UCHAGUZI CHADEMA; Mikutano ya kihistoria CHADEMA kuanza leo

Septemba 2014; mwezi na mwaka mwingine kuendeleza historia ya mapambano

Mkutano Mkuu wa Baraza la Wazee wa CHADEMA unaofanyika Jumamosi Septemba 6, mwaka huu katika Ukumbi wa Mlimani City jijini Dar es Salaam, unapuliza kipyenga cha mfululizo wa mikutano kadhaa ya kitaifa ambayo itahitimishwa Septemba 14, kwa Wajumbe wa Mkutano Mkuu kumchagua Mwenyekiti wa Chama Taifa na makamu wake wa Tanganyika na Zanzibar.

Mkutano huo wa Baraza la Wazee ambao utachangua uongozi wa ‘washauri’ wa chama kwa miaka mitano ijayo, ni mwendelezo wa mchakato wa uchaguzi wa ndani ya chama ulioanza kwenye ngazi ya misingi (vitongoji na mitaa) nchi nzima kisha ukafuatiwa na matawi (vijiji na mitaa), kata, majimbo/wilaya, mikoa na sasa hatimaye ngazi ya taifa.

Baada ya Baraza la Wazee kuchagua uongozi wao utakaokuwa madarakani kwa mujibu wa Katiba ya Chama hadi uchaguzi mwingine, watafuatia ‘wapiganaji’ wengine ambao ni Baraza la Vijana wa CHADEMA (BAVICHA), ambao watakutana kwenye mkutano wao mkuu Septemba 10 mwaka huu kuchagua uongozi wao wa miaka mitano ijayo.

Baraza la Wanawake wa CHADEMA (BAWACHA) watafuata baada ya BAVICHA. Septemba 11 Mkutano Mkuu wa BAWACHA utakutana ambapo utachagua Mwenyekiti wa baraza na makamu wake wa Tanganyika na Zanzibar. Mkutano huo utafuatiwa na kikao cha Kamati Kuu ya sasa itakayoketi kwa mara ya mwisho (kabla ya nyingine mpya kuchaguliwa) Septemba 12, mwaka huu.

Kikao hicho cha Kamati Kuu pamoja na masuala mengine, kitafanya maandalizi ya kikao kingine cha juu kitakachoketi siku inayofuata, Septemba 13, ambacho ni Baraza Kuu la Chama.

Baraza Kuu la Chama nalo pamoja na masuala mengine, litakuwa ni mtangulizi wa Mkutano Mkuu wa CHADEMA utakaoketi Septemba 14 kuhitimisha uchaguzi wa ndani ya chama na kupuliza kipyenga cha ‘mchakamchaka’ wa kuelekea uchaguzi wa serikali za mitaa, uandikishaji wa daftari la wapiga kura na hatimaye uchaguzi mkuu wa mwaka kesho.

Baraza Kuu la Chama litakutana tena katika kikao chake cha kwanza Septemba 15 kwa ajili ya kupiga kura kuthibitisha uteuzi wa Katibu Mkuu wa Chama na naibu wake wa Tanganyika na Zanzibar na kuchagua wajumbe wa Kamati Kuu.

Matukio hayo ya kihistoria ya uchaguzi wa ndani ya chama yatahitimishwa Septemba 16 kwa Kamati Kuu mpya kuketi kwa mara ya kwanza kuweka mipango mikakati ya kuingia kazini rasmi. Hakuna kulala mpaka kieleweke.

0 Comments:

Post a Comment