LHRC Waibua Hoja Nzito Kuhusu Mustakabali wa Uhuru wa Habari Tanzania



Katika kuadhimisha Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari Duniani, wadau wa sekta ya habari nchini wameeleza wasiwasi mkubwa juu ya hali ya uhuru wa vyombo vya habari, wakionya kuwa mwenendo wa kudorora unaendelea kushuhudiwa na unaweza kuathiri mustakabali wa demokrasia na haki ya kupata taarifa.



Akizungumza jijini Arusha Aprili 29, 2026, Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu, Anna Henga, alisema kuwa tathmini ya hali ya haki za binadamu nchini inaonesha kuwa sekta ya habari ni miongoni mwa zilizoathirika zaidi, hasa katika kipindi cha uchaguzi kilichopita.


Alifafanua kuwa katika kipindi hicho, wanahabari kadhaa walikamatwa kinyume cha taratibu, wengine kushikiliwa bila kufikishwa mahakamani, huku baadhi wakiripotiwa kupotea katika mazingira ya kutatanisha na wengine kuuawa. Matukio hayo yameripotiwa katika maeneo mbalimbali ikiwemo Musoma, Dar es Salaam na Arusha.



“Matukio haya yanaashiria kuwepo kwa mazingira magumu kwa uhuru wa vyombo vya habari na usalama wa wanahabari nchini,” alisema Dkt. Henga.


Aidha, alieleza kuwa kufungwa kwa huduma za intaneti, hasa wakati wa uchaguzi, kumeendelea kuwa kikwazo kikubwa kwa vyombo vya habari vya mtandaoni. Alibainisha kuwa hatua hiyo inadhoofisha upatikanaji wa taarifa kwa wananchi na kuathiri uwazi.



“Unapofunga intaneti, unazuia kabisa uwezo wa vyombo vya habari kutekeleza majukumu yake katika zama za kidijitali,” alisisitiza.


Katika hatua nyingine, Dkt. Henga aligusia changamoto ya kufungiwa kwa baadhi ya vyombo vya habari kwa nyakati tofauti, hali inayodhoofisha ukuaji wa tasnia hiyo. Aliongeza kuwa hata katika robo ya kwanza ya mwaka 2026, matukio ya kukamatwa kwa wanahabari na kufungiwa kwa vyombo vya habari yameendelea kuripotiwa.



Akizungumzia suala la ubunifu, alisema kuwa hauwezi kustawi katika mazingira yenye hofu na vikwazo. Alifafanua kuwa wanahabari wanapofanya kazi katika mazingira yasiyo na uhuru, hulazimika kujikita katika maudhui ya kawaida badala ya yale yenye kuchochea mabadiliko chanya katika jamii.


“Mwanahabari hawezi kuwa mbunifu ikiwa hana uhuru wa kufanya kazi yake kwa uhuru na usalama,” alieleza.


Kuhusu mfumo wa kisheria, Dkt. Henga alieleza kuwa licha ya Katiba ya Tanzania Ibara ya 18 kulinda uhuru wa kutoa na kusambaza taarifa, bado kuna mapungufu katika baadhi ya sheria za habari na maudhui ambazo zinatajwa kukandamiza uhuru huo.


Alisisitiza umuhimu wa kufuata misingi ya haki (due process), akibainisha kuwa wanahabari na vyombo vya habari vinapaswa kupewa fursa ya kusikilizwa kabla ya kuchukuliwa hatua zozote za kisheria au kiutawala.


Aidha, alizungumzia mahusiano kati ya serikali na vyombo vya habari, akieleza kuwa bado yana mvutano, huku vyombo vya habari vikionekana kama wakosoaji badala ya washirika muhimu katika kukuza uwazi na uwajibikaji.


Katika mjadala uliofanyika sambamba na maadhimisho hayo, wadau mbalimbali walijadili mustakabali wa tasnia ya habari nchini, wakisisitiza umuhimu wa kuimarisha uadilifu wa habari katika enzi ya kidijitali na kupambana na changamoto ya taarifa potofu.


Maadhimisho ya mwaka huu, ambayo ni ya 33 nchini Tanzania, yamewakutanisha wanahabari, wahariri, wanazuoni, wanaharakati wa haki za binadamu pamoja na wawakilishi wa serikali, yakilenga kujadili nafasi ya vyombo vya habari katika kukuza demokrasia, uwazi na maendeleo endelevu.


Kwa ujumla, wadau wametoa wito kwa serikali kuchukua hatua madhubuti za kuboresha mazingira ya kisheria na kiutendaji ili kulinda uhuru wa vyombo vya habari. Wamesisitiza kuwa bila hatua hizo, hali inaweza kuendelea kudorora na kuathiri haki ya wananchi kupata taarifa sahihi kwa wakati pamoja na maendeleo ya kidemokrasia nchini.


0 Comments:

Post a Comment