Shinikizo la damu na magonjwa ya moyo yameendelea kuwa tishio kubwa kwa afya ya wananchi, baada ya kubainika kuwa kati ya wananchi takribani 3,000 waliojitokeza katika kambi ya uchunguzi wa afya ya moyo na magonjwa yasiyoambukiza kwa mikoa ya Kanda ya Kaskazini, asilimia 25 waligundulika kuwa na shinikizo la damu huku asilimia 9 wakibainika kuwa na matatizo ya moyo.
Taarifa hiyo imetolewa na Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI), Dkt. Peter Kisenge, leo Jumanne Januari 06, 2025, wakati wa ziara ya Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Amos Makalla, aliyefika kukagua zoezi hilo la uchunguzi na matibabu bure katika Hospitali ya Arusha Lutheran Medical Centre (Seliani).
Dkt. Kisenge amesema changamoto ya shinikizo la damu imeonekana kuwaathiri zaidi wananchi wenye umri wa kuanzia miaka 45 hadi 80, hali inayochangiwa kwa kiasi kikubwa na mtindo mbaya wa maisha ikiwemo kutofanya mazoezi ya mwili, unene uliokithiri, ulaji usiozingatia lishe bora, unywaji wa pombe kupita kiasi na uvutaji wa sigara.
Ameeleza kuwa ulaji mkubwa wa vyakula vya wanga hususan nyakati za jioni bila kufanya mazoezi husababisha nishati hiyo kubadilika kuwa mafuta mwilini na kuongeza hatari ya kupata magonjwa yasiyoambukiza, ikiwemo shinikizo la damu na magonjwa ya moyo.
Akizungumzia mustakabali wa huduma za moyo mkoani Arusha, Dkt. Kisenge amesema ujenzi wa Kituo cha JKCI katika Hospitali ya Seliani utaimarisha upatikanaji wa huduma za kibingwa kwa wananchi wa Arusha na mikoa ya jirani, pamoja na kuwahudumia watalii na washiriki wa Michuano ya Mataifa ya Afrika (AFCON) itakayofanyika mkoani Arusha mwaka 2027.
“Nichukue fursa hii kuwahimiza wananchi kupima afya zao mara kwa mara, hasa afya ya moyo. Ndiyo maana JKCI imeamua kutembea mikoa mbalimbali nchini kutoa huduma za uchunguzi wa moyo bure,” amesema Dkt. Kisenge.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Arusha, AmosMakalla, ameishukuru JKCI kwa kufungua kituo cha huduma za moyo mkoani Arusha, akisema hatua hiyo itapunguza rufaa kwenda Dar es Salaam na kuwasaidia wananchi kupata matibabu kwa wakati.
Makalla amesema wananchi wasiokuwa na uwezo na watakaopata rufaa ya matibabu zaidi watawezeshwa na Serikali ili kupata huduma za kibingwa katika Taasisi ya Moyo JKCI Dar es Salaam, huku akihamasisha wananchi kujiunga na mifumo ya bima ya afya kwa wote.
Wananchi wa Mkoa wa Arusha na mikoa ya jirani wameishukuru Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwezesha programu ya vipimo na matibabu bure ya magonjwa ya moyo, wakisema imekuwa msaada mkubwa kwa wananchi wenye kipato cha chini na wale waliokuwa hawajawahi kupima afya ya moyo hapo awali.

















































