Marehemu Mwalimu Martin Mpemba, aliyekuwa Diwani wa Kata ya Kiziguzigu, Wilaya ya Kakonko, Mkoa wa Kigoma, amefariki dunia usiku wa April 3, 2025, baada ya kushambuliwa na mtu asiyejulikana. Tukio hili lilitokea katika Kijiji cha Kibingo, Kata ya Kiziguzigu, ambapo Marehemu Mpemba alikumbwa na kifo cha kikatili baada ya kupigwa na kitu chenye ncha kali kichwani.
Katibu wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Kigoma, Christopher Palangyo, alipokuwa akizungumza na viongozi wa chama na waombolezaji mjini Kakonko, alisema:
"CCM imesikitishwa na tukio la kifo cha Diwani Mpemba ambaye ameuawa baada ya kupigwa na kitu chenye ncha kali kichwani wakati akitokea sokoni kurudi nyumbani kwake jana jioni."
Palangyo alisisitiza umuhimu wa kuhakikisha wahusika wa mauaji haya wanakamatwa haraka na hatua stahiki za kisheria zichukuliwe, akiongeza:
"Jeshi la polisi linapaswa kuhakikisha wauaji wanapatikana haraka na kuchukuliwa hatua za kisheria. Mauaji ya namna hii hayakubaliki katika jamii iliyostaarabika."
Aidha, Palangyo alisisitiza kwamba uchunguzi wa haraka unahitajika ili kuondoa mashaka na wasiwasi miongoni mwa wananchi kufuatia tukio hili la kusikitisha, akisema:
"Uchunguzi wa haraka ufanywe ili kuondoa mashaka na wasiwasi ambao umewakumba wananchi baada ya tukio hili."
Katika kutoa salamu za pole, Palangyo alikabidhi ujumbe wa rambirambi kutoka kwa Mwenyekiti wa CCM Taifa na Rais Samia Suluhu Hassan pamoja na Katibu Mkuu wa CCM Taifa, Dkt. Emmanuel Nchimbi, na kusema:
"Chama kinaungana familia, wana-CCM na wananchi wote katika msiba huu."
Msiba huu umeligubika jimbo la Kakonko na kuacha simanzi kubwa miongoni mwa wananchi na wafuasi wa CCM, huku hatua za kisheria zikisubiri kuchukuliwa ili kuhakikisha haki inatendeka.
0 Comments:
Post a Comment