AKAMATWA KWA KUKUTA NA SARE ZA POLISI, PINGU


Kamanda wa Polisi, Kanda Maalum ya Dar es Salaam Lazaro Mambosasa

Mhudumu wa Hoteli ya Sleep Inn, na mkazi wa Mwananyamala kwa kopa, anashikiliwa na polisi  kwa kukutwa na sare za  polisi, silaha, cheo cha koplo na pingu.

Kamanda wa Polisi, Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa ametoa taarifa kwa hiyo leo kuwa Jeshi la Polisi lilipokea taarifa kutoka kwa msiri kuwa kuna mtu mmoja  anatumia sare za Jeshi la Polisi kuwakamata watu na kuwafunga pingu, kuwatishia bastola ili kufanikisha  kupora mali maeneo mbalimbali ya Jiji.

“Baada ya kupata taarifa hizo Jeshi la Polisi lilianza ufuatiliaji mara moja na kuweka mtego. Mnamo tarehe 12 Mei 2018 majira ya saa nne usiku huko Mwenge Bamaga Polisi  walifanikiwa kumkamata mtuhumiwa huyo,” amesema Mambosasa katika taarifa hiyo
Mambosasa amesema baada ya kufanya naye mahojiano mtumiwa alikiri kumiliki sare na vifaa mbalimbali vya Jeshi la Polisi na kukubali kuwapeleka askari hadi nyumba anayoishi.

“Baada ya kufanya upekuzi kwenye nyumba hiyo alikutwa na sare za Jeshi la Polisi, pingu, cheo cha koplo wa Polisi, mfuko wa kuhifadhia bastola na bastola aina ya GLOCK 17 ambayo imefutwa namba zake za usajili ikiwa haina risasi,” amesema kamanda Mambosasa.

Mtuhumiwa huyo ameshafikishwa mahakamani kujibu tuhuma zinazomkabili.

0 Comments:

Post a Comment