Na Gift Mongi,Moshi
Matokeo ya utafiti wa kuongeza uzalishaji wa zao la mpunga kwa bara la Afrika uliofanyika kwa kipindi cha miaka mitano kuanzia mwaka 2017 hadi 2022 yamebainisha kuwepo kwa matumizi yasiyo sahihi ya maji ikiwemo upotevu wa maji.
Akifungua mkutano wa tathimini ya utafiti huo meneja wa tume ya Taifa ya umwagiliaji mkoa wa Kilimanjaro mhandisi, Said Ibrahim alisema utafiti huo uliofanyika katika mikoa miwili ya Kilimanjaro pamoja na Arusha.
Pia ilishirikisha taasisi mbalimbali zikiwemo chuo cha ufundi Arusha, (ATC)Chuo cha mafunzo ya kilimo Kilimanjaro(KATC) na shirika la JIRCAS kutoka nchini Japan ambapo kupitia utafiti huo uzalishaji wa zao la mpunga utaenda kuongezeka.
Alisema utafiti huo umewawezesha wakulima kujifunza namna ya kutumia njia bora na sahihi za matumzi ya maji na kuepusha yasipotee hivyo kuwa na uhakika wa kulima na kuvuna kwa kipindi kirefu hata kama kutakuwepo na upungufu wa maji katika eneo husika.
"Utafiti huu ulihusisha wadau mbali mbali hivyo kumalizika kwake tumejifunza njia nyingi katika kuzuia huu upotevu wa maji zikiwemo zile njia za asili ambazo hazina gharama kubwa ikilinganishwa na njia za kisasa, "alisema
Kwa mujibu wa mhandisi Said ni kuwa utafiti huo ni vizuri ukatumiwa na akulima ili waweze kuongeza uzalishaji na kujiongezea kipato ambapo alisema skimu moja ilikuwa ikitoa tani 5 za mpunga lakini baada ya utafiti kwa sasa ni kati ya tani 7 hadi 9.
Dr Yusuph Mhando kutoka chuo cha ufundi Arusha(ATC) alisema kupitia mradi huo wameweza kujifunza namna ya kuzalisha na kutengeneza miundombinu ya umwagiliaji ambayo itatumika kuzuia upotevu wa maji kwa wakulima
"Nashukuru sisi kama chuo cha kuzalisha wataalam kshirikishwa katika utafiti huu na pia tumeona na kujifunza jinsi ya kwenda kutengeneza miudombinu ya umwagiliaji ambayo itaenda kuzuia upotevu wa maji"alisema
Mkuu wa chuo cha mafunzo ya kilimo Kilimanjaro, (KATC), Nicodemus Shauritanga alisema kupitia mafunzo hayo waliweza kujifunza kwa vitendo chuoni hapo sambamba na wakulima wa skimu ya Lower Moshi ambapo matokeo yalionekana na hivyo kwa sasa ni muda kwa wakulima wa eneo hilo kupitia tafiti huo kabla ya kuanza kilimo ili kuepusha upotevu wa maji
Alisema utafiti huo unawawezesha wadau walioshirikishwa kujua na kutumia njia sahihi za kilimo cha mpunga na kuachana na kile kilimo cha kimazoea ambacho kimekuwa kikitumia maji mengi na eneo kubwa bila kuwa na tija
"Kupitia utafiti huu unaweza kubaini kuwa unaweza kulima eneo ndogo na ukawa na matumizi kidogo ya maji matokeo yae yakawa ni mazuri zaidi kuliko mkulima aliyetumia eneo kubwa bila kufuata utaratibu na njia sahihi za kilimo cha mpunga kama utafiti ulivyoonesha"alisema.
0 Comments:
Post a Comment