Mbunge Jimbo la Kawe kupitia tiketi ya CHADEMA, Halima Mdee amekamatwa na Jeshi la Polisi leo asubuhi kwenye uwanja wa ndege wa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere Jijini Dar es Salaam akitokea nchini Afrika Kusini alikokuwa akipatiwa matibabu.
Mbunge wa Jimbo la Ubungo, Saed Kubenea (CHADEMA), amesema Halima Mdee amekamatwa leo na Jeshi la Polisi Kwa kile walichodai ni hatua ya Mdee kushindwa kuripoti kwenye kituo cha polisi kama masharti ya dhamana yalivyoagiza japo
alitoa taarifa ya udhuru."Ni kweli Halima Mdee amekamatwa leo asubuhi akiwa Airport Jijini Dar es Salaam na Jeshi la Polisi, inafahamika kuwa Mdee ni miongoni mwa viongozi wa Chadema wanaoshtakiwa kwenye kesi ambayo ipo Mahakamani ambapo Mwenyekiti Freeman Mbowe akiwa mmoja wao", amesema Kubenea.
Pamoja na hayo, Kubenea ameendelea kwa kusema "walikuwa nje kwa dhamana kabla ya kesi kupelekwa Mahakamani, kwa hiyo Halima alikuwa hajaenda kuripoti Polisi siku waliyoambiwa waende kuripoti Polisi kwa maana yeye alikuwa nje ya nchi. Sasa amerejea nchini leo asubuhi ndipo walipomkamata Airport".
Kwa upande mwingine, Kubenea amesema kukamatwa kwa Halima Mdee bila shaka Jeshi la Polisi linataka kumuunganisha na viongozi wengine waliokuwa gerezani mpaka muda huu lisha ya kwamba wamepatiwa dhamana.
CHAMA CHA DEMOKRASIA NA MAENDELEO (CHADEMA) TAARIFA KWA UMMA-KUKAMATWA KWA MHE. HALIMA MDEE (MB)
Leo Jumapili tarehe 01 Aprili 2018, majira ya saa tisa alfajiri Mhe. Halima Mdee (Mb) alikamatwa akiwa uwanja ndege wa Dar Es salaam alipokuwa amerejea nchini akitokea Nchini Afrika Kusini alipokuwa anapatiwa matibabu.
Mpaka mchana wa leo tarehe 01 Aprili, 2018 Jeshi la Polisi wameendelea kumshikilia Katika Kituo Kikuu cha Polisi Dar es Salaam na hajapatiwa dhamana pamoja na daktari wake kuwathibitishia polisi kuwa Mheshimiwa Halima ni mgonjwa.
Tunasikitishwa na kulaani kitendo hiki cha Polisi kuendelea kumshikilia mgonjwa ambaye alikuwa amelazwa hospitalini.
Tunatoa mwito kwa Jeshi la Polisi limpatie dhamana ili aweze kuendelea na matibabu yake, Kwani dhamana ni haki yake na zaidi ni kuwa huyu bado ni mtuhumiwa na ni Mgonjwa ambaye ametoka hospitalini.
Mwisho Jeshi la Polisi litawajibika kwa watanzania endapo afya ya Mhe. Halima Mdee ikitetereka au ikidhoofu zaidi na lawama zote zitakuwa juu yao.
Imetolewa Leo Jumapili tarehe 01 Aprili, 2018
John Mrema - Mkurugenzi wa Itifaki, Mawasiliano na Mambo ya Nje - CHADEMA

0 Comments:
Post a Comment