UNYAMA HUU KWA WASICHANA WA KAZI ZA NYUMBANI MPAKA LINI?

'Hausigeli' ajeruhiwa na bosi wakeMFANYAKAZI wa ndani 'hausigeli',
Melina Mathayo (15), mkazi wa Boko, Dar es Salaam, amelazwa katika
Hospitali ya Mwananyamala kwa matibabu baada ya kupigwa na bosi wake
na kumsababishia majeraha sehemu mbalimbali za mwili wake ikiwemo
sehemu za siri.

Mtoto huyo ambaye ametokea Kijiji cha Nyaishozi, Wilaya ya Bukoba,
Kagera, alikuja jijini Dar es Salaam kufanya kazi za ndani kwa
mwanamke aliyefahamika kwa jina la Yasinta Rwechungura.

Akizungumza na waandishi wa habari hospitalini hapo juzi, alisema
tangu amefika, bosi wake huyo amekuwa na tabia ya kumpiga mara kwa
mara, kumchana sehemu za mgongoni kwa wembe na kumfinya sehemu zake
za siri kwa kucha, hali iliyomsababishia makovu mengi mwilini.

Alisema mwanzoni mwa wiki hii, bosi wake aliporudi kutoka kazini
alianza kumfokea na hatimaye kumpiga kwa waya kichwani na
kumsababishia jeraha ambalo lilimfanya kutokwa na damu nyingi.

"Amekuwa akinipiga muda mrefu na kunifanyisha kazi bila kunilipa
mshahara, ananiambia ananiwekea. Wakati alipokuwa ananipiga nilijaribu
kupiga kelele, lakini nilikosa msaada kutokana na nyumba yake kuwa
mbali na nyumba nyingine.

"Alikuwa akimaliza kunipiga ananiambia hata nikienda nyumbani
wakiniuliza haya makovu ya nini, niseme ni yeye alikuwa akinipiga
kwani hawana uwezo wa kumfanya chochote," alisema.

Alisema hospitalini hapo alipelekwa na mdogo wa bosi wake huyo baada
ya kumuonea huruma na kuona anazidiwa pamoja na ustawi wa jamii.

Daktari wa zamu ambaye hakutaka kutajwa jina, alisema mtoto huyo
aliletwa akiwa na hali mbaya na kusema sasa ana nafuu ingawa bado
wanaendelea kumfanyia vipimo zaidi.

Katika tukio jingine, mtoto Fatuma Hassani (10) mkazi wa Tandale,
amefikishwa hospitalini hapo baada ya mama yake mkubwa kumuunguza
mikono na miguu kwa banio la moto.

Mtoto huyo alisema mama yake huyo alimfanyia ukatili huo baada ya
kuchukua sh 500 kwenda kununua chakula.

Alisema siku hiyo mama yake huyo aliondoka nyumbani bila kuwaachia
chakula na kumpa sh 1,000 akachote maji yeye na mdogo wake, lakini
kutokana na kusikia njaa, aliamua kuchukua sh 500 na kwenda kununua
chakula.
source tanzania daima

0 Comments:

Post a Comment