KIWANDA cha kungeneza nguo na vyandarua cha A to Z cha jijini Arusha, kuanza kutengeneza bidhaa zitokanazo na taka ngumu za chupa za maji na mifuko ya sandarusi maarufu kama salfeti.
Aidha uzalishaji huo mbali ya kulinda mazingira kwa kuondoa chupa na mabaki ya bidhaa za plastiki zinazozagaa mitaani lakini pia unatarajiwa kutoa ajira kwa wananchi.
Mtendaji Mkuu wa Kiwanda hicho Viral Shah, alimweleza hayo Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, Hamad Chande, wakati alipokitembelea kiwanda hicho mwishoni mwa wiki alipofanya ziara ya siku moja mkoani Arusha.
Alisema kuwa wanatarajia kukusanya taka ngumu za plastiki zitokanazo na chupa za maji na mifuko ya sandarusi kisha watazichakata na kutengeneza malighafi kwa ajili ya kutengenezea vifungashio mbadala ambavyo hutumika kufungasha na kubebea bidhaa kwenye maduka makubwa ya jumla na rejareja.
Shah alisema tayari utafiti wa uwekezaji huo umeshafanyika ikiwemo kufanyia tathmini maeneo ambayo taka hizo zitakusanywa kwenye wilaya zote za sita za mkoa wa Arusha.
"Vijana watakuwa wamepata ajira wakisubiri matarajio ya ajira walizosomea, watakusanya chupa na kusubiri magari ya kiwanda kuzipitia na watalipwa kwa mwezi.Tutawapa vitambulisho maalumu vya kiwanda ili wasibughudhiwe, lakini pia tutaomba baraka za Wizara inayohusika ili kufuata miongozo na taratibu zilizopo," alisema Shah
Alisema kuwa tayari kiwanda chake kimeshanunua mashine moja ya kutengeneza malighafi kutokana na takangumu za chupa za maji, ambazo zitatengeneza ndoo, vikapu vitokanavyo na plastic ambacho ni rafiki wa mazingira.
"Tutahakikisha hakuna taka ngumu aina ya chupa za maji zinazagaa mitaani, chupa badala ya kuwa kero sasa zinageuka uchumi na ajira, tunaomba Serikali ijiandae kutupatia wataalamu katika kutekeleza mpango huo ili tuibue ajira kwa vijana,"alisema Mtendaji mkuu huyo wa kiwanda cha A to Z.
Aidha aliiomba Serikali kutambua mchango wa kiwanda hicho ambacho hutengeneza vyandarua maalumu kwaajili ya kujikinga na malaria na kusambaza kwa Nchi za Afrika.
kwani hadi sasa kimeajiri wafanyakazi Watanzania zaidi 800.
Kwa upande wake, Naibu Waziri, Chande alishukuru jitihada na maono ya kiwanda hicho, kwani zaidi ya kuindolea kero Serikali itokanayo na kuzagaa kwa chupa za maji lakini pia kusaidia ajira na kipato kwa vijana hilo likiwa ni kipaumbele na ahadi za Serikali kila wakati.
"Hilo ni jambo jema anzeni tutawapa ushirikiano wote utakao hitajika, naomba na wawekezaji wengine nchini waige hili, tupanue wigo wa ajira lakini pia na usafi wa mazingira yetu ambayo sote tunayategemea ili tuendelee kuishi" alisema Naibu Waziri huyo.



0 Comments:
Post a Comment