BASHUNGWA ASITISHA UKAGUZI NYIMBO ZA WASANII KABLA YA KUSAMBAZWA




Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo,  Innocent Bashungwa ameliagiza Baraza la Sanaa nchini, (BASATA) kusitisha utekelezaji wa Kanuni ya  25 ya mwaka 2018, inayotaka kazi zote za Sanaa kukaguliwa na Baraza hilo  kabla ya kusambazwa.


Ameyasema hayo Mei 08, 2021 katika kikao chake na  Viongozi wa Vyama na Mashirikisho ya Muziki na Filamu nchini kilicholenga kuzungumzia Kanuni hiyo inayohusu uhakiki wa kazi za Sanaa  kabla ya kuingia sokoni au kusambazwa.


Bashungwa amesisitiza kuwa maelekezo hayo ya kusitishwa kwa matumizi ya Kanuni hiyo ni kwa upande wa Muziki pekee ila kwa upande wa Filamu itaendelea kutumika kama kawaida.


 

"Nawaelekeza BASATA  kuharakisha mchakato wa kurekebisha Kanuni hiyo kwa kuwashirikisha wadau  wao wa vyama na mashirikisho ili kuweza kupata Kanuni mpya isiyodumaza Tasnia ya Muziki lakini izingatie maadili ya Taifa" alisisitiza Bashungwa.




Aidha Waziri huyo ameelekeza BASATA kushirikiana na wadau kuandaa mwongozo utakao kuwa ukitoa dira njema ya uendeshaji na ukuzaji wa tasnia ya Muziki.


Bashungwa pia amewatoa hofu Wasanii kuhusu suala la ugawaji wa Mirabaha kwa kuelezea kuwa Serikali imeandaa mifumo ya kidijitali ambayo itarahisisha ukusanyaji wa mirabaha hiyo na kuongeza gawio.


"COSOTA imekuwa na changamoto ya ukusanyaji wa mirabaha kutokana na uhaba wa watumishi hivyo kwa kupitia mfumo mpya wa kidijitali utakao anzishwa hivi karibuni utarahisisha ukusanyaji wa mirabaha hiyo, Serikali inataka kutoa gawio la pesa nyingi kwa wasanii na siyo fedha kidogo hivyo tunawaomba mvumilie kidogo kuanzia mwaka mpya wa fedha mambo yatakuwa mazuri," amesema Bashungwa.


Naye mmoja wa wasanii hao Soggy Doggy alimshukuru Mheshimiwa Waziri kwa maamuzi  aliyoyafanya na kumpongeza ambapo ameahidi kuendelea kushirikiana na wasanii wenzake katika Muziki ili kukuza na  kuiendeleza tasnia hiyo.


0 Comments:

Post a Comment