A TO Z WASALIM AMRI KWA MORANI WA KIMASAI


 
 
 
Wananchi zaidi ya 500 kutoka mitaa mbalimbali ya Kata ya Mateves jijini Arusha jana Jumamosi walifunga lango Kuu la kuingia kwenye Kiwanda cha A to Z kinachotengeneza bidhaa za aina mbalimbali zikiwemo Vyandarua na Nguo wakipinga Kiwanda hicho kutiririsha maji taka kwenye makazi yao.

Wakiwa na silaha za jadi walipita kwenye lango la kwanza wakiwa na lengo la kuingia ndani ya kiwanda hicho lakini hawakuweza kuvuka lango la pili ambalo ulinzi ulikuwa umeimarishwa na kampuni binafsi ya ulinzi.

Magari mawili ya Polisi kutoka Kituo Kikuu cha Arusha walifika kuhakikisha usalama katika kiwanda hicho kinachozalisha idadi kubwa ya Vyandarua chini ya mpango maalumu wa kupambana na Maralia barani Afrika,kikiwa kimewahi kutembelewa na Rais wa zamani wa Marekani,George Bush.

Wananchi hao,wakiongozwa na Mwenyekiti wa rika la vijana(Morani),Festo Olodi wanalalamikia uongozi wa Kiwanda hicho,kuruhusu maji yanayotokana na uzalishaji kuingia kwenye makazi yao hali inayosababisha athari za kiafya kwa wananchi na mifugo.

Mkuu wa wilaya ya Arusha,John Mongela alifika na kutembelea eneo linalolalamikiwa,kuzungumza na uongozi wa Kiwanda hicho na baadae kuagiza yajengwe mabwawa na ukuta wa kuzuia maji hayo kuingia kwenye makazi ya wananchi ndani ya siku saba.

"Nataka tukubaliane hali ilivyo haitawezekana kuzuia maji hayo kwa siku moja,hata nyie mnaoshinikiza mjenge ukuta leo,baada ya kuujenga utaanguka tu,sitaki tuwe na majibu mepesi tuwe na subira ndani ya siku saba tutarudi hapa kuona hali ilivyo,naamini hakutakuwa na maji taka yanayotoka kiwandani"

Hali hiyo ilizua manung'uniko miongoni mwa wananchi hao,kwamba kuwapa siku saba ni nyingi wakati afya za wananchi zikiwa hatarini na baadhi ya mifuko ikifa kutokana na kunywa maji yanayotoka kiwandani.

Katika hatua nyingine iliyozua hasira kwa wananchi hao ni kitendo cha walinzi kumzuia Diwani wa Kata ya Mateves kuungana na Mkuu wa wilaya kuingia ndani ya kiwanda hicho kukagua eneo linalopitisha maji machafu na kushiriki vikao vya kutafuta suluhu.

Mkazi mwingine,Meleiyo Korongo alidai eneo lao linakabiliwa na ukame hivyo kukosa maji safi na salama na kwamba hatua ya kiwanda hicho kutirisha maji machafu kuingia kwenye korongo linalotumiwa na wananchi wa eneo la Oljoro ni kuhatarisha afya zao.

Kwa muda wa takribani saa tano hakuna gari lililoruhusiwa kuingia au kutoka kiwandani hapo kutokana na wananchi hao kudhibiti lango kuu.Uongozi wa kiwanda hicho ukiongozwa na Afisa Utawala,Godwin Abed alisema watahakikisha wanadhibiti maji hayo ndani ya siku walizokubaliana.

0 Comments:

Post a Comment