Mbunge wa Bunge la Afrika Mashariki (EALA) kutoka Tanzania, Dr. Abdulla Hasnuu Makame, amemuelezea Waziri Mkuu Mstaafu wa Kenya, Raila Amolo Odinga, kama kiongozi wa kipekee, mwana demokrasia wa kweli, na rafiki wa karibu wa Watanzania, aliyekuwa na mchango mkubwa katika kudumisha umoja wa Afrika Mashariki.
Akizungumza Oktoba 16, 2025, katika kikao maalum cha Bunge la Afrika Mashariki kilichofanyika jijini Arusha, Makame alizungumza kwa hisia kali wakati akichangia hoja ya kuomboleza kifo cha Raila, iliyowasilishwa na Mbunge wa Kenya, Suleiman Shahbal, na kuungwa mkono na wabunge wote wa EALA.
“Raila alikuwa mwana demokrasia wa kweli. Alijitolea maisha yake yote kupigania haki, usawa na maendeleo ya watu wake. Hata katika changamoto kubwa, aliweka mbele maslahi ya taifa kuliko binafsi. Huu ndio moyo wa uongozi wa kweli,” alisema Makame.
Akizungumzia uhusiano wa Raila na Tanzania, Makame alisema historia inaonesha kuwa uhusiano wa familia ya Odinga na Tanzania ni wa muda mrefu na wa kipekee tangu enzi za kupigania uhuru.
“Raila na kaka yake, Dkt. Oburu Odinga, walikuja Tanzania mwaka 1962 wakiwa vijana wadogo, wakikimbia ukoloni wa Uingereza nchini Kenya. Walipokelewa jijini Dar es Salaam na aliyekuwa Katibu Mkuu wa TANU, Oscar Kambona, na kupelekwa kwa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, ambaye aliwapatia pasi za kusafiria za Tanganyika ili waweze kusoma nje ya nchi. Huo ndiyo mwanzo wa urafiki wa kudumu kati ya familia ya Odinga na taifa la Tanzania,” alisimulia Makame.
Makame aliendelea kueleza kuwa Raila aliendelea kudumisha uhusiano huo wa kihistoria hadi uhai wake wa mwisho.
“Mwezi Juni mwaka huu (2025), Raila alitembelea Tanzania kwa ajili ya harusi ya mtangazaji wa Star TV, Edwin Odemba. Alikuja licha ya uchovu na ratiba ngumu, akionesha namna alivyojali urafiki na watu wa Tanzania. Huo ndio utu wake — mtu aliyegusa maisha ya kila mmoja, awe kiongozi au mwananchi wa kawaida,” alisema Makame.
Mbunge huyo aliongeza kuwa Raila alikuwa rafiki wa karibu wa viongozi wa Tanzania, hasa hayati Dkt. John Pombe Magufuli, akisema uhusiano wao ulikuwa wa kindugu na wa kuheshimiana.
“Raila alikuwa karibu sana na Rais Magufuli. Walikutana mara nyingi, ndani na nje ya nchi. Waliunganishwa na imani katika maendeleo ya Afrika kupitia umoja, uwajibikaji na uzalendo,” alisema.
Akizungumzia mchango wa Raila katika siasa za Afrika Mashariki, Makame alisema kiongozi huyo aliweka msingi wa kuimarisha ushirikiano wa kikanda na alikuwa sauti muhimu katika kuhimiza Afrika kujitazama kama moja.
“Raila alikuwa Pan-Africanist wa kweli. Aliamini Afrika haiwezi kusimama ikiwa imegawanyika. Alipigania kuondoa mipaka ya kikoloni na kujenga bara lenye umoja, lenye sauti moja duniani,” alisema Makame.
Makame aliwataka viongozi wa Afrika Mashariki kuiga mfano wa Raila kwa kutilia mkazo umoja, amani na maslahi ya wananchi.
“Raila ametufundisha kuwa uongozi si heshima ya cheo, bali ni huduma kwa watu. Tumuige katika unyenyekevu, uthubutu na upendo wake kwa wananchi. Afrika imepoteza nguzo muhimu ya uongozi wa kizalendo,” alihitimisha Makame kwa huzuni.
Kikao hicho kiliongozwa na Spika wa EALA, Joseph Ntakirutimana, ambapo wabunge walitoa salamu za rambirambi kwa familia ya Raila Odinga na wananchi wa Kenya, wakimtaja kama “nguzo ya demokrasia, mtetezi wa haki, na rafiki wa kudumu wa Tanzania.”





0 Comments:
Post a Comment