WATUHUMIWA WA UGAIDI WATISHIA KUGOMA KUFIKA MAHAKAMANI

WASHTAKIWA 61 wa kesi za  ugaidi wamesema hawatafika tena mahakamani  mpaka watakapopewa taarifa kuwa upelelezi wa kesi zao umekamilika kwani wamesota mahabusu gereza la Kisongo kwa zaidi ya miaka minne huku kesi ikishindwa kuendelea kutokana na kile kinachoelezwa upelelezi haujakamilika.
Waliyasema hayo jana mbele Hakimu Mkazi, Nestory Barro, wa Makahama ya Hakimu Mkazi Arusha anayesikiliza mashauri yao kuua, kujaribu kuua, kujisajili na kusafirisha vijana kujiunga na kikundi cha kigaidi cha Al- Shabaab.
Wapiganaji wa Al-Shabaab Picha kwa hisani ya CFR Backgrounders

Mmoja wa washtakiwa hao ambaye jina lake halikuweza kupatikana mara aliieleza mahakama hiyo kuwa  wanataka kutoa taarifa kuwa wamevumilia mateso kwa muda wa miaka minne ,familia zao zimesambaratika hivyo leo (jana) ndiyo siku yao ya mwisho kufika mahakamani hapo.
Maombi na malalamiko ya washitakiwa hao yalitokana na hatua ya Wakili wa Serikali, Penina Joachim, kuiomba mahakama hiyo kupanga tarehe nyingine ya kutajwa kwa mashauri hayo kwani  upelelezi wa kesi hizo bado haujakamilika.

"Tunaomba kutoa taarifa kuwa leo ndiyo mara ya mwisho kuja mahakamani mpaka waendesha mashitaka watakaposema upelelezi umekamilika,hivyo usiandike tarehe ya sisi kuletwa mahakamani maana hatutarudi,nimeagizwa niwawakilishe wenzangu.

"Juzi tulifanya kikao jela na kukubaliana hili,gharama ni kubwa ya kutuleta hapa,tunawapa hofu watu barabarani jinsi tunavyoletwa kwa ulinzi mkali mahakamani,hatuwezi kukanyaga hapa labda kesi ipelekwe Mahakama Kuu ikaanze kusikilizwa," alisisitiza mshitakiwa huyo.
Washitakiwa hao walimlalamika Mkuu wa Makosa ya Upelelezi mkoa wa Arusha(RCO), kuwa licha ya kuwatembelea gerezabi Januari mwaka huu na kuwaahidi ndani ya miezi miwili upelelezi utakuwa umeshakamilika lakini mpaka sasa upelelezi haujakamilika.

Walisema RCO alishaongea nao  sana kuhusu msukumo  wa kesi hizo lakini bado wanaona sheria zinatumika kuwakandamiza.

"" Kama huku ni kizuizini basi watuambie tumekaa kizuizini kwa muda usiojulikana,ni bora kufia jela kuliko dhuluma hii,nataka nguvu ya dola itumike nione wataitumiaje kutulazimisha kuja mahakamani,"alisisitiza mshitakiwa mwingine huku akitokwa na machozi.

Mshitakiwa mwingine alidai kuwa alikamatwa na mtoto wa IGP Mahita ambaye hakumtaja jina ila alidai kuwa  alimuambia kuwa wataendelea kumshikilia mpaka wake zake wawili watakapoolewa na kuwa ni kweli wameshaolewa hivyo anashangaa kwa nini bado wanaendelea kumshikilia.
"Wanaotufanyia hivi watambue iko siku yao nao dunia itageuka giza litawafika, waangalie mfano wa Nape (aliyekuwa Waziri wa Habari,Sanaa na Michezo,Nape Nnauye),aligeukwa akashikiwa bastola,iko siku nao watakuwa chini," alisema mshitakiwa mwingine.

Baada ya kusikiliza hoja za watuhumiwa hao Hakimu Baro,alisema kuwa atampigia simu RCO ili amuulize kuhusu suala hilo huku akiwafafanulia kuwa suala la kufika mahakamani siyo hiari ni la lazima.
"Huku lazima mtakuja haki ya Mungu, suala la kuja mahakamani siyo hiari, nitampigia RCO nimwambie mmekuwa wakali mnataka kunitoa roho ila hayo maamuzi yenu mengine siyo mazuri,"alisema Hakimu Barro
Hata hivyo mmoja wa watuhumiwa hao alipingana na watuhumiwa wenzake na kudai kuwa yeye atafika mahakamani hapo tarehe nyingine kesi hiyo itakapopangwa kutajwa huku wenzake wakilalamikia ndugu zao kutokuruhusiwa kuingia mahakamani jambo linalowafanya washindwe kufahamu kinachoendelea.

Washitakiwa hao walio kwenye makundi tofauti  wanashitakiwa  chini ya makosa ya Sheria ya kuzuia ugaidi,ambapo Sheria namba 22 ya Mwaka 2002 inaeleza kuwa upelelezi wa shauri ukikamilika,Mahakama Kuu ndiyo yenye mamlaka ya kusikiliza kesi hizo na kutoa uamuzi.

Mbali na mashitaka hayo pia wanadaiwa kuhusishwa na tukio la milipuko ya mabomu kwenye Baa ya Arusha Night Park,Viwanja vya Soweto jijini Arusha katika mkutano wa Kampeni za uchaguzi mdogo wa madiwani,Kanisa la Mtakatifu Joseph Mfanyakazi lililopo eneo la Olasiti milipuko iliyosababisha vifo vya watu na majeruhi.
Kesi hizo ziliahirishwa hadi Aprili 11 mwaka huu zitakapotajwa tena.


0 Comments:

Post a Comment