Viongozi wakuu wa China na Marekani walikubaliana katika mkutano wao wa mwezi April mwaka huu kushughulikia mpango wao wa siku 100, uliolenga kufikia kuondoa tatizo la kukosekana uwiano wa kibiashara na tatizo la Korea Kaskazini. Siku ya mwisho ya mpangokazi huo ilikuwa ni Jumapili iliyopita ambapo hakuna mafanikio ya msingi yaliyofikiwa.
Yafuatayo ni maoni ya Profesa Masaharu Hishida kutoka Kitivo cha Sheria cha Chuo Kikuu cha Hosei, juu ya mwelekeo wa sera ya China kuhusu Korea Kaskazini.
"Kwa kifupi, China imekuwa ikikerwa na hatua za kutojali za Korea Kaskazini, lakini pia imekuwa ikizingatia ushawishi wake kwa Korea Kaskazini kama moja ya raslimali kuu ya kidiplomasia.
Tuseme Korea Kaskazini ni mdogo wa mwisho wa China anayeonyesha kila aina ya tabia mbaya; China inataabika kumdhibiti mdogo mtu huyo na jirani anamuambia China,"Wewe ni kaka mkubwa hivyo unapaswa kuchukua hatua kumdhibiti."
Ninafikiri China imekuwa ikinufaika na muundo huo wa diplomasia na kuutumia kwenye uhusiano wa China na Marekani kwenye "mpango wa siku 100," ambao uliripotiwa kupendekezwa na China.
Chini ya mpango wa siku 100, China ilikubali kuiwekea shinikizo zaidi Korea Kaskazini. Kwa upande wake, Marekani ilikubali kuchukua msimamo wa wastani kuhusiana na maswala ya uchumi ya China. Kwa maneno mengine, walifikia makubaliano katika masuala ya usalama na biashara katika majadiliano hayo.
Ninadhani tunaweza kusema kuwa China pia imefanikiwa katika kuchelewesha hatua madhubuti zilizokuwa zimepangwa kuchukuliwa na Marekani dhidi ya Korea Kaskazini kwa kipindi fulani.
Hata hivyo Korea Kaskazini imekuwa ikifanya vitendo visivyozingatia weledi na vya kichokozi. Katika hali kama hiyo, baadhi ya wakosoaji au watafiti wamesema kwenye mitandao ya intaneti au kwenye magazeti kuwa Marekani imekataa kukubali pendekezo juu ya kuondokana na silaha za nyuklia kwenye Rasi ya Korea lililowasilishwa na Korea Kaskazini mwaka 1991.
Pia waligusia kuwa Marekani haijatekeleza makubaliano makubwa yaliyofikiwa mwaka 1994 kati ya Marekani na Korea Kaskazini jijini Geneva nchini Uswizi. Wanadai Marekani ndiyo inayopaswa kuchukua jukumu kubwa zaidi kwenye suala la nyuklia katika Rasi ya Korea.
Wizara ya mambo ya Nje ya China imesisitiza njia kuu ya kufikia suluhisho haipo mikononi mwa serikali ya China. Ninafikiri China inajaribu kuzuia kuibuka kwa nadharia inayoitwa, "Nadharia ya Jukumu la China" baada ya kumalizika kwa mpango wa siku 100.
Ama, China huenda ikadhani kuwa Marekani haitoamua kutumia kiasi fulani cha nguvu ya kijeshi dhidi ya Korea Kaskazini, licha ya kuwa China huenda ikawa na wasiwasi juu ya uwezekano wa kuchukuliwa hatua hizo baada ya kukubaliwa kwa mpango wa siku 100. Iwapo vita itazuka, kutakuwa na uharibifu mkubwa zaidi ya inavyotarajiwa. Kwa hiyo China, labda inaamini Marekani, haitokubali kuchukua jukumu hilo.
Ninafikiri China itashughulikia suala la Korea Kaskazini katika namna ambayo haitakubaliana na shinikizo la Marekani. Nchi hiyo inaweza kuonyesha dhamira ya kufikia uhusiano wa karibu na Urusi ambayo inasisitiza zaidi majadiliano kuliko shinikizo. Pia China huenda ikaashiria mwelekeo wa kupitia upya uhusiano na Korea Kusini uliozorota kufuatia hatua ya kupelekwa mfumo wa hali ya juu wa kukabiliana na makombora wa Marekani-THAAD."
Hayo ni maoni ya Profesa Masaharu Hishida kutoka Kitivo cha Sheria cha Chuo Kikuu cha Hosei, juu ya mwelekeo wa sera za China kuhusiana na Korea Kaskazini.

0 Comments:
Post a Comment