ASKOFU AWAGEUKIA WENZAKE

Askofu wa Makanisa ya Baptist Tanzania Arnoid Manase 
ASKOFU Mkuu wa Makanisa ya Baptist Nchini,Mch.Arnold Manase amepinga matamko na waraka uliotolewa na maaskofu wenzake kwa kueleza kuwa  kila kanisa  likiachwa litoe waraka wake nchi hii haitatawalika.


Akitoa salamu za pasaka katika kanisa hilo lililopo Ngarenaro jijini Arusha,Askofu Manase amesema kuwa ipo haja kwa  serikali na taasisi za dini kuketi kiti cha maridhiano kuliko hali ilivyo kwa sasa,ambapo kila upande unatoa matamko yake kwa lengo la kukosoa utawala uliopo madarakani.


“Kila kanisa ama taasisi yoyote ikiamua kutoa waraka wake hii nchi itaongozeka???...Suala la utawala na uongozi si jambo rahisi sana kwa sababu anayetawaliwa kila mtu anautashi wake’’Amesema


Ameongeza kwa kusema kuwa hakuna sababu ya kuitabiria nchi mabaya  kwani ukitenda jambo baya linaenea zaidi kuliko wema ,hivyo hakuna ulazima wa kujibu ubaya ila kama kuna mapungufu kwa pande zote mbili baina ya serikali na watawaliwa bora wakakaa chini na kufikia maridhiano.


Aidha alisisitiza kila kanisa linawajibu wa kuombea amani kwani amani ni msingi wa maisha na ikiachwa ikapotea ni vigumu kurejesha kirahisi,kwa sababu nchi zilizopoteza amani watu wake hawana maisha yenye furaha.


Awataka watu waliopewa dhamana ya kuongoza nchi ama jamii tuwaombee wasitumie nafasi zao kuibomoa nchi , waongoze kwa hekina ya kutatua changamoto zinazojitokeza ili kunusuru mpasuko unaotaka kujitokeza.


Amesema si jambo la msingi kwa kila dini ama taasisi yoyote kusimama na kutoa waraka wake ila watumie msingi wa mashauriano ikiwemo kukaa pamoja kwa pande mbili zinazovutana.

0 Comments:

Post a Comment