NANYARO MSHUKIA DC MONGELA

DIWANI wa kata ya levelos, Ephata Nanyaro, CHADEMA), ameibua madai
mazito kuwa, kuna mfanyabiasha amejiua baada ya kibanda chake kuvunjwa
na mgambo wa jiji kuanza kugawana mali zake ikiwemo simu wakati wa
operesheni safisha jiji.

Aidha amehoji sababu za zoezi hilo kuendeshwa kwa upendeleo kwa kuonea
wanyonge huku akiuliza kigezo kilichotumika kuliacha kontena
linalotazamana na benki ya NBC,  barabara ya Sokoine wakati mengine
yakiondoshwa.

Pia amelaani kauli ya kibaguzi aliyodai kuwa ilitolewa na mkuu wa
wilaya ya Arusha, John Mongela, aliyowaeleza wafanyabiashara
ndogondogo kuwa kama hawawezi kufuata taratibu za jiji, basi warudi
kwao walipotoka Moshi na Babati.


Aliyasema hayo mwishoni mwa wiki wakati akichangia kwenye kikao cha
kawaida cha baraza la madiwani ambapo kulitokea kutofautiana kimsimamo
kati ya madiwani wa Chadema, ambao wanataka zoezi hilo liboreshwe ili
lisikiuke haki za binadamu huku wale wa CCM wakiona kuwa zoezi hilo
linaenda sawa.

Nanyaro alisema kuwa kwenye kata yake kuna wafanyabiashara wanaofanya
shughuli zao kwenye eneo lisilokubalika kisheria lakini hawajaguswa na
zoezi la safisha jiji kwa kuwa eneo hilo Umoja wa Wanawake wa CCM,
(UWT), wanakusanya ushuru jambo aliloonya kuwa si sahihi.

"Sote tunataka jiji liwe safi lakini si kwa gharama za maisha ya watu,
kuna mfanyabiashara mmoja alijiua pale kwenye kata yangu baada ya
kibanda chake kung'olewa na mgambo wa Jiji , kisha  wakaanza kugawana
simu zake, kuna watu watatu wamevunjwa miguu wakati zoezi hili
likiendelea nammoja yuko hapo nje.

"Mgambo wanapiga sana wananchi wakati wakitekeleza zoezi hili, na mimi
ni mmoja wa waliopigwa wakati nikifuatilia kadhia wanayopata wananchi,
cha kushangaza hakuna hatua zozote zilizochukuliwa dhidi ya mgambo
hawa mpaka sasa wanaendelea na kazi kama kawaida licha ya malalamiko
mengi ya wananchi," alisema diwani huyo wa levelos.

Nanyaro alitaka baraza hilo kwa kauli moja lilaani kauli ya DC,
Mongela ya kuwataka wamachinga kurudi kwenye miji yao ya asili kama
hawako kuondoka kutii utaratibu kwa kile alichoeleza kuwa si ya
kiungwana, inachochea chuki miongoni mwa jamii.

Naye Diwani wa kata ya Sekei, Crispin Tarimo, alihoji sababu za CCM
kutumia magari ya halmsahauri kwenda kukagua miradi ya maendeleo
ambayo inatekelezwa na halmashauri jambo alilodai kuwa ni matumizi
mabaya ya fedha za umma.

Pia alitaka baraza hilo kuangalia utaratibu mzuri utakaowawezesha
wafanyabiashara ndogondogo wakiwemo mafundi chrehani, maudindi saa na
wachoma mahindi kufanya shughuli zao badala ya kuwaondoa huku kukiwa
hakuna utaratibu mahsusi juu yao kwa kile alichoonya kuwa biashara
hizo zinawaingizia kipato cha kuebndesha maisha yao na familia zao.

Kwa upande wake diwani wa kata ya kati, Abdulrasul Tojo, (CCM),
alipongeza zoezi hilo la safisha jiji alilodai kuwa limeleta heshima
kwa halmashauri hiyo huku akitaka busara itumike kwa mafundi cherehani
aliodai kuwa hawapo barabarani bali huendeshea shughuli zao
vibarazani.

Alisema kuwa hata wanawake wanaochoma mahindi nyakati za jioni nao
waangaliwe kwani haiwezekani kuwapeleka eneo moja kutokana na namna
biashara hiyo inavyofanyika.

Akijibu hoja hizo, Mkurugenzi wa jiji la Arusha, Juma Iddi, alisema
kuwa hakuna sheria inayowaruhusu mgambo kupiga watu lakini inapotokea
wakichokozwa wakati wakitekeleza wajibu wao nao huamua kujibu mapigoa
ambapo ukishapigwa hata ukichukua hatua za sheria ukweli unabaki
palepale kuwa umepigwa.

"Kuna raia wamepigwa na kuna mgambo wamepigwa na wameumizwa huo ndiyo
ukweli, yote haya ni makosa ya jinai inapaswa kutolewa taarifa polisi
ili sheria iweze kufuata mkondo wake, hakuna suala la kushughulikiwa
kiutawala hasa linapohusisha jinai," alisema Iddi.

Hata hivyo alisema kuwa wanatarajia kuongea na Chuo Cha Polisi Moshi,
(CCP), ili waweze kuwapatia mafunzo mgambo wa jiji ambapo katika mwaka
ujao wa fedha wanatazamia kuajiri askari wasaidizi 36 waliohitimu CCm
jambo alilodai kuwa litasaidia kupunguza masuala ya uonevu kwa
wananchi.

"Tumeshaondoa mafundi cherahani na wauza mahindi, naomba hayo maeneo
yabaki wazi, hapa mjadala wetu uwe tunafanya nini hawa wamachinga
wafanye biashara bila kuchafua mazingira, tuepueshe baraza hili
kujadili kuvunja sheria ," alisema Mkurugenzi huyo.

Kuhusu ziara ya CCM kukagua miradi ya maendeleo, Iddi alisema kuwa
ilikuwa ni utekelezaji wa maelekezo ya Serikali iliyotaka Vionngozi wa
CCM kupita kukagua utekelezaji wa ilani yao ambapo wao walitoa
wataalam na gari kwa ajili ya kwenda kutoa ufafanuzi juu ya miradi
hiyo.

Kwa upande wake Meya wa JIji, Gaudence Lyimo, (CCM) alisema kusema
kuwa kuruhusu biashara ya kuuza mahindi vibarazani ni hatari kwani
watu wengine ambao wanamawazo wanaweza wasione vizuri hivyo kuungua.

0 Comments:

Post a Comment