Arusha, Tanzania — Uzinduzi wa kitabu Tawasifu ya Balozi Daniel Ole Njoolay umefanyika jijini Arusha na kuhudhuriwa na viongozi wa Serikali, wabunge, wanadiplomasia, wasomi, viongozi wa dini, pamoja na wananchi kutoka maeneo mbalimbali.
Katika hafla hiyo, Salim Salim, kwa niaba ya kamati ya maandalizi, aliwasilisha muhtasari wa yaliyomo ndani ya kitabu hicho na kusisitiza kuwa ni miongoni mwa kazi bora zaidi za kihistoria na kiwasifu kuwahi kuandikwa na mtumishi wa umma nchini Tanzania.
Akiwasilisha muhtasari huo, Salim alisema kwamba mara tu alipokianza kitabu hicho, hakutaka kukiweka chini kwa sababu simulizi za Balozi Njoolay zinamvuta msomaji kutoka ukurasa mmoja hadi mwingine.
“Balozi anafanana na wazee wetu wa zamani ambao walikuwa mabingwa wa kutoa hadithi. Daniel is a master storyteller,” alisema.
Sifa za viongozi wakuu wa Taifa
Katika muhtasari wake, Salim alinukuu maneno ya viongozi wakuu wa nchi yaliyomo kwenye kitabu hicho, ikiwemo Dibaji iliyoandikwa na Waziri Mkuu Mstaafu Mhe. Joseph Sinde Warioba, ambaye alimwelezea Balozi Njoolay kama kiongozi wa mfano wa kuigwa.
Katika maneno yake yaliyohifadhiwa mwishoni mwa kitabu, Mhe. Warioba anasema:
“Sifa zake ni mfano wa kuigwa. Amefanya kazi ndani ya umma kwa bidii, ubunifu, uadilifu na uaminifu… nimekisoma kitabu hiki kwa msisimko. Kina mengi ya kujifunza, hasa kwa vijana wanaoanza maisha ya utumishi na uongozi.”
Salim pia alinukuu maneno ya Rais Mstaafu Benjamin William Mkapa (apumzike pema peponi), aliyewahi kumwambia Balozi:
“Mkuu, ninachokupendea huwa unasema ukweli hata kama ule ukweli unaniumiza.”
Zaidi ya tawasifu ya kawaida
Salim alifafanua kuwa kitabu hicho hakisimulii tu historia ya maisha ya Balozi Njoolay, bali kinafundisha maadili, unyenyekevu, uongozi na misingi ya utu wa mtu. Alisema maneno tawasifu au wasifu hayatoshi kueleza uzito wa yaliyomo ndani ya kitabu hicho.
“Kitabu hiki ni ushuhuda hai (a living testimony) wa jinsi Daniel alivyojibu kwa ukarimu wito wa kutumikia na kushirikiana na Muumba. Kina kusukuma kufikiri, kujiangalia, na kutathmini ubora na udhaifu wa maisha yako,” alisisitiza.
Alikilinganisha kitabu hicho na kazi kubwa za viongozi maarufu duniani kama Nelson Mandela (Long Walk to Freedom), Barack Obama (Dreams from My Father), na Mahatma Gandhi (All Men Are Brothers), akisisitiza kuwa kitabu cha Ole Njoolay nacho kina nafasi ya kutafsiriwa kwa Kiingereza siku zijazo.
Hazina kwa Taifa
Mwisho wa hotuba yake, Salim Salim alisema wazi kuwa Balozi Daniel Ole Njoolay ni hazina muhimu kwa Taifa la Tanzania, na kwamba bado kuna haja kubwa ya kuendelea kumtumia katika majukumu ya kitaifa.
Akihitimisha, alinukuu maneno ya Mchungaji Martin Luther King Jr.:
“Swali kuu la kujiuliza maishani ni hili: Unawafanyia nini watu wengine?”
“Mhe. Daniel anaelewa uzito wa swali hili, na amelifanyia kazi kwa kiwango cha juu sana. Lakini haya yote hayatoshi kusimuliwa—ni lazima usome kitabu mwenyewe,” aliongeza.
Uzinduzi huo mgeni rasmi alikuwa Waziri wa Habari Prof. Palamagamba Kabudi ambapo viongozi mbalimbali walihudhuria akiwemo Naibu Waziri wa Mambo ya Nje, James Millya, Mbunge wa Arumeru Magharibi, Dr Lukunay, viongozi wa Chama Cha Mapinduzi, ( CCM) , viongozi wa umma wastaafu na watu mashuhuri.





0 Comments:
Post a Comment