Mshitakiwa, Lengai ole Sabaya akiwa ameshikwa bega na wakili wakw, Moses Mahuna wakati akitoka mahakamani
ALIYEKUWA Mkuu wa wilaya ya Hai, Lengai Ole Sabaya na wenzake sita wamekutwa wana kesi ya kujibu kwenye kesi ya uhujumu uchumi inayowakabili hivyo wataanza kujitetea Januari 17, mwaka huu.
Uamuzi mdogo ulitolewa leo (Januari 14,2022) na Hakimu Mkazi, Patricia Kisinda wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha anayesikiliza shauri hilo la uhujumu uchumi namba 27/2021.
“Mahakama baada ya kupitia ushahidi wa mashahidi wote 13 na kuangalia vilelelezo vyote 12 mahakama imejiridhisha kuwa upande wa jamhuri wamedhibitisha mashitaka yanayowakabili washitakiwa wote,” ameleza Hakimu Kisinda wakati akisoma uamuzi huo mdogo na kuongeza.
…Kwa hiyo washitakiwa wote wana kesi ya kujibu kwa mujibu wa sheria ya uhujumu uchumi kama ilivyorekebishwa mwaka 2019 na na kifungu namba 230 cha sheria ya mwenendo wa makosa ya jinai sura ya 20 kama ilivyorekebishwa mwaka 2019,”
…Mahakama inawataka washitakiwa wote kujitetea kama ambavyo sheria inaeleza,”.
Washitakiwa wengine kwenye shauri hilo ni pamoja na Enock Nkeni, (41) maarufu Dikdik, Watson Mwahomange, (27) maarufu Mamimungu,John Aweyo, maarufu Mike One, Silvester Nyengu, (26) maarufu Kicheche, Jackson Macha, (29) na Nathan Msuya, (31).
Lengai Ole Sabaya akifurahia jambo na mawakili wake muda mfupi kabla mahakama haijatoa uamuzi mdogo kuwa ana kesi ya kujibu
Sabaya peke yake anakabiliwa na makosa matatu ikiwemo matumizi mabaya ya madaraka alipokuwa mkuu wa Wilaya ya Hai huku washtakiwa wengine wote wakikabiliwa na makosa mawili ya kuongoza genge la uhalifu na utakatishaji fedha.
SABAYA NA WENZAKE KULETA MASHAHIDI ZAIDI YA 10
Wakili wa Utetezi, Moses Mahuna ameileza mahakama hiyo kuwa wataleta mashahidi zaidi ya 10 na vielelezo vinavyoweza kuwa sawa na idadi ya mashahidi hao.
“Tutajitetea na tutakuwa na jumla ya mashahidi wasiopungua 10 na wote watajitete wakiwa chini ya kiapo na vielelezo ambavyo idadi yake siwezi kuijua kwa sasa inaweza kuendana na idadi ya hao mashahidi,” ameeleza Mahuna.
Wakili huyo wa utetezi ameomba mahakama iahirishwe ili wapate muda wa kujiandaa ikiwemo kuwaandaa mashahidi na vielelezo.
“Mheshimiwa kwa kuwa muda huu ndiyo tumepokea uamuzi huu mdogo, na ili tuweze kujiandaa na kesi kwa kuwaandaa mashahidi wetu, kukusanya vielelezo na kuweza kuviwasilisha wakati mashahidi wanatoa ushahidi wao,” ameleza Mahuna na Kuongeza.
…Ni ombi letu mahakama ionelee vema kwa kutupa nafasi iweze kuahirisha shauri hili kwa leo na kutupangia tarehe nyingine ya karibu kulingana na diary ya mahakama,”
Awali ilidaiwa mahakama hapo kuwa washitakiwa hao wanadaiwa waliyafanya makosa hayo Januari 21, 2021 katika eneo la kwa Mrombo jijini Arusha.
Kwenye shauri hilo, Sabaya peke yake anakabiliwa na makosa matatu ikiwemo matumizi mabaya ya madaraka alipokuwa mkuu wa Wilaya ya Hai huku washtakiwa wengine wote wanakabiliwa na makosa mengine mawili ya kuongoza genge la uhalifu na utakatishaji fedha.
Makosa hayo wanadaiwa waliyafanya Januari 21, 2021 katika eneo la kwa Mrombo jijini Arusha ambapo katika kosa la kwanza linalowakabili washtakiwa wote saba ni kuongoza genge la uhalifu, la pili linalomkabili Sabaya peke yake ni kujihusisha na vitendo vya rushwa na la tatu linalomkabili Sabaya pia ni kujihusisha na vitendo vya rushwa ambapo anadaiwa kuchukua Sh90 milioni.
Ilidaiwa mahakamani hapo kuwa kosa la nne linalomkabili Sabaya mwenyewe ni matumizi mabaya ya madaraka huku kosa la tano linalowakabili wote saba likiwa ni utakatishaji fedha ambapo wanadaiwa kupata Shilingi 90 milioni huku wakijua kupokea fedha hizo zao la kosa la vitendo vya rushwa.
Katika kesi hiyo inayovuta hisia za wengi upande wa Jamhuri ulileta jumla ya mashahidi 13 na vielelezo 12 ambapo awali waliahidi kuleta mashahidi 20 mahakamani hapo.
Mashahidi hao ni pamoja na Mkurugenzi msaidizi anayesimamia utawala wizara ya fedha na mipango, Renatus Msangira, (45), Kaimu meneja wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Mkoa wa Arusha, Kayobyo Majogolo(41).
Wengine ni mwangalizi wa geti (mlinzi) na mfanyakazi kwa Mrosso,Adanbest Peter Marandu(61), pamoja na Philemon Tilatwa Kazidila,(64), Juma Nuhu, (28) na Mfanyakazi wa Benki ya CRDB, Geofrey Nko.
Mashahidi wengine wa Jamhuri, afisa uchunguzi wa kielektroniki kutoka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa nchini,(TAKUKURU) Johnson Kisaka, Meneja Benki ya CRDB tawi la Kwa Mromboo, Mary Mayoka Kimasa(40) na mmiliki wa Moroso Injector pump, Frances Mrosso.
Wengine ni dalali wa magari kutokea jijini Dar es Salaam, Sabri Abdallah Sharif ,(36), Meneja wa ulinzi na ushirika wa vyombo vya ulinzi na usalama Vodacom PLc,Tegeta DSM James Lisao Wawenje(39) na Afisa uchunguzi wa TAKUKURU, Ramadhani Rajab Juma, (39)
0 Comments:
Post a Comment