KESI YA SABAYA YASIKILIZWA KIDIGITALI

ALIYEKUWA Mkuu wilaya ya Hai, Lengai Ole Sabaya aliongea na wakili wake Faudhia Mustafa


KESI ya uhujumu uchumi inayomkabili aliyekuwa mkuu wa wilaya ya Hai, Lengai Ole Sabaya  imeshindwa kuendelea leo kutokana na kilele cha maadhimisho ya wiki ya sheria.


Aidha shauri hilo limeendeshwa kwa njia ya mtandao na Hakimu Mkazi, Patricia Kisinda akiwa kwenye mahakama ya wilaya ya Monduli huku washitakiwa na mawakili wakiwa kwenye chumba cha mahakama ya hakimu mkazi Arusha kilichopo kwenye kituo jumuishi cha utoaji haki Arusha.

Washitakiwa hao iliwabidi wapite mbele ya 'screen' ya TV iliyofungwa mahakamani hapo ili kumwezesha hakimu kuwaona ambapo waliitwa majina kuanzia mshitakiwa wa kwanza mpaka wa saba.

Washitakiwa wengine kwenye shauri hilo ni pamoja na Enock Nkeni, (41) maarufu  Dikdik, Watson Mwahomange, (27) maarufu Mamimungu,John Aweyo, maarufu  Mike One, Silvester  Nyengu, (26) maarufu Kicheche, Jackson Macha, (29) na Nathan Msuya, (31).

 



"Shauri lilikuwa linakuja kwa ajili ya upande wa jamhuri kumuuliza shahidi maswali tuko tayari kwa ajili ys kuendelea," amesema wakili wa utetezi Moses Mahuna mara baada ya kuwatambulisha mawakili wengine wa utetezi Faudhia Mudtafa na Fridolini Bwemelo.

Kwa upande wake wakili wa serikali Mwandamizi, Janet Sekule alieleza kuwa, " Kama alivyowasilisha wakili Mahuna shauri lilikuwa linakuja kwa ajili ya maswali ya dodoso kwa shahidi,".

"Lakini kwa upande wetu kwa sababu ya shughuli za 'law day' ukiangalia muda saa hizi ni saa nane (mchana) kama itawezekana tunaomna kesi iendelee kesho kulingana na maamuzi ya  mahakakama yako,".

Wakili Mahuna akajibu, "hatuna pingamizi na ombi la mawakili wa serikali tunaomba tuendelee kesho,".

Hivyo Hakimu Mkazi Kisinda ameahirisha shauri hilo mpaka mpaka  kesho (Februari 3,2022) saa tatu na nusu asubuhi ambapo Sabaya ataendelea kuulizwa maswali ya dodoso na mawakili wa jamhuri.

Sabaya ambaye ni shahidi wa tatu kwa upande wa utetezi ambapo tayari Mshitakiwa Nyengu alishajitetea peke yake akifuatiwa na mke wa Sabaya, Jesca Nassary ambaye alimtetea mume wake.

Washitakiwa hao walianza kujitetea baada ya mahakama kuwaona wana kesi ya kujibu baada ya kusikiliza ushahidi uliotolewa mahakamani hapo na mashahidi 13 wa upande wa Jamhuri ambao waliwasilisha vielelezo 12.

Katika shauri hilo linalovuta hisia za wengi , Sabaya peke yake anakabiliwa na makosa matatu ikiwemo matumizi mabaya ya madaraka alipokuwa mkuu wa Wilaya ya Hai huku washtakiwa wengine wote wanakabiliwa na makosa mengine mawili ya kuongoza genge la uhalifu na utakatishaji fedha.

 

Makosa hayo wanadaiwa waliyafanya  Januari 21, 2021 katika eneo la kwa Mrombo jijini Arusha ambapo katika kosa la kwanza linalowakabili washtakiwa wote saba ni kuongoza genge la uhalifu, la pili linalomkabili Sabaya peke yake ni kujihusisha na vitendo vya rushwa na la tatu linalomkabili Sabaya pia ni kujihusisha na vitendo vya rushwa ambapo anadaiwa kuchukua Sh90 milioni.

Ilidaiwa mahakamani hapo kuwa kosa la nne linalomkabili Sabaya mwenyewe ni matumizi mabaya ya madaraka huku kosa la tano linalowakabili wote saba likiwa ni utakatishaji fedha ambapo wanadaiwa kupata Shilingi 90 milioni huku wakijua kupokea  fedha hizo zao la kosa la vitendo vya rushwa.



0 Comments:

Post a Comment