Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Tundu Lissu, leo, Jumamosi, Aprili 5, 2024, ametengua uteuzi wa aliyekuwa Mjumbe wa Sekretarieti ya Kamati Kuu ya chama hicho na Mtaalamu wa dawati la jinsia, Catherine Ruge.
Uamuzi huu wa kiongozi huyo umeleta hisia mseto miongoni mwa wanachama na wafuasi wa chama hicho, huku baadhi wakimpongeza Lissu, wengine wakikosoa vikali hatua hiyo, wakisema inakiuka kanuni za chama.
Taarifa hiyo imetolewa na Mkurugenzi wa Mawasiliano na Uenezi wa CHADEMA, Brenda Rupia, kupitia chapisho lake kwenye mtandao wa kijamii wa X (Twitter), lakini haijafafanua wazi sababu za kutenguliwa kwa uteuzi wa Ruge.
Pamoja na kutokuwepo kwa sababu rasmi, baadhi ya vyanzo vya ndani vimeeleza kuwa uamuzi huu umetokana na msimamo wa Ruge kutokuwa na uungaji mkono wa moja kwa moja kwa kampeni ya ‘No Reform, No Election’. Hii ni baada ya kubainika kuwa Catherine Ruge, ambaye pia amewahi kuwa Katibu Mkuu wa Baraza la Wanawake la CHADEMA (BAWACHA), alikuwa miongoni mwa makada wa chama hicho wanaopinga kampeni hii.
Makada hao, waliotangaza kujitenga na msimamo wa chama, wakiwemo wanachama wanaojiita 'G-55', walituma waraka kwa Katibu Mkuu wa CHADEMA, John Mnyika, wakipendekeza chama hicho kuepuka kujitosa kwenye kampeni hiyo.
Badala yake, walishauri chama kiendelee kushiriki uchaguzi huku kikisisitiza mabadiliko. Walipendekeza kwamba CHADEMA isiache kushiriki uchaguzi lakini iendelee kupigania mabadiliko kupitia michakato ya kidemokrasia.
Lissu na viongozi wengine waandamizi wa chama hicho, akiwemo Makamu Mwenyekiti Tanzania Bara, John Heche, wanaendelea kusimamia oparesheni ya ‘No Reform, No Election’ kwa nguvu katika mikoa ya Kusini, ikiwemo Lindi, Mtwara, na Ruvuma.
Katika muktadha huu, uamuzi wa Lissu kumvua uteuzi Ruge umepelekea baadhi ya wanachama na wafuasi wa CHADEMA kuonekana kutofurahi, huku baadhi wakikosoa hatua hiyo kwa kusema kuwa inapingana na katiba ya chama, hususan sehemu inayohusu taratibu za kuchukua hatua dhidi ya viongozi wa chama.
Mrema alikumbusha kanuni za chama zilizowekwa katika katiba kuhusu hatua za kinidhamu dhidi ya viongozi, akisisitiza kwamba kila kiongozi anapaswa kupewa nafasi ya kujieleza kabla ya kuchukuliwa hatua za kinidhamu.
Kanuni hizi zinaonyesha kuwa taratibu za kinidhamu zinapaswa kufuatwa kwa umakini ili kuhakikisha haki za viongozi zinaheshimiwa.
Kwa sasa, hali ndani ya CHADEMA inaendelea kuwa tete huku wanachama wakitafakari uamuzi huu na matarajio yao ya kisiasa kwa chama hicho kuelekea uchaguzi mkuu.
0 Comments:
Post a Comment