![]() |
| Mkurugenzi wa shule ya Lucky Vincent Bw. Innocent Mushi (kushoto) akiwa na mwalimu Mkuu Msaidizi wakitoka katika mahakama hiyo Mara baada ya kuahirishwa kwa kesi inayowakabili. |
MMILIKI wa shule ya Lucky Vicent, Innocent Moshi anayeshtakiwa kwa makosa matano ikiwemo kuruhusu gari lake kubeba abiria huku likiwa halina leseni wala bima anatarajiwa kusomewa maelezo ya awali agosti 24, mwaka huu.
Kwenye shauri hilo namba 78/2017 linalovuta hisia za wengi mmiliki huyo wa shule anakabiliwa na mashitaka manne huku moja wakishitakiwa pamoja Mwalimu Mkuu Msaidizi wa shule hiyo,Long'ino Mkama.
Hakimu, Jasmine Abdul, wa mahakama ya Arusha alipanga tarehe hiyo jana baada ya Wakili wa Serikali Alice Mtenga, kuieleza mahakama hiyo kuwa upelelezi wa shauri umekamilika.
Washitakiwa hao ambao wanatetewa na Wakili maarufu jijini hapa, Method Kimomogoro, wanadaiwa kuruhusu abiria 13 waliozidi kuingia kwenye gari kinyume na utaratibu na sheria za usalama barabarani na kusababisha vifo vya wanafunzi 32,walimu wawili na dereva mmoja .
Awali wakisomewa mashitaka yao Mei 12, mwaka huu na Mwanasheria wa Serikali, Rose Sule, alisema mahakamani hapo kuwa washtakiwa hao walitenda makosa hayo Mei 6, mwaka huu katika eneo la Kwa Morombo jijini Hapa.
![]() |
Alisema katika shitaka la pili Moshi anadaiwa kuruhusu gari hilo kuendeshwa bila kuwa na bima na shitaka la tatu ni kushindwa kuwa na mkataba na dereva wake ambaye kwa sasa ni marehemu,Dismas Gasper.
Mmiliki huyo wa Lucky Vicent alisomewa shitaka la nne analodaiwa kuruhusu gari lake kubeba abiria waliozidi uwezo wa gari ambapo abiria 13 walizidi.
“Mtuhumiwa unakabiliwa na kosa la nne ambalo ni la kubeba abiria waliozidi zaidi ya 13 ambapo Mei 6, Mwaka huu ukiwa Mkurugenzi, Afisa Msafirishaji na mmiliki wa Lucky Vicent ulibeba na kusafirisha abiria zaidi ya 13, kinyume cha sheria,” alidai Wakili wa Serikali Sule.
Wakili huyo wa Serikali akisomea shitaka mwalimu Mkama, alidai kuwa akiwa na nafasi ya MwalimuMkuu Msaidizi na mwandaaaji wa safari hiyo aliruhusu kupakia abiria zaidi ya 13 kwenye gari liliosababisha vifo vya watu 35.
Washitakiwa hao walikana mashitaka ambapo washitakiwa hao wapo nje baada ya kukidhi masharti ya dhamana yaliyowataka wawe na wadhamini wawili wenye vitambulisho na kusaini hati ya shilingi 15 milioni kila mmoja.
Aidha wametakiwa kutosafiri nje ya mkoa wa Arusha mpaka kesi hiyo itakapomalizika mahakamani hivyo wakatakiwa kukabidhi hati za kusafiria mahakamani hapo.
Mnamo Mei 6, mwaka huu wanafunzi 32 ,walimu wawili na dereva mmoja wa shule ya Lucky Vicent waliofariki kwa ajali eneo la Rhotya ,wakielekea mjini Karatu katika shule ya msingi Tumaini kufanya mtihani wa ujirani mwema.



0 Comments:
Post a Comment