MBOWE AJENGEA WANANCHI WAKE NYUMBA ZOTE ZILIZOCHUKULIWA NA MAFURIKO

 KIONGOZI wa Kambi Rasmi ya Upinzani bungeni, Freeman Mbowe, (CHADEMA), ametoa msaada wa matofali ya kujengea nyumba zote zilizoanguka kutokana na mafuriko yaliyotokana na mvua zinazoendelea kunyesha kwenye jimbo lake la Hai, ambapo jumla ya nyumba 50 ziliathirika.
Pia, ametoa sh milioni 2 zitumike kujengea choo cha shule ya msingi Elerai ambacho kimezama kutokana na mafuriko hali iliyoiweka kwenye hatari ya kufungwa kutokana na kukosekana kwa huduma hiyo.
Aidha, Mkuu wa wilaya hiyo, Antony Mtaka, alimmwagia sifa kiongozi huyo akimuombea Mungu azidi kumbariki kwani ameonyesha uongozi kwa kuwapa wapiga kura wake kitu cha kudumu watakachobaki nacho kama ukumbusho wakiendelea kumkumbuka hata ikitokea amekuwa Rais wa nchi.
Tukio hilo lilitokea juzi kwenye kijiji cha Rundugai ambapo Mbowe alimkabidhi Katibu Tawala, Zuhura Chikira fedha taslim sh milioni 7,250,000 kwa ajili ya shughuli hizo mbele ya Mkuu wa wilaya ambapo vijiji vilivyoathiriwa ni Rundugai, Kawaya na Chemka vilivyopo Kata ya Masama Rundugai.
 Mbowe alitoa msaada huo baada ya majadiliano baina yake na wananchi hao ambao walimweleza kuwa akiwapatia matofali ya kujengea nyumba itakuwa imewasaidia kurudi kuungana pamoja na familia zao hivyo kuondoka kwenye nyumba za majirani wanakohifadhiwa kwa sasa.
Mbunge huyo alirejea taarifa za athari ya mafuriko iliyoandaliwa na ofisi ya Mkuu wa Wilaya ilionyesha kuwa nyumba zilizoathiriwa ni 50 ambapo fundi aliyekuwa kwenye mkutano huo alimweleza Mbowe kila nyumba inahitaji matofali 350 na kila tofali ni sh 300 ndipo mbunge huyo akatoa fedha taslimu sh 5,250,000.
Aliwashukuru wale wote waliotoa msaada wa hali na mali kwa wananchi hao huku akiahidi kufuatilia misaada zaidi kwenye ofisi ya Waziri Mkuu kitengo cha maafa ili kuona namna miundo mbinu ya barabara, reli, mifereji ya umwagiliaji kwenye eneo hilo itakavyoweza kuboreshwa kwa haraka kwani kwa sasa imeharibiwa kabisa na mvua.
Hata hivyo Kwa suala la choo cha shule, aliiomba ofisi ya mkurugenzi wa halamashauri ambayo Mwenyekiti alikuwepo, (Clemence Kwayu) mbunge wa viti maalum, Lucy Owenya na baadhi ya madiwani pamoja na mkuu wa wilaya Mtaka wasiifunge shule hiyo kwani itawaathiri watoto kitaaluma.

 Mbowe aliamua kuchangisha fedha kutoka kwa watu alioongozana nao kwenye msafara wake na ule wa mkuu wa wilaya ambapo zilipatika sh laki 5 na yeye alijazia sh milioni 1.5 zikatimia sh milioni 2 alizozitoa ili zitumike kujengea choo hicho kwani tayari kulikuwa na misaada mingine iliyotolewa na wadau wengine ikiwemo saruji kwa ajili ya ujenzi wa choo hicho.
Kwa upande wake Mkuu wa wilaya Mtaka akiongea na wananchi hao aliwashukuru kwa msaada waliowapatia wahanga hao wa mafuriko kutokea tukio hilo litokee huku akimwagia sifa Mbowe."Jambo la msingi sana nimshukuru Kaka Mbowe, Freeman umekuwa kaka yetu wa ukweli, umeguswa, huu ndiyo utumishi wa watu kwa sababu watu walipanga foleni wakakuchagua kuwa mbunge wao ..."Mrejesho wako kwao umekuwa ni jambo lenye faraja mimi ninaamini hata Mungu atakubariki nisifanye kufuru kwa kukuita malaika lakini nasema Mungu akubariki kwa jambo hili jema ambalo umelifanya," alisema Mkuu huyo wa wilaya.
Aliahidi kuwa Serikali itasimamia kuona msaada huo unatumiwa kama ulivyokusudiwa huku akiwaonya wananchihao kuhakikisha matofali hayo yanatumika kujengea nyumba za wahanga wa mafuriko.  "Haitapendeza mbunge amewapa fedha za kununua tofali, kesho ukachukua tofali ukaenda kumuuzia mtu mwingine halafu ikifika mwezi wa nane ukamdai tofali, umepewa tofali kajenge nyumba kweli ili ikifika wakati useme kweli mimi nilipata mafuriko mwaka fulani aliyekuwa mbunge wetu mheshimiwa Mbowe inaweza ikawa ameshakuwa Rais kipindi hicho," alisema Mtaka huku akishangiliwa na wananchi.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Halmashauri, Kwayu alisema kuwa wakati umefika sasa serikali kutumia wataalam kutengeneza mfumo wa kukinga maji itakayowezesha maji kuhifadhiwa hasa nyakati za mvua ili yaje yatumike kipindi cha kiangazi.  Akisema kuwa maeneo hayo ya Rundugai huwa yanakabiliwa na tatizo kubwa la maji lakini nyakati za mvua kama hizi hakuna jitihada zozote zinazofanywa kuhifadhi maji ya mvua badala yake huachiwa yanaenda yote baharini.

0 Comments:

Post a Comment