Pinda aimwagia sifa hotel ya Ngurdoto



WAZIRI Mkuu, Mizengo Pinda, ameipongeza hoteli ya Kitalii ya Ngurdoto yenye hadhi ya nyota tano, iliyopo nje kidogo ya jiji la
Arusha,kwa kuweza kujenga ukumbi mkubwa wa kisasa  wa mikutano ya kimataifa wenye uwezo wa kutumiwa na watu zaidi ya 3000 kwa wakati mmoja.

 

Aidha, amekitaka kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Arusha,  (AICC), kuboresha kumbi zake ili ziende  na wakati kulingana na mahitaji ya soko la kimataifa vinginevyo wanaweza kukosa mikutano.

 

Waziri Mkuu, Pinda aliyasema hayo mwanzoni mwa wiki Jijini hapa wakati alipokuwa akifungua mkutano wa wadau wa
maji unaofanyika katika ukumbi huo.

 

Alisema kuwa katika kuwatia moyo wawekezaji kama hao walioamua kuwekeza fedha zao kwenye sekta ya utalii hasa ujenzi wa kumbi za mikutano ambayo  inaliongezea Taifa sifa, Serikali  itajitahidi kuleta mikutano ya kutosha nchini.


"Kwa kweli hili jengo ni la kisasa sana, nimetembea sehemu nyingi hapa nchini sijawahi kuona ukumbi wa kisasa kama huu , kwa kweli Mrema (mmiliki wa hotel hiyo) ametuokoa sana ,hii ni changamoto kwa AICC wajitahidi kuboresha kumbi zao vinginevyo watapigwa mweleka,''alisema Waziri Mkuu Pinda.

Awali, akimkaribisha Waziri Mkuu kuzungumza kwenye mkutano huo, Mkuu wa mkoa wa Arusha, Magesa Mulongo, alisema kuwa mkoa huu umekidhi vigezo vya kimataifa vya kuweza kuandaa na kuhudumia mikutano ya kimataifa jambo aliloomba Serikali kuangalia uwezekano wa kuleta mikutano mingi.

Alisema kuwa Arusha inakidhi vigezo vingi vinavyohitajika kufanikisha mikutano ya kimataifa ikiwemo kuwa na hoteli nyingi zenye kumbi za kisasa  pamoja na huo waliokuwa wakiutumia unaofahamika kama "Tanzania Convention Center" ambao haupatikani popote nchini.

"Karibuni sana Arusha yale mambo yetu ya zamani tumeshaacha na wale waliodhani  wangekutana na  mabomu sasa hayapo tena, karibuni kwenye ukumbi mpya wa kisasa zaidi, mheshimiwa Waziri Mkuu lazima mikoa mingine wakubali kutuachia mkoa wa Arusha kuandaa mikutano mbalimbali kwa sababu vigezo vyote tunavyo''alisema Mulongo.

Alisema kuwa mkoa huu kitovu  cha utalii nchini na utavivutio vingi vya kumfanya mgeni afurahie madhari yaliyopo hivyo aliwataka hata hao waliohudhuria mkutano huo kutumia fursa ya kufika jijini hapa kwa kuvitembelea sanjari na kuhamasisha wadau wengine kufika Arusha kwa ajili ya mikutano na utalii.

 


0 Comments:

Post a Comment