MBUNGE wa Jimbo la Arusha Mjini, Godbless Lema, (Chadema) amesema kuwa Mkuu wa mkoa huu, Magesa Mulongo, Mkuu wa wilaya, John Mongela, Kamanda wa polisi mkoa, Liberatus Sabas na Mkuu wa polisi wa wilaya, (OCD) wanapaswa kuondolewa kwenye nafasi hizo kwa kushindwa kudhibiti matukio ya mauaji ya raia yanayoendelea mfululizo bila wahusika kukamatwa.
Aidha, amedai kuwa yeye kama mwakilishi wa wananchi amemwandikia RPC barua kuomba taarifa ya wananchi waliouawa kwa kupigwa risasi na watu wanaokuwa kwenye bodaboda kwa zaidi ya mwezi mmoja sasa hajapatiwa ila huzipeleka kwa wafanyabiashara hivyo humlazimu yeye kuzifuata huko.
Aliyasema hayo juzi muda mfupi baada ya kutembelea familia ya Nickson Mtaita na kutoa pole kutokana na kifo cha mtoto wao, Christine (3) aliyepigwa risasi kichwani na watu waliokuwa kwenye bodaboda ijumaa iliyopita akiwa amelala kwenye kiti cha gari yao.
Lema alisema kuwa tatizo lililopo ni viongozi hao aliodai kuwa wameshindwa kuyapa uzito unaostahili matukio hayo kutokana na kuzoea damu hivyo inapaswa waletwe wengine watakaoyashughulikia na kuhakikisha hali ya jiji hili kiusalama inakuwa shwari.
"Mimi mbunge mwakilishi wa wananchi nimeomba hii taarifa kwa RPC sipatiwi lakini nilienda kwa( anamtaja jina mfanyabiashara wa madini) nikiwa nimeambatana na mbunge mwenzangu, Beatrice Shelukindo nikamkuta RPC yuko ndani ya ofisi akatokea kwa mlango wa nyuma.
" Tulipoingia (anamtaja jina mfanyabiashara huyo) aliniambia RPC amemweleza kuwa wamekamata watuhumiwa wa mabomu kwa hiyo hali itakushwari wasiwasi utaisha, nikatarafakari hizi taarifa sipatiwi kama mwakilishi wa wananchi ila wafanyabiashara wanapewa," alisema Lema.
Alisema kuwa hata akimpigia simu RPC hapokei lakini yupo tayari kwenda kwa wafanyabiashara kwa madai kuwa huenda hufuata fedha huku akihoji hatua ya baadhi ya wafanyabiashara kutundika picha za RPC na OCD aliyehama, Gires Muloto kwenye ofisi zao.
"Ukienda kwenye ofisi nyingi za wafanyabiashara wakubwa hasa wa mawe,utakuta kuna picha ya Sabas,,Mroto na picha ya Rais Kikwete,maana yake ni kwamba wanatishia wafanyabiashara, nataka niwape wananchi namba ya Chikawe ili wawe wanampa taarifa kwani wanahofia kutoa taarifa kwa Polisi"alidai
"Kuna matukio mengi ya uhalifu na mauaji yanaendelea hapa Arusha, nyumba kati ya 5 hadi 10 zinavamiwa au watu kuporwa hutokea na yameshika kasi zaidi toka machinga wameondolewa na kunyang'anywa bidhaa zao," alisema Lema
Mbunge huyo aliwataka wananchi wanapokuwa na taarifa zitakazosaidia kuwabaini wahalifu wampigie simu Waziri wa Mambo ya ndani,Mathias Chikawe,kwa namba 0685777222 ili ziweze kufanyiwa kazi.
"Jeshi la polisi Arusha lina mahusiano mabaya na wananchi, mmesikia yule polisi aliyekuwa akiandika maelezo (kutoka kwa mke wa Mtaita, Ruth akiwa ndani ya gari lililotumika siku ya tukio) juu ya tukio la kifo cha Yule mtoto akisema kuwa hakuna raia aliyepiga simu polisi kuwaarifu juu ya tukio la risasi ingawa waliona.
"Hili si jambo jema hata kidogo jeshi la polisi ni vema likafumuliwa ili kuwafanya wananchi kuliamini kwani kwa sasa mtu anaweza kutoa taarifa halafu akahojiwa muda mrefu na wakati mwingine kushikiliwa kama mualifu jambo linalowafanya kukwepa kutoa taarifa," alisema Lema.
Waziri wa Mambo ya Ndani, Chikawe alipoongea na Tanzania Daima kwa njia ya simu alisema kuwa atafuatilia suala hilo ili kujua undani wake huku akiahidi kuongea na mbunge huyo ambaye pia ni Waziri Kivuli wa Mambo ya ndani.
Hata hivyo juhudi za kumpata RPC Sabas, Mkuu wa mkoa, Mulongo na Mkuu wa wilaya ya Arusha, Mongela hazikuzaa matuba baada ya simu zao kuita bila kupokelewa na wakati mwingine zikikatwa hata walipotumiwa ujumbe mfupi wa maneno kwa njia ya simu hawakujibu.
Awali, Mtaita alimweleza Lema nje ya chumba cha kuhifadhia maiti cha hopitali ya mount Meru muda mfupi baada ya kusimamia uchunguzi wa mwili wa mtoto wake, kuwa wanatazamia kumzika mtoto wao huyo jana (jumatatu) Uru mkoani Kilimanjaro baada ya kukamilisha taratibu zote.
Alimweleza namna tukio hilo lilivyotokea majira ya saa 1 usiku maeneo ya Olasite karibu na kona ya kuelekea nyumbani kwao ambapo walisimama kwa ajili ya kununua maji ya kunywa wakati wakishauriana nani kati ya yeye na mke wake ashuke kununua maji aliona mtu akimsemesha kwa dirishani.
"Nilishusha kioo ili kumsikiliza ingawa alikuwa aking'ang'ania kufungua mlango lakini alishindwa kwa kuwa nilikuwa 'nimelock' akaniambia anataka fedha mke wangu alikuwa ameshika shilingi elfu 2 nikaichukua nikampa nikaona amekasirika akatoa bastola akazunguka upande wa pili alikokuwa amekaa mke wangu.
"Ilibidi niondoe gari kwa kasi na yuke kijana akapanda pikipiki akaanza kunifuata kwa kasi kwa kweli nilijitahidi ndipo akapiga risasi kwenye mlango wa nyuma eneo alilokuwa amelala mtoto wetu mdogo ingawa hatukujua imempata mpaka tulipoenda mbele ndiyo tukamuona anatoka damu kwenye macho," alisema Mtaita.
Tanzania Daima ilishuhudia tundu la risasi kwenye mlango huo wa nyuma ambapo mke wa Mtaita, Ruth alisema kuwa watu hao hawakuwa wamejiziba uso ingawa si watu wanaowafahamu.
Kumekuwa na matukio ya wanawake wanaoendesha magari jijini hapa kupigwa risasi wakiwa barabarani na watu wanaokuwa kwenye bodaboda ambapo tayari watano wamejeruhiwa huku wawili wakiripotiwa kufariki dunia
AKIBA COMMERCIAL BANK PLC YAWATOA HOFU WATEJA WAKE WA KARIAKOO
-
Akiba Commercial Bank Plc imeendelea kujitoa si tu kuhudumia wateja wake
bali pia kushiriki katika juhudi za kijamii wakati wa dharura na majanga,
ikiwa ...
8 hours ago
0 Comments:
Post a Comment