JUMUIYA YA KIKRISTO TANZANIA-TAARIFA KWA UMMA KUHUSU WAJUMBE WA BUNGE
MAALUM LA KATIBA KUTOKA CCTJumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT) inachukua
fursa hii kuvishukuru vyombo mbalimbali vya habari kwa jinsi ambavyo
vimekuwa vikitoa taarifa mbalimbali kuhusu kazi na matamko ya CCT.
Kuhusiana na mchakato wa kuandikwa kwa Katiba mpya, CCT inaamini kuwa
suala hili ni la MARIDHIANO na sio la ubabe wa kikundi au chama fulani
cha siasa.-Kama ambavyo ilitangazwa na Mhe. Rais Januari 2014 kuwa
Taasisi mbalimbali zipeleke mapendekezo ya wajumbe wanaoweza kuteuliwa
kuwa wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba, CCT ilipeleka mapendekezo ya
wajumbe tisa na kati ya hao Mhe. Rais alimteua mjumbe mmoja tu ambaye ni
Bibi Esther Msambazi. Mjumbe huyu aliyeteuliwa ni Mkristo wa kawaida
(lay Christian) na wala si Kiongozi wa Dhehebu lolote la Wanachama wa
CCT na pia hata sio Mzee wa Kanisa analotoka bali Mkristo mwaminifu wa
kawaida. Huyu ndiye mwakilishi wa CCT kwenye Bunge Maalum la Katiba.
Viongozi wengine wa Dini ya Kikristo (Maaskofu na Wachungaji) waliopo
katika Bunge hilo HAWAKUTUMWA NA CCT na wala CCT haina taarifa ni vipi
walichaguliwa kuwa wajumbe wa Bunge hilo Maalum.-Aidha, pia Jukwaa la
Wakristo Tanzania haliwatambui Viongozi hao kwani Jukwaa hilo linaundwa
na Taasisi za TEC, CCT, PCT na SDA. Kutokana na misingi ya imani ya
taasisi hizi kwa umoja wake, Viongozi wakishakubaliana jambo fulani kwa
pamoja na kwa umoja wao wanalisimamia na kulitekeleza. NDIYO YAO NI
NDIYO NA HAPANA NI HAPANA kwa kuwa hawana ndimi mbili na wala
hawatumikii Mabwana wawili. Kwa mantiki hiyo, CCT ikiwa mmoja wa taasisi
zinazounda Jukwaa la Kikristo Tanzania inaendelea kusisitiza kuwa
msimamo wa viongozi wa dini kama ulivyotolewa na Jukwaa la Kikristo
Tanzania kuhusiana na Maoni waliyopeleka kwa Tume ya Kukusanya Maoni ya
Wananchi chini ya Uenyekiti wa Mhe. Jaji Mstaafu Warioba na Matamko
waliyotoa ni sahihi na itaendelea kuyasimamia na kuyasambaza hadi
yamfikie kila Mkristo ili wananchi wa Tanzania wapate Katiba
wanayoitaka. Aidha, Viongozi hao wa Jukwaa la Wakristo Tanzania haliwezi
kutafuta maoni ya Viongozi wa Dini walioko katika Bunge Maalum la
Katiba kwa sababu hawawatambui kama wawakilishi wa taasisi zao na hivyo
kukataa kwa nguvu zote yale ambayo viongozi hao waliopo Bungeni watakuwa
wakiyasema. Mwisho kabisa tunawaomba viongozi hao wajiulize, “hivi sisi
tumetumwa na tunamwakilisha nani humu Bungeni?”-Imetolewa leo-September
05, 2014Na: JUMUIYA YA KIKRISTO