TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Katika kutekeleza kazi ya mbunge ya kuisimamia Serikali itakumbukwa
kwamba tarehe 12 Mei 2014 nilichukua hatua bungeni ya kutaka Serikali
kutatua kwa dharura matatizo katika mtambo wa maji wa Ruvu Juu yenye
kukosesha maji kwa wananchi wa Mkoa wa Dar Es Salaam na Pwani.
Nilitaka kwa mujibu wa Kanuni ya 49 ya Kanuni za Kudumu za Bunge Toleo
la mwaka 2013, Waziri wa Maji Prof Jumanne Maghembe atoe kauli bungeni
juu ya matatizo ya maji katika maeneo yanayohudumiwa na mabomba kutoka
katika mtambo kwa kuweka bayana iwapo kuna hujuma na kurejesha kwa
haraka huduma kwa wananchi.
Kufuatia hatua hiyo hali ya upatikanaji wa maji iliongezeka katika
maeneo machache ndani ya siku chache lakini kwa sasa katika maeneo
mengi yanayohudumiwa na mabomba kutoka katika mtambo wa Ruvu Juu
katika kata za Kwembe, Kibamba, Mbezi Lois, Msigani, Kimara, Saranga,
Ubungo na Makuburi matatizo ya maji yamejirudia.
Katika kuendelea kutekeleza wajibu wa kibunge wa kuishauri na
kuisimamia Serikali natoa mwito wa wazi kwa wenyeviti wa bodi za
Wakurugenzi na Maafisa Watendaji Wakuu wa Mamlaka ya Maji Safi na Maji
Taka Dar Es Salaam (DAWASA) na Kampuni ya Maji Safi na Maji Taka
(DAWASCO) ndani ya siku tatu kusimamia kazi ya dharura kuhusu matatizo
ya mtambo wa maji wa Ruvu Juu yanayoendelea mpaka hivi sasa.
Aidha, ndani ya siku hizo tatu wajitokeze mbele ya vyombo vya habari
kutoa maelezo kwa umma kueleza kwanini mpaka sasa huduma ya maji
katika maeneo mengi katika Jimbo la Ubungo na Jiji la Dar Es Salaam
kwa ujumla yanayohudumiwa na mabomba yanayotoka katika mtambo wa Ruvu
Juu hayapati huduma ya maji inavyostahili na lini matatizo yaliyopo
yatapatiwa ufumbuzi.
Kwa upande mwingine, ndani ya muda huo huo wa siku tatu Katibu Mkuu wa
Wizara ya Maji ajitokeze mbele ya vyombo vya habari na kueleza umma
matokeo ya uchunguzi uliopaswa kufanyika ndani ya mwezi mmoja kubaini
kama matatizo ya mara kwa mara ya Mtambo wa maji wa Ruvu Juu
yanatokana na masuala ya kiufundi, kiuendeshaji au makosa mengine ya
kibinadamu.
DAWASA, DAWASCO na Wizara ya Maji wasipojitokeza ndani ya siku tatu
mbele ya vyombo vya habari kutoa maelezo kwa umma nitachukua hatua za
kibunge nitakazoona zinafaa dhidi ya Waziri wa Maji Prof. Jumanne
Maghembe kwa kulidanganya Bunge kupitia kauli ya Serikali aliyotoa
Bungeni mwezi Mei 2014.
Ikumbukwe kwamba tarehe 12 Mei 2014 ikiwa ni sehemu ya kutimiza wajibu
wa mbunge wa kuwawakilisha wananchi nilieleza Bunge kwamba matatizo
katika mtambo wa Ruvu Juu yamekuwa yakijirudiarudia kwa nyakati
mbalimbali kwa kipindi cha takribani miezi mitatu kati ya Januari
mpaka Mei 2014 katika maeneo ambayo awali yalikuwa yakipata mgawo wa
maji.
Nilichukua hatua hiyo kwa niaba ya wananchi wanaohudumiwa na mtambo
huo katika kata za Kwembe, Kibamba, Mbezi Lois, Msigani, Kimara,
Saranga, Ubungo na Makuburi kwenye Jimbo la Ubungo; na kata
mbalimbali za majimbo ya Kibaha Mjini, Kibaha Vijijini, Segerea nk.
Kufuatia hatua hiyo, Mwezi Mei 2014 Waziri wa Maji Prof. Maghembe
alitoa kauli ya Serikali ya kueleza matatizo yanayoukabili mtambo wa
kuzalisha maji wa Ruvu Juu kwa ajili ya Jiji la Dar es salaam na
maeneo ya DAWASA katika mkoa wa Pwani.
Katika kauli yake Waziri Maghembe alikiri kwamba kwa takribani siku 67
(kati ya tarehe 01.03.2014 na tarehe 06.05.2014) mtambo ulizalisha
maji chini ya kiwango na kufikia kati ya lita milioni 8.2 na lita
milioni 57.4 ikilinganishwa na lita milioni 82 kwa siku, ambazo ndio
uwezo halisi wa mtambo huo.
Katika kauli yake bungeni, Waziri Maghembe aliorodhesha matatizo ya
mtambo wa Ruvu Juu kuwa ni: Kuharibika kwa pampu mara kwa mara
kunakosababishwa na uchakavu unaosababishwa na umri kua mkubwa miaka
(60), kukatika kwa Umeme mara kwa mara, maji kuwa na tope jingi sana
(turbidity) wakati wa mvua na mafuriko hali inayopunguza uwezo wa
pampu za kusukuma maji na husababisha kusagika kwa vifaa vya pampu na
ugumu wa upatikanaji wa vipuri halisi (genuine parts).
Hata hivyo, Waziri Maghembe hakukiri wala kukanusha juu ya madai ya
kuwepo kwa udhaifu, uzembe, ufisadi na hujuma katika mitambo ya vyanzo
vya maji na mitandao ya mabomba ya maji.
Waziri Maghembe alieleza Bunge kwamba Wizara imechukua hatua za
kutatua matatizo yaiyopo kwa kuchonga vipuri na vifaa vya pampu katika
karakana zilizopo hapa nchini kwa kuwatumia wataalamu wa jeshi,
kuagiza vipuri nje ya nchi na kutoa matangazo kwa wananchi kuhusu
upungufu wa maji pale uzalishaji unapopungua/kusimama.
Waziri Maghembe alilieleza bunge kwamba baada ya hatua hizo uzalishaji
wa Maji wa Mtambo wa Ruvu Juu unaendelea kurudi katika hali yake ya
kawaida na kutoa mfano wa kwamba tarehe 17 Mei, 2014 uzalishaji wa
maji ulikua lita milioni 80.3 kwa siku.
Aidha, Waziri Maghembe alitoa kauli Bungeni kwamba Wizara ya Maji
imeunda Kamati Maalum ambayo imeanza kufanya tathmini ya kina juu ya
chanzo cha matatizo ya mara kwa mara katika mtambo wa kusafisha maji
wa Ruvu Juu.
Waziri Maghembe alieleza kwamba kamati hiyo itafanya uchunguzi kubaini
kama matatizo hayo yanatokana na masuala ya kiufundi, kiuendeshaji au
makosa ya binadamu na kuahidi kwamba kamati itatoa taarifa yake katika
kipindi cha mwezi mmoja.
Mwezi mmoja umepita tangu nilipohoji bungeni tarehe 12 Mei 2014, hivyo
ni wakati muafaka kwa mamlaka zote zinazohusika kuweza kutoa mrejesho
juu ya uchunguzi huo na hatua nyingine za haraka za kuboresha
upatikanaji wa maji safi kama nilivyozieleza katika hoja binafsi
niliyoiwasilisha bungeni kwa niaba ya wananchi tarehe 4 Februari 2013.
Wenu katika uwakilishi wa wananchi,
John Mnyika (Mb)
22 Juni 2014
Serikali Yatajivunia Mafanikio ya Maboresho ya Bandari ya Dar es Salaam
Katika Siku 100 za Uongozi wa Rais Samia
-
Na Avila Kakingo, Michuzi Tv
MSEMAJI wa Serikali na Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na
Michezo, Gerson Msigwa, amesema Serikali ya Awam...
8 hours ago
0 Comments:
Post a Comment