutanisha mawaziri wenye dhamana ya masuala ya utalii na maliasili kutoka nchi wananchama wa UNWTO wa ukanda wa Afrika wanaokadiriwa kufikia zaidi ya 50.

Dkt Pindi amesema wanatarajia  kujadili  mustakabali wa ustawi wa maendeleo ya sekta ya utalii barani Afrika hasa baada ya athari za mlipuko wa janga la Uviko 19.



"Uviko 19 umeathiri utalii wa kimataifa kwa wastani wa kati ya asilimia 50 hadi 85 katika nchi mbalimbali ikiwemo Tanzania," amesema Dkt Pindi .



Amesema mkutano huo mbali ya mawaziri wa utalii pia utanatarajiwa kuwakutanisha wadau mbalimbali wakiwemo wataalam wa utalii na ukarimu katika ngazi ya kimataifa na kikanda,watoa huduma kwenye mnyororo wa utalii,wawekezaji pamoja na watu mashuhuri zaidi ya 150.



Waziri huyo wa maliasili na utalii amesema kuwa pia mkutano huo utaenda sanjari matukio mbalimbali ikiwemo jukwaa la uwekezaji kwa ajili ya kutangaza fursa za uwekezaji zilizopo nchini ambapo pia itazinduliwa 'Investment Guideline', (Tourism Doing Business) sambamba na  Marketing Symposium kwa ajili ya kuwajengea uwezo wadau wa utalii kuhusu masuala ya masoko.



" Pia kutafanyika uzinduzi wa A tour ofa African Gastronomy  pamoja na ziara za mafunzo, (FAM Trips) ambapo washiriki watapata nafasi ya kutembelea vivutio vya utalii vilivyopo Tanzania  ikiwemo Hifadhi ya Ngorongoro, Jumuiya ya wanyama pori ya Buruge na city Tour ya vivutio mbalimbali katika jiji la kitalii la Arusha,"amesema Dkt Pinda.



Amesema kulingana na sera ya Taifa ya utalii ya mwaka 1999 mkutano huo ni muhimu kwa kuwa ni mojawapo ya jitihada za serikali katika kuongeza idadi ya watalii nchini pamoja na kutanua wigo wa mazao ya utalii nchini kupitia uendelezaji wa mazao ya utalii kimkakati hususani utalii wa mikutano.



"Mkutano huo utawezesha kujengea uwezo wataalam wao na wadau wa utalii katika kutangaza utalii, kuendeleza na kufungamanisha mazao ya utalii katika kanda mbalimbali za utalii nchini, kulingana na shabaha yao ya kuongeza idadi  ya watalii kufikia milioni tano na mapato ya dola za marekani bilioni sita ifikapo mwaka 2025," amesema Waziri Pinda.


Kwa upande wake mkuu wa mkoa wa Arusha, John Mongella  amesema mkutano huo utakuwa na  fursa adhimu ya kukuza uchumi wa jiji la Arusha ,mikoa ya jirani na Tanzania kwa ujumla.

Hivyo akawasihi wananchi na wakazi wa Arusha  kuchangamkia  fursa zitakazotokana na mkutano huo wa kihistoria.

0 Comments:

Post a Comment