Tanga, Tanzania – Wanafunzi wa Shule ya Msingi Kazita iliyopo Wilayani Muheza, mkoani Tanga, wamefanya ziara ya mafunzo kwa vitendo katika Mapango ya kihistoria ya Amboni, wakiongozwa na Mwalimu wao maarufu, Jao Kalesi – anayefahamika kwa jina la kisanii Mwl. Pawa.
Ziara hiyo imelenga kuwawezesha wanafunzi hao kupata maarifa ya moja kwa moja kuhusu historia ya Mapango ya Amboni, urithi wa utamaduni wa Taifa, harakati za kupigania uhuru, pamoja na umuhimu wa uhifadhi wa mazingira na utalii endelevu.
Akizungumza katika ziara hiyo, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Huduma za Utalii na Masoko kutoka Mamlaka ya Hifadhi ya Eneo la Ngorongoro (NCAA), Mariam Kobelo, aliwapongeza walimu wa Shule ya Kazita kwa kuchukua hatua ya kuwaelimisha wanafunzi kwa njia ya vitendo, akisisitiza kuwa juhudi hizo zinachangia kuandaa kizazi chenye uelewa wa kutunza urithi wa Taifa.
“Natoa pongezi za dhati kwa Mwl. Kalesi kwa ubunifu wa kutumia muziki katika ufundishaji, ikiwemo kutumia wimbo maarufu wa msanii Mbosso 'Pawa' kama chombo cha kuwahamasisha wanafunzi kujifunza kwa ari na kwa njia bunifu. Hii ni njia ya kipekee inayowafanya wanafunzi kushiriki kikamilifu katika kujifunza,” alisema Kobelo.
Kwa upande wake, Mwalimu Jao Kalesi alieleza dhamira yake ya kuendelea kushirikiana na walimu wenzake kutangaza Mapango ya Amboni kama eneo muhimu la kujifunzia historia na utamaduni, huku akiomba taasisi nyingine za elimu kufuata mfano huo.
Naye Afisa Uhifadhi Daraja la Pili na Mkuu wa Mapango ya Amboni, Ramadhan Rashid, alieleza kuwa katika mwaka wa fedha 2024/2025, mapango hayo yamepokea jumla ya wageni 19,743 na kuingiza zaidi ya shilingi milioni 40, akionyesha mafanikio ya kiuchumi yanayotokana na utalii wa ndani na nje ya nchi.
Kwa niaba ya wanafunzi wenzake, Juma Omari Mchevu – mwanafunzi wa Shule ya Msingi Kazita – aliishukuru NCAA kwa fursa waliyopewa ya kutembelea mapango hayo, na kuwasihi wazazi kuhakikisha watoto wao wanapata nafasi ya kujifunza kwa njia ya ziara za elimu.
Mapango ya Amboni, ambayo ni mojawapo ya vivutio muhimu vya urithi wa Taifa, vinasimamiwa na Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA). Mamlaka hiyo inaendelea kuboresha miundombinu ya utalii ili kuhamasisha wageni wa ndani na nje kutembelea eneo hilo lenye historia ya kipekee.








0 Comments:
Post a Comment