MBUNGE
wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe (CHADEMA), ameingizwa katika kashfa ya
kuwatumia wasanii na kujipatia zaidi ya sh milioni 100.
Tuhuma hizo nzito zilitolewa jana bungeni na Msemaji Mkuu wa Kambi
Rasmi ya Upinzani Bungeni, Joseph Mbilinyi alipokuwa akiwasilisha maoni
ya kambi hiyo kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya
Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo kwa mwaka 2014/2015.
Sugu alidai Zitto, alifanya ufisadi huo kwa kutumia kampuni yake ya
Leka Dutigite Limited yenye ubia na kampuni nyingine ya Advisors Ltd
ambazo zinadaiwa kuwa za Zitto.
Alisema Leka Dutigite, imesajiliwa kwa malengo ya kuendeleza wasanii
na sanaa, lakini imekuwa kichaka cha kuficha ufisadi wa wasanii.
Kwa mujibu wa Sugu, Kambi Rasmi ya Upinzani imebaini kuwa Desemba 10,
mwaka 2012, Hifadhi ya Taifa ya Saadani, ilihamisha sh milioni 1.2
kwenda kwenye akaunti na. 0150357447800 iliyoko Banki ya CRDB tawi la
Pugu Road, Dar es Salaam, inayomilikiwa na Leka Dutigite Ltd.
Hifadhi ya Taifa ya Saadani inamilikiwa na Mamlaka ya Hifadhi za Taifa (TANAPA), ambayo ni shirika la umma.
Sugu, alisema siku moja baadaye, fedha hizo zilitolewa taslimu kutoka kwenye akaunti hiyo.
Alisema baada ya hapo, kati ya Januari 14 na Februari 7 mwaka 2013, akaunti ya Leka Dutigite Ltd iliingiziwa sh milioni 28.6.
Fedha hizi zote ziliingizwa kama fedha taslimu na mtu aitwaye
Mchange. (sh milioni 3.6 Januari 14, 2013 na sh milioni 25, Januari 23
na Februari 7, 2013).
Kufikia Februari 7, 2013, fedha hizo zote zilikwishatolewa benki.
Sugu, alisema Februari 28 mwaka 2013, akaunti ya Leka Dutigite Ltd,
iliingiziwa sh milioni 32,367,000 na Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii
(NSSF).
Alisema kwa mujibu wa taarifa za kibenki, siku hiyo hiyo, fedha hizo zilitolewa kwenye akaunti hiyo.
Alisema siku nne baadaye, yaani Machi 4, 2013, NSSF ilifanya malipo
mengine kwenye akaunti ya Leka Dutigite Ltd kwa mikupuo miwili ya sh
milioni 46,663,000 na siku hiyo hiyo fedha hizo nazo zilitolewa kutoka
kwenye akaunti hiyo kwa mikupuo miwili.
“Kwa hiyo, katika kipindi cha miezi mitatu kati ya Desemba, 10, 2012
na Machi, 4, 2013, Leka Dutigite Ltd. ililipwa sh milioni 119,930,000
kwa utaratibu huo huo wa ingiza na toa fasta.
Kati ya fedha hizo, sh milioni 12. 2 zililipwa na TANAPA na sh milioni 79,027,000 zililipwa na NSSF,” alisema Sugu.
Msemaji huyo alisema katika mazingira ya kawaida, sio kitu cha ajabu
kwa mashirika ya umma kama NSSF na TANAPA kufanya biashara na watu au
taasisi mbali mbali kama kampuni binafsi.
Alisema wamenasa nakala ya mkataba unaohusu Maandalizi ya Filamu
(Documentary) kwa ajili ya kuhamasisha Shughuli za Utalii katika Hifadhi
ya Taifa ya Saadani kwa kutumia Wasanii kutoka Kigoma.
Mkataba huo umesainiwa Desemba 5 mwaka 2012, kati ya Hifadhi ya Taifa
ya Saadani na Leka Dutigite Ltd na una thamani ya sh milioni 12. 2
kiasi kile kile kilicholipwa na Hifadhi hiyo.
Kwa mujibu wa nyaraka za BRELA, ofisi za Gombe Advisors Ltd. ziko
kwenye jengo la City House, Mtaa wa Mkwepu, Dar es Salaam, ziliko ofisi
za Leka Dutigite Ltd.
Nyaraka zinaonyesha kuwa wakurugenzi wa Gombe Advisors Ltd. ni Zitto
Zuberi Kabwe, ambaye kazi yake inatajwa kuwa ‘mchumi’, na Raphael
Ongangi ambaye anatajwa kuwa ‘mchambuzi wa fedha na vitega uchumi’
Alibainisha kuwa Ongangi, aliwahi kutajwa na gazeti la kila wiki la
Mawio la Desemba 26, 2013 kuwa ni mmoja wa washauri wa Zitto Zuberi
Kabwe na anasemekana kuwa msaidizi wake.
“Kwa kadri ya ufahamu wa Kambi Rasmi ya Upinzani ya Bunge lako
tukufu, Mheshimiwa Zitto Kabwe hajawahi kutangaza maslahi aliyonayo
kwenye mikataba ya Gombe Advisors Ltd. na Leka Dutigite Ltd. na NSSF na
TANAPA.
Alisema Zitto alipaswa kutangaza maslahi yake kwani yeye sio tu
Mbunge anayebanwa na masharti ya Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma,
bali pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Fedha za Serikali
(PAC) ambayo mashirika yaliyotajwa yako chini yake.
source tanzania daima
source tanzania daima
0 Comments:
Post a Comment