MWENYEKITI w Taifa wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe leo Machi 16, 2022 ameongoza kikao cha kamati kuu ya chama hicho ikiwa ni kikao chake cha kwanza tokea atoke gerezani alikokaa kwa miezi nane.
Kikao hicho kinaendelea jijini Dar es Salaam ambapo wajumbe na viongozi waandamizi wa chama hicho wanashiriki na baadhi ya wajumbe akiwamo Tundu Lissu, Godbless Lema wakishiriki kwa njia ya mtandao.
Mkurugenzi wa Itikadi, Uenezi na Mambo ya Nje wa Chadema, John Mrema amesema ajenda za kikao hicho ni pamoja na Mbowe kupokea taarifa za mwenendo wa chama tangu alivyokuwa gerezani hadi sasa.
Amesema ajenda nyingine kuwa ni pamoja na mwenendo wa kisiasa nchini, maandalizi ya mkutano wa baraza kuu la Chadema utakaofanyika mwezi.
“Leo ndio mara ya kwanza kwa Mbowe kushiriki kikao hiki baada ya kukaa gerezani miezi nane, ni kikao muhimu kwetu kwa sababu aliyekuwa akiendesha kikao kwa kipindi hicho ni makamu mwenyekiti wa Chadema Bara, Lissu," amesema Mrema na kuongeza.
“Ni kikao cha kumjulisha mwenyekiti (Mbowe), hali ya siasa, mwenendo wa chama na masuala mengine yanayoendelea. Baada ya kikao tutatoa taarifa rasmi kwa umma, yale yaliyojadiliwa na uamuzi uliofikiwa na kamati kuu,” .
Miongoni mwa wajumbe wengine waliohudhuria kikao hicho ni pamoja na John Mnyika (Katibu Mkuu), Salum Mwalimu (Naibu Katibu Mkuu-Zanzibar), Benson Kigaila (Naibu Katibu Mkuu Bara) na Catherine Ruge ambaye ni Katibu Mkuu wa Baraza la Wanawake la Chadema (Bawacha).
Machi 4, 2022 Mbowe na wenzake watatu walitoka gerezani baada ya Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) kuwasilisha hati ya kutokuwa na nia ya kuendelea na kesi iliyokuwa imefunguliwa dhidi yake na wenzake watatu katika Mahakama Kuu Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi jijini Dar es Salaam.
0 Comments:
Post a Comment