WANANCHI MWIKA KUSINI SASA WAJA KIVINGINE BAADA YA KUFANIKIWA UKARABATI WA BARABARA SASA WAZIGEUKIA SHULE KONGWE

 


Na Mwandishi Wetu, Moshi


Katika kuhakikisha kuwa shule  kongwe katika kata ya Mwika Kusini iliyopo wilaya ya Moshi mkoani Kilimanjaro zinarudi katika ubora wake wananchi kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo wameanza kuzikàrabati shule hizo kwa nguvu zao wenyewe kama walivyofanya kwenye mradi wa barabara.


Wananchi hao waliweza kukarabari barabara zenye urefu wa  takribani kilomita 64 hususan katika kijiji cha  Kiruweni ambapo fedha zaidi ya milioni 600 zilitumika kwa kuchimba barabara hizo sambamba na uwekaji wa moramu na ujengaji wa  kingo za maji.


Baada ya kufanikiwa kwa kiwango kikubwa wananchi hao kwa sasa wamejikita katika kuongeza nguvu kwa kukarabati shule kongwe ili ziweze kuwa na mazingira rafiki katika utoaji wa elimu sambamba na kuwa na muonekano wa kisasa.


Tayari zoezi hilo limeanza katika shule ya msingi Karoro ambapo ujenzi wa choo cha walimu unaendelea ili kuondoa adha iliyokuwa ikiwakumba walimu wapatao 6 kujisaidia choo kimoja na wanafunzi



Pia ukarabati wa ofisi ya walimu uwekaji wa sakafu katika baadhi ya vyumba vya madarasa shule ya msingi Mawanda unaendelea na umefikia hatua nzuri ila bado haujakamilika


Hata hivyo bweni la wasichana katika shule ya sekondari Mangi Marialle unaendelea ambapo sasa pindi litakapokamilika huenda kiwango cha ufaulu kwa wasichana kikaongezeka.



John Tarimo ni diwani wa kata ya Mwika Kusini ambapo amesema wananchi hao kwa sasa wamejikita katika kuchangamkia maendeleo na kuwa bado miradi hiyo hajakamilika na michango bado inahitajika ili mambo mengine yafuate


'Hawa ni wananchi wenye maono waliona ni vyema kufanya kile wanachokiona kinafaa kwa muda huo na sio kusubiri serikali ifanye kila jambo kwani mengine yapo ndani ya uwezo wetu'anasema


Anasema kuwa wananchi hao wameamini kuwa maendeleo yataletwa na wao wenyewe na ndio maana wamekuwa mstari wa mbele katika kuhakikisha wanafikia kile wanachokiamini badala ya kuishi kwa kusubiria kila kitu waletewe.


Kaanael Malle mkazi wa Mawanda anasema maono ya wadau hao wa maendeleo kutaenda kuifufua shule yao na iweze kuwa na mazingira rafiki ya utoaji wa elimu tofauti na ilivyokuwa hapo awali  mithili ya ghofu.



0 Comments:

Post a Comment