TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa,(TAKUKURU) imerejesha zaidi ya shilingi bilioni 1.36 ambazo ni fedha za umma na kodi mbalimbali za serikali zilizokuwa zimechepushwa kwa njia ya rushwa na kufanyia ubadhirifu.
Fedha hizo zimekabidhiwa leo, Aprili 24, 2021 kwa walengwa na Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU, Brigedia Jenerali, John Mbungo kwenye ofisi zao mkoani Arusha akiwa na Mkuu wa taasisi hiyo mkoani Arusha, James Ruge.
Alikabidhi shilingi milioni 212 za Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma,(PSSF), ikiwa ni sehemu ya shilingi milioni 293 walizoziokoa kutokana na vitendo vya rushwa kwa kuingia mikataba mibovu na udanganyifu wa dhamana.
"Kati ya fedha hizo, tayari shilingi milioni 77 zilishawekwa katika akaunti ya PSSSF. Fedha hizi za umma za watumishi, zilichepushwa kwa njia ya rushwa na waajiri mbalimbali wasio waaminifu na hivyo kujinufaisha wao binafsi," amesema Brigedia Jenerali, Mbungo.
Amesema kuwa fedha hizo ni sehemu ya shilingi bilioni 1.86 zilizotolewa kinyume cha sheria na taratibu zinazosimamia vyama vya ushirika zikiwemo SACCOS ambapo SACCOS za AUWSA na AICC zilipokea fedha hizo na kushindwa kuzirejesha serikalini kwa wakati.
"Tumefanikisha ulipwaji wa zaidi ya shilingi milioni 7.6 ambazo ni fedha za mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii,(NSSF). Fedha hizo ni makato ya michango ya watumishi yaliyopaswa kuwasilishwa NSSF tawi la Arusha lakini fedha hizo zilichepushwa kwa njia ya rushwa na waajiri," amesema mkurugenzi kuu huyo wa TAKUKURU.
Aliwataka waajiri wote nchini kuhakikisha wanawasilisha makato ya michango ya akiba za waajiriwa wao katika mifuko stahiki ya hifadhi za jamii kwani kinyume cha hapo ni kufanya matumizi mabaya ya ofisi jambo ambalo ninkosa kisheria.
Brigedia Jenerali, Mbungo alikabidhi shilingi milioni 11 ikiwa ni sehemu ya zaidi ya shilingi milioni 112 ambazo ni fedha za umma za matrekta zilizotolewa na Mfuko wa Pembejeo wa Taifa, (AGOTF) zilizostahili kureshwa serikalini ambapo kati ya fedha hizo shilingi milioni 101.5 tayari zimeshawekwa katika akaunti ya serikali.
Amesema fedha hizo zilitolewa na serikali tangu mwaka 2018 kwa lengo la kuwasaidia wakulima kuondokana na kilimo cha jembe la mkono lakini baadhi ya wanufaika hawakufanya rejesho mpaka TAKUKURU ilipoingilia kati.
"Natoa Rai kwa taasisi au mtu yeyote atakayepokea mkopo wa serikali na kushindwa kuurejesha kwa wakati afahamu kwamba kufanya hivyo ni kosa la jinai pamoja na rushwa kwani kwa kupitia fedha hizo mhusika atakuwa amezitumia kujinufaisha kwa matumizi binafsi na hivyo kutenda kosa la rushwa," alionya mkurugenzi mkuu huyo wa TAKUKURU.
Amesema kiasi cha shilingi milioni 519 kimewekwa kwenye akaunti ya Mamlaka ya Mapato nchini, (TRA) tawi la Arusha ikiwa ni fedha ambazo makampuni ya utalii, ujenzi na kilimo ya jijini hapa yalikwepa kulipa kodi za serikali.
Brigedia Jenerali Mbungo alikabidhi kiasi cha shilingi miliono 227.8 kwa wananchi waliodhulumiwa kwa njia ya rushwa na waajiri wao, waendeshaji katika huduma za kifedha pamoja na wabia katika biashara walizokuwa wakifanya.
"Vilevile nitakabidhi kwa wananchi, kadi za ATM 100 za benki ya NMB na CRDB zilizokuwa zimechukuliwa na wanufaika hao kinyume na matakwa ya taratibu za benki," amesema Brigedia Jenerali Mbungo.
Alikabidhi shilingi milioni 50.9 ambazo ni fedha za vyama vya ushirika zikiwemo SACCOS na AMCOS za jijini Arusha ambapo fedha hizo zimetokana na baadhi ya viongozi na wanachama wa vyama hivyo kufanya ubadhirifu na ufujaji huo wa fedha.
Aidha Brigedia Jenerali Mbungo amesema TAKUKURU mkoani Arusha wanaendelea na uchunguzi wa tozo za vibali vya ujenzi, utozaji wa ushuru wa huduma na ushiru wa uzoaji taka.
"Katika uchunguzi huu tumefanikiwa kuokoa fedha za Halmashauri ya wilaya ya Arumeru kiasi cha shilingi milioni 117.8 ambazo zilikuwa hatarini kuhujumiwa kwa njia ya rushwa " amesema Brigedia Jenerali Mbungo.
Amemkabidhi mkurugenzi wa halmashauri hiyo shilingi milioni 19.5 ambapo alidai kiasi kingine kimeshaingizwa kwenye akaunti ya halmashauri hiyo.
"Leo nitakabidhi kompyuta kwa mkurugenzi wa halmashauri ya Arumeru kwa niaba ya hospitali ya wilaya hiyo ya Tengeru ambayo ndiyo wamiliki wa kompyuta hiyo," amesema Brigedia Jenerali Mbungo na kuongeza.
"Kompyuta hii ni mali ya serikali iliyokuwa imemilikishwa mtu binafsi jambo ambalo ni matumizi mabaya ya madaraka na kunyume na kufungu cha 31 cha sheria ya kuzuia na kupambana na rushwa Na. 11 ya mwaka 2007,".
Pia alikabidhi nyaraka za umiliki wa ardhi za viwanja vitatu vilivyopo wilayani Arumeru vyenye thamani ya shilingi milioni 18.5 mali ya Alex Msengi, Emmanuel Segeja na Bertha Pallangyo.
0 Comments:
Post a Comment