DIWANI wa Kata ya levelos, Ephata nanyaro, (CHADEMA), amelitaka Jeshi la polisi mkoani Arusha kuacha kufanya kazi kwa mashinikizo ya kisiasa kwani inaweza kuhatarisha amani na usalama pindi wananchi wakiona hakuna haki.
Amedai kuwa siku chache baada ya kutoa kauli kwenye baraza la madiwani akilaani kauli ya kibaguzi ya Mkuu wa Wilaya, John Mongela aliyedaiwa kuwaeleza machinga wasiotaka kutii kanuni za jiji warudi kwenye maeneo waliyotoka Moshi na Babati, jeshi la polisi limemtengenezea kesi ya jinai ya kumpiga mgambo wa jiji.
Nanyaro aliyasema hayo jana akiongea na waandishi wa habari jijini hapa ambapo alisema kuwa alipigiwa simu juzi (jumatatu) asubuhi na askari wa upelelezi aliyejitambulisha kwake kama, Evarest akimtaka afike polisi ili apelekwe mahakamani yeye pamoja na Naibu Meya, Prosper Msofe, (CHADEMA) ambapo wanatarajia kufika polisi leo (jumatano) asubuhi.
Alisema kuwa kesi hiyo ni ya kubambikizwa kwani April, 16 mwaka huu majira ya asubuhi yeye na Naibu Meya, Msofe, walipigwa na mgambo kwenye ghala la Halmashauri hiyo lililopo Levelos baada ya wao kufuatilia malalamiko ya wananchi kuwa huwa wanafungiwa huko na kupigwa na mkia wa faru ambapo mpaka sasa wananchi watatu wamevinjwa miguu.
"Tulienda kupatiwa huduma ya kwanza kwenye kituo cha afya, Ngarenaro, tukiwa pale alifika DC, Mongela, hakutusemesha bali alienda moja kwa moja upande alipokuwa mgambo mmoja aliyejifanya amepigwa lakini hakuwa na jeraha la aina yoyote kisha akatoka kwenda kuongea na wananchi waliokuwa wamekusanyika nje," alisema Nanyaro.
Tulipotoka pale tulienda kituo cha kati cha polisi kuchukua fomu namba tatu ili tukapatiwe matibabu zaidi kwenye hospitali ya mkoa ya Mount Meru lakini tulinyimwa kwa maelekezo ya Mkuu wa Polisi wa Wilaya, (OCD), Giles Muroto aliyedai kuwa atawapa akishapata maelekezo ambapo walifuatilia mpaka saa moja usiku bila mafanikio hivyo wakaenda kutibiwa hivyohivyo .
"Ndiyo maana nawaambia Jeshi la polisi linafanya kazi kwa mashinikizo, kuna taarifa kuwa kuna kikao kischo rasmi kilichoendeshwa na Mkuu wa wilaya akishirikiana na watu wa usalama waliopanga kutushtaki ili kulipa kisasi kwa misimamo tuliyoitoa kwenye kikao cha baraza lakini sisi tunaamini mahakamani haki itatendeka.
"kama wangekuwa wanatumia weledi wangetuambia yule dada aliyejaribu kumpiga risasi polisi akilinda benki ya CRDB amechukuliwa hatua gani za kisheria manake taarifa zilizopo ni kuwa hakufunguliwa hata jalada polisi.
"Yule hakuchukuliwa hatua kwa kuwa anamahusianao na (Mkuu wa mkoa, Magesa Mulongo) tena nina wasiwasi kama Yule askari aliyenusurika kupigwa risasi kama atakuwa bado yuko kazini mtakumbuka siku ile yule mwanamke akiingizwa pale hospitali ya Selian DC , Mongela alikuwa akizuia waandishi msipate picha," alisema nanyaro.
Hata hivyo juhudi za kumpata mkuu wa wilaya , Mongela na kamanda wa polisi mkoani hapa, Liberatus Sabas kujibu madai hayo hazikuzaa matunda baada ya simu zao kuita muda wote bila kupokelewa hata walipotumiwa ujumbe mfupi wa simu hawakujibu.
0 Comments:
Post a Comment