| Lengai Ole Sabaya akiongea na wakili wake Moses Mahuna alipoletwa mahakamani jana Novemba 2,2021 |
Katika mashitaka hayo Sabaya anakabiliwa na mashitaka yote matano ya kuongoza genge la uhalifu, matumizi mabaya ya madaraka, kushawishi na kujipatia fedha kwa njia ya rushwa na kutakatisha fedha.
Washitakiwa sita waliobaki wakikabiliwa na mashitaka mawili kila mmoja ya kuongoza genge la uhalifu na utakatishaji fedha kinyume cha sheria.
Hati hiyo ya mashitaka imesomwa Septemba 9, 2021 na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Tarsila Gervas mbele ya hakimu mkazi, Dkt. Patricia Kisinda anayesikiliza shauri hilo la uhujumu uchumi namba 27/2021.
Akiwasomea mashitaka hayo, Wakili wa Serikali Mwandamizi, Tarsila aliieleza mahakama hiyo kuwa, shitaka la kwanza linawakabilia washitakiwa wote saba ni la kuongoza genge la uhalifu kinyume cha sheria ya uhujumu uchumi.
Akisoma maelezo ya kosa, Wakili huyo ameeleza kuwa, mnamo Januari 22, mwaka huu, Sabaya akiwa katika maeneo tofauti ndani ya jiji la wilaya ya Arusha akiwa mtumishi wa umma kwa nafasi ya mkuu wa wilaya ya Hai iliyopo mkoani Kilimanjar na anadaiwa kukiuka masharti yake ya ajira.
Sabaya anadaiwa kushirikiana na washitakiwa wenzake sita ambao si maafisa wa serikali lakini kwa makusudi kabisa walifanya vitendo vya uhalifu kwa kutumia nafasi ya Lengai ole Sabaya ambaye ni mtumishi wa umma na kujipatia fedha za Kitanzania shilingi milioni 90 kwa manufaa yao.
Katika Shitaka la pili linalomkabili Sabaya peke yake ni la kujihusisha na vitendo vya rushwa kinyume na sheria ya kupambana na kuzia rushwa.
Imedaiwa mahakamani hapo kuwa mnamo Januari 22, 2021, Sabaya akiwa kwenye maeneo ya Kwamrombo yaliyo katika kwenye jiji na wilaya ya Arusha alijihusisha na vitendo vya rushwa kwa kumtaka Frances Mroso ampatie shilingi milioni 90 za Kitanzania.
Sabaya anadaiwa kushirikiana na washitakiwa wenzake sita kama kushinikiza kupatiwa kiasi hicho cha fedha ili wasitoe taarifa za jinai dhidi ya Mrosso ambapo kwa wakati huo walikuwa wakimtuhumu kwamba alikuwa na makosa ya ukwepaji kodi.
Kosa la tatu ni kujihusisha na vitendo vya rushwa, shitaka linalomkabili Sabaya peke yake anayedaiwa kuwa mnamo Januari 22, 2021 alijihusisha na vitendo vya rushwa kwa alijipatia shilingia milioni 90 kutoka Frances Mrosso akishirikiana na washitakiwa wenzake sita katika kumshinikiza ili wasitoe taarifa ya kosa la jinai ambalo walimtuhumu nalo Mrosso.
Kosa la nne ni matumizi mabaya ya madaraka kinyume cha sheria ya kuzuia na kupambana na rushwa ambalo linamkabili Sabaya peke yake ambapo anadaiwa mnamo Januari 22, 2021 akiwa kwenye maeneo ya Kwamromboo jijini na wilayani Arusha alitumia vibaya mamlaka yake ya ukuu wa wilaya ya Hai iliyopo mkoani Kilimanjaro.
Sabaya anadaiwa kwa makusudi kabisa alimtisha Mrosso kumfungulia mashitaka ya kukwepa kodi kinyume cha sheria za tawala za mikoa kwa madhumuni ya kujipatia shilingi milioni 90 kwa faida yake na washitakiwa wengine sita.
Kosa la tano ni utakatishaji fedha kinyume na sheria ambalo linawakabili washitakiwa wote saba ambapo wanadaiwa kuwa mnamo Januari 22, 2021 maeneo ya Kwamrombo
, wote kwa pamoja walijipatia fedha kiasi cha shilingi milini 90 wakati wakijua walipokuwa wakipokea fedha hizo ni zao la vitendo vya rushwa.
Washitakiwa wote walikana mashitaka hayo
0 Comments:
Post a Comment