UKAWA INAENDESHA KWA MICHANGO YA WABUNGE

UMOJA wa Katiba ya Wananchi, (UKAWA) umesema kuwa wanajiendesha kwa
fedha zao walizochangishana wenyewe ambapo kila mbunge ametoa sh 1
milioni  hivyo kuwataka wananchi kuwapuuza wale wanaoeneza propaganda
kuwa wanapewa fedha na wafadhili toka nje ya nchi.

Aidha wamesema kuwa maboresho ya daftari la wapiga kura ni lazima
yafanyike kabla ya kura ya katiba mpya kufanyika ili kuwawesha
wananchi wengi ambao kwa sasa hawajajiandikisha kuweza kushiriki zoezi
hilo.

Hayo yalisemwa juni 15, mwaka huu na mbunge wa Nyamagana, Ezekia Wenye, (CHADEMA),
wakati alipokuwa akiongea kwenye siku ya kumbukumbu ya mauaji ya watu
wanne na majeruhi zaidi ya 80 yaliyosababishwa na  bomu lililorushwa
kwenye mkutano wa kufunga kampeni za Chadema kwenye viwanja vya Soweto
jijini hapa.

Mbunge huyo alisema kuwa yeye ni mwenyekiti wa fedha wa Ukawa, jambo
alilodai kuwa wana fedha za kutosha kabisa kuendesha harakati za
kupigania kuheshimiwa kwa maoni ya wananchi kwenye rasimu ya katiba.

"Ukawa inaundwa na wabunge wa Chadema, CUF na  NCCR Mageuzi, pale
kwenye bunge la Muungano tuko zaidi ya 90 bado kule kwenye baraza la
Wawakilishi, sasa piga hesabu kila mmoja katoa shilingi milioni 1,
fikiria tuna fedha kiasi gani.

"Niwahakikishie kama Serikali haitakuwa tayari kufanya mazungumzo na
sisi kutuhakikishia rasimu itakayojadiliwa ndani ya bunge la katiba ni
ile ilioyoletwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba hatutarudi bunge na
tukirudi nadhani hata nyie mtatushangaaa sana, " alisema Wenje.
Aliwataka wananchi kuwapuuza wale wanaodai kuwa wapinzani wanapoenda
ikulu kujadili na Rais masuala muhimu yanayohusu maslahi ya umma
inapotokea yameshindikana bungeni kuwa wanafuata Juisi kwa madai kuwa
uwezo wao wa kufikiri ni mdogo kutokana na ukweli kuwa hakuna mbunge
anayekosa fedha ya kununua juisi hiyo.

Kwa upande wake Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema, (CHADEMA),
alisema kuwa anataarifa kuwa Chama Cha Mapinduzi, (CCM) kimewaagiza
wananchi kujiunga kwenye vikundi ili kiwapatie mikopo kwa utaratibu
nafuu hivyo akawataka wananchi hao wakaichukue na kuondoka kwa
utaratibu huohuo.

Akizungumzia tukio la mabomu la Juni 15, mwaka uliopita, Lema alidai
kuwa lilitekelezwa na polisi na ushahidi wanao na inazidi
kuthibitishwa na hatua ya Rais, Jakaya Kikwete kukataa kuunda tume
huru ya kimahakama walikoahidi kukabidhi ushahidi wa picha za mnato na
video.

"Kwa kipindi cha mwaka mzima sasa tunaimba iundwe, Tume huru ya
kimahakama lakini haiundwi, Rais na viongozi wa Serikali wako kimya
kama vile wale waliokufa na kujeruhiwa  pale Soweto si Watanzania,"
alisema lema.

Bomu hilo lilisababisha kifo cha Mwenyekiti wa BAWACHA< Kata ya Sokon
I, Judidh Moshi aliyefariki kwenye eneo la tukio na vifo vya watoto
wengine watatu huku watu wengine kadhaa wakijeruhiwa vibaya kwa risasi
za moto walizodai kuwa walipigwa na askari polisi.

Tukio hilo lilitokea  muda mfupi baada ya Mwenyekiti wa Taifa wa
Chadema, Freeman Mbowe aliyeambatana na viongozi wa mkoa na wilaya
akiwemo Lema kushuka jukwaani na kuanza kuchangisha fedha kwa ajili ya
kugharamia shughuli za uchaguzi wa marudio wa kata nne za Kaloleni,
Kimandolu, Themi na Elerai uliotarajiwa kufanyika siku inayofuata.

MWISHO

0 Comments:

Post a Comment