HUKUMA YA SABAYA YAKWAMA, SASA KUTOKULEWA JUNI 10



HUKUMU ya kesi ya uhujumu uchumi inayomkabili aliyekuwa Mkuu wa wilaya ya Hai, Lengai Ole Sabaya na wenzake sita imeshindwa kutolewa baada ya hakimu aliyesikiliza shauri shauri hilo, Patricia Kisinda kuwa nje ya kituo cha kazi.


Hukumu ya shauri hilo linalofuatiliwa na watu wengi ilikuwa itolewe leo Mei 31,2022  ambapo Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha, Fadhil Mbelwa ameeleza kuwa haitaweza kusomwa kwani hakimu aliyesikiliza shauri hilo hayupo.


Amesema kuwa kutokana na hakimu Mkazi Mwandamizi, Kisinda anayesikiliza shauri hilo namba 27/2021 kuwa kwenye kazi nje ya ofisi, shauri hilo litarudi mahakamani hapo Juni 10, mwaka huu kwa ajili ya kusomwa hukumu.



"Shauri limekuja kwa ajili ya hukumu na liko kwa Hakimu Mkazi Mwandamizi, Patricia Kisinda lakini siku ya leo amepangiwa majukumu mengine ya kikazi nje ya ofisi hataweza kutoa hukumu leo hadi Juni 10, 2022," amesema Hakimu Mbelwa wakati akiahirisha kesi hiyo.




Washitakiwa wengine kwenye kwenye kesi hiyo ni pamoja  na Enock Mnkeni, Watson Mwahomange, John Aweyo, Sylvester Nyegu, Jackson Macha na Nathan Msuya.


Mawakili wa Jamhuri waliokuwa mahakamani ni pamoja na Mawakili wa Serikali waandamizi, Janeth Sekule, Felix Kwetukia, Wakili wa Serikali Neema Mbwana na Mwendesha Mashitaka wa Takukuru, Jacopiyo Richard.


Kwa upande  wa utetezi walikuwa  Mawakili Mosses Mahuna, Fridolin Bwemelo, Edmund Ngemela na Sylvester Kahunduka ambao wanawatetea washitakiwa sita isipokuwa Mwahomange ambaye anajitetea mwenyewe mahakamani hapo.




Awali kwenye shauri hilo, Sabaya peke yake anakabiliwa na makosa matatu ikiwemo matumizi mabaya ya madaraka alipokuwa mkuu wa Wilaya ya Hai huku washtakiwa wengine sita  wakikabiliwa na makosa mengine mawili ya kuongoza genge la uhalifu na utakatishaji fedha.


Makosa hayo wanadaiwa waliyafanya  Januari 21, 2021 katika eneo la kwa Mrombo jijini Arusha ambapo katika kosa la kwanza linalowakabili washtakiwa wote saba ni kuongoza genge la uhalifu, la pili linalomkabili Sabaya peke yake ni kujihusisha na vitendo vya rushwa na la tatu linalomkabili Sabaya pia ni kujihusisha na vitendo vya rushwa ambapo anadaiwa kuchukua Sh 90 milioni.


Ilidaiwa mahakamani hapo kuwa kosa la nne linalomkabili Sabaya mwenyewe ni matumizi mabaya ya madaraka huku kosa la tano linalowakabili wote saba likiwa ni utakatishaji fedha ambapo wanadaiwa kupata Shilingi 90 milioni huku wakijua kupokea  fedha hizo zao la kosa la vitendo vya rushwa.

Katika kesi hiyo inayovuta hisia za wengi upande wa Jamhuri ulileta jumla ya mashahidi 13 na vielelezo 12 ambapo awali waliahidi kuleta mashahidi 20 mahakamani hapo huku upande wa utetezi ukileta mashahidi nane akiwemo mke wa Sabaya, Jesca Nassary na washitakiwa wote saba kila mmoja akijitetea.
 
Mashahidi Mashahidi wa Jamhuri ni pamoja na Mkurugenzi msaidizi anayesimamia utawala wizara ya fedha na mipango, Renatus Msangira, (45), Kaimu meneja wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Mkoa wa Arusha, Kayobyo Majogolo(41).

Wengine ni mwangalizi  wa geti (mlinzi) na mfanyakazi kwa Mrosso, Adanbest Peter Marandu, (61), pamoja na Philemon Tilatwa Kazidila,(64),  Juma Nuhu, (28) na Mfanyakazi wa Benki ya CRDB, Geofrey Nko.

Mashahidi wengine wa Jamhuri ni afisa uchunguzi wa kielektroniki kutoka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa nchini,(TAKUKURU), Johnson Kisaka, Meneja Benki ya CRDB tawi la Kwa Mromboo, Mary Mayoka Kimasa, (40) na mmiliki wa Mrosso Injector pump, Francis Mrosso.

Wengine ni dalali wa magari kutokea jijini Dar es Salaam, Sabri Abdallah Sharif ,(36), Meneja wa ulinzi na ushirika wa vyombo vya ulinzi na usalama Vodacom PLC,Tegeta DSM James Lisao Wawenje, (39) na Afisa uchunguzi wa TAKUKURU, Ramadhani Rajab Juma, (39).

 Washitakiwa hao wamerudishwa mahabusu kwenye gereza na Kisongo kwani mashitaka yanayowakabili hayana dhamana.

 



 

 

 

0 Comments:

Post a Comment