MAJALIWA: MAPATO YA UTALII YAMEONGEZEKA KWA ASILIMIA 81.8

WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa, amesema kuwa sekta ya utalii nchini imeanza kuimarika hasa baada ya kuathiriwa  kutokana na janga la ugonjwa wa UVIKO 19 ambapo kwa mwaka 2022 mapato ya utalii yameongezeka kwa asilimia 81.8.



Ameyasema  hayo leo Oktoba 5, 2022 wakati akifungua mkutano wa 65 wa Shirika la  Umoja wa Mataifa la utalii,(WTO) kamisheni ya Afrika, (CAF) unaofanyika kwa siku mbili jijini Arusha ukiwajumuisha mawaziri wa utalii na wadau utalii kutoka nchi wanachama


Waziri Mkuu amesema kuwa  kabla ya janga la Uviko-19 kuingia nchini mwaka 2019 Tanzania iliingiza dola za Kimarekani bilioni 2.6 zilizotokana na sekta ya utalii na kuchangia ajira za moja kwa moja na zisizo za moja kwa moja milioni 1.5



Majaliwa amesema kwa mwaka 2022 takwimu zinaonyesha  sekta ya utalii inabidi kuimarika zaidi hususani baada ya uzinduzi wa filamu ya The Royal Tour ambapo Rais Samia Hassan Suluhu aliitengeneza na kuizindua mwezi Aprili nchini Marekani kwa lengo la kuvutia zaidi watalii kutoka eneo jilo aliloliita kuwa la kimkakati kiutalii.

"Takwimu za mwaka 2021 zinaonesha kuwa watalii wanaokuja nchini Tanzania wameongezeka kwa asilimia 48.6 kutoka watalii 620,867 mwaka 2020 na kufikia watalii 922,692 mwaka 2021," amesema Waziri Mkuu Majaliwa.

Amesema baada ya uzinduzi huo mapato yatokanayo na utalii yameongezeka kwa asilimia 81.8 kutoka Dola za Kimarekeni milioni 714.59 mwaka 2020 na kufikia Dola za Kimarekani bilioni 1.3 mwaka 2021.


Pia amesema Tanzania baada ya janga hilo ikiendelea kufanya jitihada mbalimbali za kufufua sekta ya utalii, ikiwemo utengenezaji wa Filamu ya The Royal Tour iliyoongeza mapato  na watalii nchini.

Kuhusu upandaji miti alisema uamuzi wa Katibu Mkuu Mtendaji wa UNWTO, Zurab Pololikashvili  kuongoza japo la washiriki wa mkutanohuo  kupanda miti ni  mnzuri kwani unaunga  juhudi Tanzania kwenye utunzaji mazingira.

Kwenye mkutano huo ambao awali mgeni Rasmi alikuwa awe ilikuwa awe Rais Samia Suluhu Hassan ambaye Waziri Mkuu ameeleza kuwa amemwakilisha kwani yuko nje ya nchi kwa majukumu mengine  ya kikazi na amemtuma salamu za baraka .

Waziri Mkuu ametumia mkutano huo kutangaza vivutio vilivyopo nchini huku akiwahakikishia washirki wa mkutano huo kuwa Tanzania ni nchi ya amani na utulivu na yenye watu wakarimu hivyo wajisikie wako nyumbani nje ya nyumbani.


Ametoa rai kwa mashirika na taasisi za kimataifa kuiamini Tanzania na kuendelea kufanya mikutano yao ya kimataifa kwani zipo kumbi nzuri zenye uwezo na viwango vya kimataifa kama huo wa hoteli ya Grand Melia na Kituo cha Mikutano ya kimataifa cha Arusha,(AICC).

Waziri Mkuu Majaliwa alirejea kauli mbiu ya mkutano huo inayohimiza kuujenga upya utalii stahimilivu wa Afrika huku akiipongeza UNWTO kamisheni ya Afrika kwa mpango huo wa kuboresha utalii hasa baada ya janga la uviko 19.

"Kauli mbiu hii inatukumbusha utekelezaji wa kauli mbiu ya UNWTO ya utunzaji mazingira, utalii na maliasili ikiwemo hifadhi za Taifa, mapori ya akiba, maporomoko ya maji na maeneo mengine ya utalii," alisema Waziri Mkuu Majaliwa na kuongeza

..Tanzania tunatekeleza hayo kupitia kauli mbinu inayosema tumerithishwa tuwarithishe,".

Alisema kuwa mefarijika kusikia wajumbe wa mkutano huo watapanda miti kama kumbukumbu, pia  inaenda sambamba na hatua iliyochukuliwa na  halmashauri mbalimbali hapa nchini ya kutunza mazingira kwa  kupanda miti hivyo akaitaka wizara ya Maliasili na Utalii kushiriliana na taasisi nyingine za serikali kuhakikisha miti itakayopandwa inakua.




Awali akimkaribisha Waziri Mkuu, Waziri wa Maliasili na Utalii, Pindi Chana, ameeleza kuwa mkutano huo umehudhuriwa na mawaziri wa utalii kutoka zaidi ya nchi 33 wanachama wa Shirika la Utalii Duniani - Kamisheni ya Afrika.

"Mkutano huu ni matokeo ya amani na utulivu uliopo nchini Tanzania tangu kupatikana kwa uhuru,  na maendeleo ya miundombinu hapa nchini na sehemu ya utekelezaji wa mpango wa Taifa wa maendeleo wa miaka mitatu ambao umeainisha utalii wa mikutano kama utalii mpya kwa lengo la kuongeza idadi ya watalii kufikia watalii milioni 5 ifikapo mwaka 2025," amesema Waziri Chana .

Alisema kwenye mkutano huo kutakuwa na jukwaa la uwekezaji na masuala ya masoko ambapo jukwaa la uwekezaji ni mahsusi kunadi fursa za uwekezaji zilizopo nchini ambapo Kituo cha uwekezaji Tanzania, (TIC) na kile cha Zanzibar  watatoa mada kwa washiriki wa mkutano huo.

"Tumelejenga kuwajengea uwezo wataalam wa utalii kutoka sekta ya umma na binafsi ili waweze kutangaza utalii ipasavyo," alisisitiza Waziri Chana.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa UNWTO, Zurab Pololikashvili amesema kuwa baada ya mlipuko wa janga la UVIKO 19 nchi nyingi duniani ziliathirika kwa kiasi kikubwa kwenye sekta ya utalii hivyo kwa sasa wanajikita kuendelea  kuweka mikakati ya kurejesha sekta hiyo katika hali yake ya kawaida.

“Wiki iliyopita tulisherehekea siku ya utalii duniani iliyokuwa na kaulimbiu ya Rethinking Tourism, ambayo tunaamini itasaidia kuirejesha sekta hii katika hali yake ya kawaida na kuendelea kusaidia kutoa mchango katika ukuaji wa uchumi na kuongeza idadi ya ajira," amesema Pololikashvili na kuongeza.


... Mkifanya kazi kwa pamoja kwa ajili ya kuboresha sekta ya utalii barani Afrika kwa kuboresha miundombinu hasa baada ya janga la UVIKO 19 itasaidia kuboresha ufanisi wa sekta ya utalii kwenye bara zima la Afrika," alisema.

Amesema kuwa Tanzania ni miongoni mwa nchi ambazo zina vivutio bora vya kutembelea kwa ajili ya utalii na watu wengi duniani wameitambua kupitia filamu maarufu ya The Royal Tour. 











0 Comments:

Post a Comment