Prof. Kabudi: “Tawasifu ya Balozi Njoolay Ni Hazina Itakayodumu kwa Vizazi Vijayo”




Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Profesa Palamagamba Kabudi, asema tawasifu ya Balozi Daniel Ole Njoolay ni hazina ya kipekee itakayodumu kwa vizazi vijavyo—hasa ikizingatiwa kwamba safari yake ya elimu, utumishi na uongozi imejaa miujiza, majaribu makubwa na ushindi uliopatikana kwa juhudi na uhodari.





Ameyasema hayo katika hafla ya uzinduzi wa kitabu cha Balozi Njoolay kilichofanyika Novemba 29, 2025 katika ukumbi wa Corridor Spring Hotel jijini Arusha kuhudhuriwa na viongozi wa serikali, akiwemo Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushurukiano wa Afrika Mashariki, James Millya, mabalozi na viongozi wastaafu.



  Prof. Kabudi alisema maisha ya Balozi Njoolay—hasa safari yake ya elimu na uongozi—yamejaa miujiza, vikwazo, ujasiri na maamuzi magumu yaliyojenga msingi wa mafanikio yake.


Katika hotuba hiyo yenye msisitizo mkubwa wa thamani ya kumbukumbu na usomaji wa vitabu, Prof. Kabudi alimshukuru Mungu kwa kuwezesha tukio hilo muhimu, huku akipongeza uthubutu wa Balozi Njoolay kuandika kitabu kinachoeleza simulizi ya maisha yake kuanzia utotoni hadi safari yake katika utumishi wa umma na diplomasia.



Alisema kitabu hicho ni zawadi muhimu kwa taifa, akibainisha kuwa ni wachache mno wenye moyo wa kuandika na kurithisha maarifa yao. Alikumbusha pia mazingira magumu aliyoyapitia Balozi Njoolay wakati jamii ya Maasai ilipokuwa ikiona elimu si jambo la lazima, hadi pale serikali ilipolazimisha watoto kwenda shule.



Prof. Kabudi aliwataka vijana na Watanzania kwa ujumla kusoma kitabu hicho ili kuishi na kujifunza kupitia uzoefu huo wa kipekee. Alihusisha umuhimu huo na desturi yake binafsi ya kusoma hotuba za Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, akisema kuwa tawasifu na hotuba hizo bado zinatoa mwanga mkubwa katika zama za leo.


Akinukuu hotuba ya Nyerere ya mwaka 1965 iliyowasisitiza vijana kujenga na kulinda taifa, Prof. Kabudi alieleza kuwa taifa linaweza kudidimia kama vijana hawajengi misingi thabiti ya uzalendo, maadili na dhamira ya kulihudumia.


Katika kuhimiza usomaji wa vitabu, Prof. Kabudi aliainisha manufaa kadhaa ikiwemo kupanua maarifa, kuchochea ubunifu, kuimarisha maadili na kuongeza uwezo wa kujenga hoja na kufanya maamuzi sahihi. Aliitaka jamii, hasa familia, kuwahamasisha watoto na vijana kusoma vitabu kama sehemu ya malezi na ujenzi wa fikra.


Kwa waandishi wa vitabu, aliwasihi kuendelea kuandika bila kukata tamaa licha ya changamoto ya wananchi wengi kutopenda kusoma. Aliwatia moyo kwamba kila kitabu ni chombo cha maarifa kitakachowanufaisha wengi katika siku za usoni.


Prof. Kabudi alimpongeza Balozi Njoolay kwa uzalendo na utumishi wake uliotukuka, akisema amekuwa mfano bora wa kuigwa na viongozi pamoja na vijana nchini. Pia alishauri kitabu hicho kisambazwe kwa njia za kidijitali ili kuwafikia wasomaji wengi zaidi ndani na nje ya Tanzania.


Baada ya hotuba hiyo, Waziri Kabudi alizindua rasmi kitabu cha Balozi Daniel Ole Njoolay, akiitimisha shughuli hiyo kwa wito wa kuenzi na kuishi hekima iliyomo katika kurasa zake.


0 Comments:

Post a Comment