UPDATES: Korea Kaskazini imefanya jaribio lingine la Kombora

Jeshi la Korea Kusini limesema Korea Kaskazini leo Alhamisi imefanya majaribio ya kile kinachoonekana kuwa ni makombora kadhaa ya masafa mafupi yenye injini yarukayo kutoka nchi kavu kwenda baharini kuelekea Bahari ya Japani.

Awali shirika la habari la Yonhap la Korea Kusini liliripoti kuwa makombora hayo huenda yalikuwa ni ya kawaida, lakini jeshi la nchi hiyo linaamini kuwa makombora hayo ni yale yenye injini yarukayo kutoka nchi kavu kwenda baharini.

Mkuu wa Majeshi ya Korea Kusini amesema makombora hayo yalirushwa leo Alhamisi asubuhi kutoka kwenye mji wa Wonsan, mashariki mwa Korea Kaskazini na yalisafiri umbali wa takribani kilomita 200. Majeshi ya Korea Kusini na Marekani yanachunguza tukio hilo.

Mei 29 mwaka huu Korea Kaskazini ilitekeleza jaribio la urushaji wa kombora kutoka eneo hilo. Kombora hilo liliruka umbali wa takribani kilomita 450 na kufikia urefu wa takribani kilomita 120 kutoka usawa wa bahari na kuanguka kwenye Bahari ya Japani ndani ya ukanda maalum wa kiuchumi wa Japani.

Korea Kaskazini ilitangaza kuwa imefanikiwa kufanya jaribio la kombora jipya linaloongozwa kwa usahihi zaidi, chini ya usimamizi wa Kiongozi Mkuu wa nchi hiyo, Kim Jong Un.

Mei 30 mwaka huu Marekani ilitangaza kufanikiwa katika mazoezi yake ya kudungua kombora lenye uwezo wa kuvuka mabara, ICBM. Marekani pia ilipeleka manowari mbili za kubebea ndege kwenye Bahari ya Japani kwa ajili ya mazoezi ya kijeshi.

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa juma lililopita liliidhinisha kwa kauli moja azimio la vikwazo vipya linalowalenga watu binafsi na makundi zaidi yanayohusika katika mpango wa uendelezaji nyuklia na makombora wa Korea Kaskazini.

Korea Kaskazini ilipinga hatua za Umoja wa Mataifa kupitia chombo cha habari kinachomilikiwa na serikali ya nchi hiyo, ikisema kuwa ni kitendo cha uhasama na ikaapa kuendelea na mipango yake ya uendelezaji wa nyuklia na makombora.

0 Comments:

Post a Comment