WANANCHI wa vijiji saba wanaoishi kuzunguka Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro, (KIA) wamemuomba Rais, Samia Suluhu Hassan kuingilia kati mgogoro wa ardhi kati yao na uwanja huo ili awanusuru wasinyang'anywe ardhi yao walioirithi kwa mababu zao.
Aidha wamedai kuwa majibu yaliyotolewa bungeni Machi 13, mwaka huu na Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mwita Waitara, juu ya mgogoro huo yamezua taharuki kubwa na wasiwasi miongoni mwao kwani hayana ukweli.
Wameyasema hayo leo, Machi 24, mwaka huu wakati wa mkutano wao maalum uliofanyika kwenye kijiji cha Tindigani ambapo kikao hicho kilihudhuriwa na wananchi kutoka vijiji hivyo saba vinavyozunguka uwanja huo kutoka kata za Kia na Rindugai.
Akisoma tamko la pamoja la wananchi hao, Katibu wa Chama ha Mapinduzi, (CCM) kata ya Kia, Stephen Laizer, amesema kuwa mwaka 1969 KIA ilitwaa hekta 460 za ardhi toka kwa wananchi hao ambazo wanadai kuwa mpaka sasa wanazishikilia na hawajaziendeleza jambo waliloshauri ni vema wakaliendeleza eneo hilo badala ya kuwanyanyasa na kutaka kuchukua maeneo mengine.
Amenukuu majibu ya Naibu Waziri, Waitara aliyotoa bungeni waliyodai ndiyo yamesababisha taharuki na wasiwasi mkubwa miongoni mwao akisema, "KIA ilitenga eneo lenye ukubwa wa hekta 11,080 mwaka 1969. Ilipima eneo hilo kwa ramani plan E5-255/18 farm no 1 mwaka 1989. Mwaka 2001 serikali ilibaini kuwepo kwa wananchi katika vijiji hivyo. Mwaka 2005 KIA ilipewa cheti cha ardhi no 22270 mwaka,".
Amesema kuwa madai ya Naibu Waziri huyo kuwa mwaka 2001 ndiyo serikali ilibaini uwepo wa wananchi kwenye eneo hilo hayana ukweli.
"Babu zetu walikuwa kwenye eneo hili kwa karne nyingi sana. Wamisionari wa kwanza waliouona hata kudai wameugundua mlima Kilimanjaro, Dkt Ludwing Kraft na mchungaji, John Rebman wanasadikika kuwa ndiyo wazungu wa awali kuwaona wamasai kwenye eneo hili, mwaka 1840," amesema Laizer na kuongeza.
"Hapa ndipo chimbuko la Maasai. Profesa Issa Shivji wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam katika utafiti wake alioufanya hapa mwaka 1998 aliandika," Wamaasai wanaamini kwamba Naiterukop (mama) ambaye ndiye mwanzilishi wa jamii ya Maasai alitokea hapa,"
"Noti ya shilingi 100 ya mwaka 1960 na mwanzoni mwa miaka ya 1970 ilikuwa na picha ya Maasai. Picha hiyo ilipigwa katika eneo hili kabla ya KIA ,"
Laizer amesema kuwa mwaka 1975 vijiji vitano vilisajiliwa kwenye eneo hilo chini ya sheria ya vijiji vya ujamaa ambavyo ni Sanya Station, Mtakuja, Majengo, Malula na Samaria.
Hata hivyo sheria ya serikali za mitaa namba 7/1982 ilifuta sheria ya vijii vya ujamaa ambapo kwenye eneo hilo vilisajiliwa vijiji viwili vya Tindigani na Chemka.
Laizer anasema Agosti 1, 1985 Wizara ya Ardhi iliyenga kilometa za mraba 110 kwa kile ilichoeleza ni kuendeleza uwanja huo bila kuwashirikisha wananchi wanaoishi maeneo hayo jambo walilodai kuwa ni kinyume cha sheria ya unyakuaji ardhi ya namba 47 ya mwaka 1967.
"Mwaka 1986 KIA ilipima eneo hili Farm No 1 Plan E5 255/18 ilisajiliwa kwa siri ikiwa na namba 23164 mwaka 1989," amesema Laizer.
Amesema baada ya kubaini Wizara ya ardhi imeipa KIA hati hiyo kinyume na sheria walichukua hatua mbalimbali ikiwemo aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo, Freeman Mbowe kulizungumzia bungeni Novemba 10, 2003.
Amesema kuwa pia kuna muhtasari wa kikao cha pamoja cha vijiji hivyo na Tasisi ya kuendeleza uwanja wa KIA, (KADCO) uliofanyika Machi 28, 2006 ambapo muhtasari huo unaeleza bayana kuwa kulikuwa na mgogoro wa ardhi baina ya pande hizo mbili.
"Bila kuzingatia mgogoro huo ulifika bungeni mara kadhaa kati ya 2000 na 2006, KIA walipewa cheti cha ardhi na 22270 Aprili 20, 2006 kwa miaka 99. Vijiji hivi vilifadhaika na kughadhibika mno kwa kuporwa ardhi yao ya urithi," amesema Laizer.
Diwani wa Kia, Tehera Mollel, akiongelea taharuki hiyo amesema "Tangu tumesikia majibu ya Naibu Waziri kata yangu imepata taharuki kubwa. Kwa niaba ya wananchi wa Kia namuomba mheshimiwa Rais, mama Samia wewe mwenyewe ndiyo unaweza kututatulia huu mgogoro," amesema diwani huyo wa Kia na kuongeza.
"Atume timu ije iangalie hili suala kwa makini kwa sababu taarifa ya Naibu Waziri ni ya uongo. Tunaomba mheshimiwa Rais aliangalie hili jambo kwa mapana. Wananchi wa Kata ya Kia wamenyanyasika, imeonekana kama sio Watanzania, wanalia wamama wanalia vijana kwani wanaenda kukosa makazi yao ya asili na hawana makazi mengine zaidi ya haya,"
Mollel amesema kuwa uamuzi huo unamaanisha kuwanyang'anya makazi, mashamba makubwa ya kilimo na malisho ya mifugo wananchi wa vijiji saba.
"Tunamuomba Rais wetu mama Samia, tunajua ni Rais wa wanyonge, anatambua unyanyasaji unaoendelea kwenye kata yetu ya Kia.Tunaomba atume tume huru ije ihakiki madhara ambayo serikali itapata baada ya kufukuza watu hawa kwa sababu naamini kamati zote zilizotumwa za mawaziri waliopita, Harson Mwakyembe na Anna Tibaijuka hazijafanya kazi halisi," amesema Mollel na kuongeza
"Tunaomba Rais atume tume huru ije kuangalia madhara, kaya zinazopata shida baada ya mgogoro huu ni kaya zaidi ya 5,000 lakini kwenye makabrasha inatamkwa kaya 200 na zaidi ambayo ni sawa na robo ya idadi ya wananchi kwenye kitongoji kimoja tu,"..
"Tuna majengo ya serikali shule za msingi na sekondari, zahanati, misikiti na makanisa. Tunaomba serikali itoe nafasi ije ijionee yenyewe. Itume tume huru ije ihakikishe ni kiasi gani wananchi wanaumia hapa
Anna Ngulai |
Bibi mwenye umri wa zaidi ya miaka 100, Anna Ngulai anayedai alishiriki kwenye ujenzi wa uwanja wa ndege wa KIA amwangukia Rais, Samia amuomba asadie kuliza mgogoro huo kwa wao kupewa haki yao ya kumiliki ardhi yao ya asili.
"Nimezaliwa tangu enzi za mababu zetu wa zamani, Mungu ameniacha niweze kutetea ardhi yangu. Hii ardhi ni yangu, nilizaliwa hapahapa," anasema Anna na kuongeza.
...Nimezaliwa hapa lakini mashangaa kila kukicha ni ugomvi tuu. Tumejenga uwanja huu , (KIA) wakati wa Nyerere sisi ndiyo tumefanya kazi ya ujenzi hapo...
....Tulikuwa tunabeba mawe kwa kutumia ngozi, maji tulikuwa tunabeba na ngozi zilizoshonwa. Tulijenga uwanja wote mpaka kambi za maaskari,".
Amos Moringe ambaye ni mwenyekiti mstaafu kijiji cha Sanya station anasema kuwa yeye alizaliwa kijijini hapo mwaka 1952.
"Nimezaliwa na kukulia hapa kwenye eneo la KIA. Wakati wanajenga kiwanja cha ndege tulikuwa tunaangalia na tunafahamu. Utawala wa kwanza wa KIA meneja alikuwa anaitwa Mathias hatukuwahi kupata mgogoro naye," anasema Moringe na kuongeza.
"Nampongeza Rais Samia kuwa Rais, naomba kilioa cha wananchi wa vijiji vya Sanya Station, Chemka na Tindigani vikufikie na utusaidie kutuondolea unyanyasaji huu,".
Moringe alidai kuwa taarifa zilizotolewa bungeni na Naibu Waziri, waitara ni za upotoshaji zenye lengo la kuwanyanyasa wananchi hivyo akaiomba Serikali iwasikie.
"Tunamuomba Rais asikie kilio yetu na akiwezekana aturuhusu sisi tuone yeye ana kwa ana, tumweleze shida yetu badala ya kusikiza watu wale ambao aitekelezi kama inavyotakiwa," anasema Moringe na kuongeza.
... Wanapotosha wanatoa taarifa za uongo wakiwa kwenye meza. Naomba serikali asitoe maagizo kwenye meza afike aone umati wa watu wanaonyanyasika,".
Naye Samweli Leng'ate ambaye ni mwenyekiti mstaafu kijiji cha Tindigani alisema anamuomba Rais Samia afike kuwasikiliza kwani mara zote mawaziri wa ardhi wanaoshughulikia suala hilo hawajawahi kukutana nao.
"Tunapata shida sana kwa sababu kila mara serikali imekuwa ikipita, hao mawaziri wa ardhi wanapitia KIA wanaenda halmashauri ya Hai lakini bila kufika eneo husika kujua matatizo ya wananchi na kujua eneo husika la mgogoro," anasema Samweli na kuongeza.
...Ninaomba sana Rais Samia , aliangalie tatizo hili la wananchi wa KIA kwa jicho la huruma kwa sababu tumelalamika sana kwa miaka mingi lakini hakuna msaada,".
Bibi, Elieka Sango mkazi wa Tindigani naye ameungana na wananchi wengine kumuomba Rais Samia kuingilia kati mgogoro huo kwa kile alichodai kuwa hawana eneo lingine la kuishi zaidi ya hapo.
"Sisi tunasikitika sana kwa sababu kila wakati sisi tuna mgogoro. Mali zetu zinapita njiani kwenda Dodoma kila pakuche. Hatuwezi kuwa wakimbizi kama wanyama," anasema bibi Elika kwa lafudhi ya Kimaasai na kuongeza.
"Tunaomba mama yetu, Rais Samia kilio yetu ikufikie kwa sababu wewe unajua hali ya mwanamke ikoje. Sisi ndiyo tunalea familia wakinamama sasa sisi tukikimbizwa tutaenda wapi na familia?," anahoji bibi Elieka na kuongeza
"Kila siku tunaambiwa ondokeni, kimbieni tuende wapi? . Mimi hapa mnavyoniona babu yangu mzaa baba amezaliwa hapa, babu yangu mzaa mama amezaliwa hapa. Mama na baba yangu wamezaliwa hapa napoambiwa niondoke nitajua ninaenda wapi?,"...
"Mimi naomba Rais wetu Samia Suluhu Hassan sikia kilio ya wamama, Tumeshukuru ulipowekwa madarakani kuwa Rais, .....Tunaomba utubebe na sisi wanawake wa KIA. Wanatunyanyasa sana, unakuta sisi tunalea watoto wetu, sisi ni wajane. Watoto wanakua wanaenda kazini anakuachia familia yake sasa tunaambiwa tuondoke tutawabeba watoto na wajukuu tuwapeleke wapi?,".
Eliaishi Laiser, katibu wa UWT tawi la Sanya station, anasema kuwa anasikitishwa na taarifa iliyotolewa ya kuwataka kuhamishwa kwenye maeneo hayo ikidaiwa kuwa ni mali ya KADCO.
"Hatuko kwenye maeneo ya KADCO sisi tuko kwenye maeneo yetu. Tunamuomba Rais Samia aingilie kati mgogoro huu kwani unatunyima hata kufanya shughuli za maendeleo kwani kila baada ya miaka kadhaa tuna mgogoro," anasema Eliaishi na kuongeza.
"Kwenye maeneo yetu tuna taasisi nyingi, tuna shule za chekechea, shule za msingi, tuna zahanati. Sisi tunasikitika kama vijana tunashindwa kufanya shughuli za kujiendeleza kwani kila baada ya muda unaibuka mgogoro tukiambiwa tuondoke,".
0 Comments:
Post a Comment